Mahakama ya Kanisa Katoliki

Historia fupi ya uanzishwaji wake.
Mambo karibu yote unayoyaona katika Kanisa yana asili yake ama katika Biblia, Mafundisho ya Mababa wenye mamlaka katika Kanisa (Magisterium), au mapokeo ya Kanisa (Tradition).

BibliaTakatifu
1Kor 6:1-6
Anathubutuje mmoja wenu kumshtaki ndugu muumini mbele ya mahakama ya watu wasiomjua Mungu badala ya kumshtaki mbele ya watu wa Mungu ? .....Aibu kwenu! Ndiyo kusema hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye hekima kiasi cha kuweza kutatua tatizo kati ya ndugu waumini? Badala yake, kweli imekuwa mtindo ndugu kumpeleka ndugu yake mahakamani, tena mbele ya mahakimu wasioamini.
Mwaka 197, Baba wa Kanisa Tertullian akiandika kuwatetea wakristo waliokuwa wanateswa, (apology) anawakumbusha watawala wa Kirumi waliokuwa wanawatesa wakristo tena kwa kusingiziwa tu, kwamba watu hawa ni wema tena wana mahakama zao nzuri wanaamua mambo yao vizuri ambayo ninyi yanawaletea magomvi. Anawashauri waige mfumo wa mahakama zao ambazo ni nzuri.
Didascalia  ni mkusanyo wa mafundisho ya mitume inaeleza kurasa baada ya kurasa kwamba kuhusu mfumo wa mahakama ya wakristu. Inamtaja askofu kama Hakimu mkuu wa kundi lake alilokabidhiwa na jinsi anavyotakiwa kuendesha kesi ya mtu aliyesingiziwa, jinsi ambavyo  hatakiwi kupokea rushwa, asiwe na upendeleo kwa watu wenye kipato na asidharau wala kuwaonea maskini katika maamuzi yake.
Kwa kifupi mahakama za Kanisa zina historia ndefu toka kwenye Maandiko Matakatifu, mapokeo ya Kanisa mpaka leo kwenye Kitabu cha Sheria za Kanisa (Code of Canon Law 1983). 

Kwanini mahakama ndani ya Kanisa:
Kanisa ni jumuiya ya wabatizwa chini wa uongozi wa wachungaji wao. Kwenye ngazi ya jimbo mchungaji wake ni askofu wa jimbo.  Kumbe jumuiya yoyote ile inahitaji sheria ili iishi vizuri. Hebu fikiria kama kusingekuwa na sheria za barabarani kwa sababu wote ni wakristu na wataendesha magari kikristu, kuna ambao wangebaki masaa mengi barabarani.
Kumbe jumuiya yoyote isiyokuwa na sheria itaishia kuwa na fujo tu. Kitakachotawala hapo ni (life of the Jungle, survival of the fittest). Kuna hatari wa wenye nguvu kukanyaga haki za wanyonge na kuwajeruhi wengine.

Mambo yanayoshughulikiwa na mahakama za Kanisa
Kanisa lina haki ya kutoa maamuzi (hukumu) kwa mashauri(kesi) zinahusu masuala ya kiroho au pale sheria za Kanisa zinapokiukwa. Maamuzi haya yanatolewa kupitia ngazi mbalimbali za mahakama za Kanisa.  Mahakama hizi zinaitwa Tribunals. Kuna mashauri mengi yanayoshughulikiwa na mahakama hizi ila nyingi zilizopa hapa nchini zinashughulikia sana masuala ya ndoa. 
Watu wanaleta maombi yao kwenye mahakama hizi ili mahakama ichunguze uhalali au ubatili wa ndoa zao ambazo zimekumbwa na matatizo na labda kuishi tena pamoja haiwezekani.  Ndio maana wengi wanaziita mahakama hizi kuwa ni mahakama za kesi za ndoa.

Ngazi  za mahakama za Kanisa.

1.  Mahakama ya mwanzo
Kila jimbo linatakiwa liwe na mahakama yake ya mwanzo kisheria. Askofu wa jimbo husika ndiye hakimu mkuu wa mahakama hiyo. Lakini kwa kuwa askofu ana kazi nyingi za kichungaji basi kwa kawaida anawachagua mahakimu kadhaa ambao wataongozwa na hakimu kiongozi anayeitwa Judicial vicar (wakili wa Askofu upande wa sheria).
Anatakiwa awe Mkleri (padri) mwenye Licentiate (masters) au (Ph. D) katika sheria za Kanisa. Na katika jimbo letu la Tanga, mimi ndiye Judicial vicar. Kutokana na uhaba wa wataalamu wa sheria za Kanisa, baadhi ya majimbo yanaungana na kufanya mahakama moja ya kimajimbo, na maaskofu wa majimbo hayo wanamchagua mmoja wao awe ndiye hakimu mkuu na mwangalizi wa mahakama hiyo. 
Mahakama hii inaweza kuwa na mahakimu wengi, na wahudumu wengine wa mahakama kadiri ya sheria za Kanisa, au inaweza kuwa ya hakimu mmoja na msaidizi wake, chini ya Askofu wa jimbo ambaye ndiye anabaki kuwa hakimu na hao wahudumu ni wasaidizi wake tu.
Fahamu, muundo na kazi zake 


2.  Mahakama ya rufaa,  mahakama  ya Jimbo Kuu
Mahakama ya mwanzo inapokea kesi kutoka katika jimbo husika na wanazifanyia mchakato wa kufikia maamuzi (process), na wakishatoa hukumu yao, hawaruhusiwi kutangaza hukumu hiyo kwa wahusika mpaka ipelekwe mahakama ya ngazi ya pili, kwa mfano hapa kwetu Tanga tunapeleka Dar es Salaam kwa sababu jimbo la Tanga liko chini ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam. 
Sasa kule Dar es Salaam mahakimu nao wanaipitia ile kesi iliyotoka kwenye mahakama ya mwanzo na kama hukumu yao itawiana  na hukumu  iliyotoka mahakama ya mwanzo basi kesi itakuwa imekwisha na hukumu hiyo watakabidhiwa wahusika.

3.  Mahakama  ya  Rufaa Roman Rota
Hii ni mahakama ya rufaa ngazi ya tatu, iko chini ya Baba Mtakatifu.  Inapokea rufaa za kesi kutoka mahakama ngazi ya pili. Pia inashughulikia kesi ambazo haziwezi kufanywa katika mahakama za ngazi ya kwanza na ya pili. Kwamfano kesi zinahusu wakuu wa mashirika ya kitawa, au kesi za maraisi wa nchi, nk.


4.  Mahakama nyingine: Apostolic Signatura na Apostolic Penitentiary.
Mahakama ya Apostolic Signatura, ni mahakama ya juu kabisa katika kanisa la Roma. Ina shughulika na kesi ambazo zimewakilishwa kwa Baba Mtakatifu mwenyewe na yeye anateua makardinali watano kuifanya kwa niaba yake.

Ila ni kesi nadra sana za namna hii. Mahakama ya Apostolic Penitentiary inajihusisha na masuala ya ndani, yaani internal forum. Zote mbili zinafanya kazi kwa niaba ya Baba Mtakatifu.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU