Ask.Nkwande: Ubabe na ushabiki hautatatua kero Zanzibar


·      Asema mazungumzo yangefaa kabla ya uchaguzi

Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda Mhashamu Renatus Nkwande    
BAADA ya Zanzibar kupata serikali mpya inayoongozwa na Rais Mohamed Ali Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufuatia uchaguzi wa marudio wa Machi 20 mwaka huu, na Chama kikuu cha upinzani visiwani humo CUF kusema hakimtambui Dkt Shein na serikali yake, Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda Mhashamu Renatus Nkwande amesema mgogoro huo ukitatuliwa kwa ushabiki na ubabe Zanzibar haitapata suluhisho na hali hiyo italeta italeta madhara kwa wananchi.

Akizungumza na gazeti Kiongozi jijini Dar es Salaam, Askofu Nkwande ameeleza kuwa, kwa sasa siasa hizo zenye mikanganyiko mbalimbali zina athari kubwa zaidi ya watu wanavyo fikiri.

Amesema kabla ya uchaguzi huo wa marudio kufanyika kulikuwa na haja ya kukaa pamoja kwa ajili ya mazungumzo ambayo kwa namna ya pekee yangesaidia kuleta hali ya utulivu visiwani humo.

“Suala hili lilipaswa lizungumziwe na kujadiliwa ili kupata suluhisho kabla ya kufanya uchaguzi huo kwani kwa kufanya uchaguzi wakati hakujafanyika mazungumzo yenye kuhusisha vyama vilivyosusia uchaguzi huo ni ubabe na ushabiki usiyo na maana utakao waathiri watu wasiyo na hatia.

Amesema kuwa ingefaa kufanya mazungumzo kabla ya uchaguzi huo kwa ajili ya kupata mwafaka ili wakati na baada ya uchaguzi pande zote mbili ziwe tayari zimepata maridhiano na wote kushiriki uchaguzi huo kwa uhuru na haki.

Akizungumzia nini kifanyike Zanzibar kwa sasa ili kuleta suluhisho amesema ni vigumu kupata suluhisho la haraka kutokana na kila upande kuwa na msimamo mkali ambapo pengine misimamo ya aina hiyo inaweza kuleta hali ya mtafaruku na kuhatarisha amani.

Katika hatua nyingine Askofu Nkwande amesema hali tete ya kisiasa viwani Zanzibar inaweza kuathiri hata uhuru wa kuabudu baina ya waislamu na wakristo endapo serikali haitakuwa makini.

Amesema ili waamini waabudu katika makanisa yao na misikiti yao suala la amani ni muhimu kuwepo na kulindwa kuwawezesha waamini hao kutimiza wajibu wao kiroho bila ya bughudha yoyote.

Tangu kuibuka kwa mgogoro wa kisiasa Zanzibar watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakisema mwarobaini wa mgogoro huo kwa kutumia jitihada za ndani, ufanywe na Rais Magufuli baada ya jitihada za viongozi wa kisiasa visiwani kukwama.

CUF wenyewe walitaka maridhiano kabla ya kurudia uchaguzi lakini mbinu hizo zilikwama na kuwasukuma wadau mbalimbali kumtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakt. John Magufuli awashawishi Wazanzibar kufanya maridhiano  ambapo wanasheria waliyasema haya yafuatayo;

Mwanaseria Mkuu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alisema Rais Magufuli hana mamlaka ya kikatiba ya kuingilia masuala ya Zanzibar ukiwamo uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20.

Alisema; “Katiba ya Zanzibar si ya Muungano, masuala ya ulinzi na usalama ndiyo ya Muungano na ndiyo sababu ulinzi umeimarishwa visiwani humo kuhakikisha nchi hiyo inakuwa salama."

Alitoa kauli hiyo wakati akifafanua mambo mbalimbali yaliyozungumzwa na wabunge wakati wa mjadala wa mwongozo wa mpango wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/17 na Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uwepo wa Serikali mbili. Hizi Serikali uwepo wake ni Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar. Ukisoma Ibara ya nne ya Katiba si tu kwamba inaweka mgawanyo wa madaraka katika mihimili mitatu ya Dola, bali inaweka mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar,” alieleza Masaju

Jaji Lubuva
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Jaji Damiani Lubuva alieleza kuwa wanaosema Rais anapaswa kuingilia kati masuala ya uchaguzi iwe Tanzania bara ama Zanzibar wanafanya makosa, kwani kwa namna yoyote Rais hana mamlaka hayo na hivyo hawezi kuingilia maamuzi ya tume hizo.

“Unaposikia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano aingilie hilo suala la uchaguzi wa Zanzibar, yeye kwa kweli hana mamlaka kabisa. Pili ni kama kujikanganya, huku unasema tuwe na tume huru isiyoingiliwa halafu huku unasema aingilie kati maamuzi ya tume” alisema Jaji Lubuva.

Tangu wakati huo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd na marais wa zamani wa Zanzibar, Dk Salmin Amour, Ali Hassan Mwinyi na Amani Karume wamekuwa kwenye mazungumzo ambayo hayakuzaa mwafaka.

Nini Kifanyike
Askofu Nkwande amesema pamoja na kwamba uchaguzi umeishapita ipo haja kwa serikali ya Zanzibar kukaa na vyama vilivyosusia uchaguzi huo hasa chama kikuu cha upinzani (CUF) kwa ajili ya maridhiano yatakayoleta amani visiwani humo.

Amesema hali ilivyo si ya kukaa kimya bali mbinu mbalimbali za maridhiano zinapaswa kufanyika na kusisitiza kuwa viongozi wa siasa wanapaswa kuangalia maslahi yawaliowengi na suala la amani lipewe kipaumbele cha kwanza.

“Hata kama kuna wanaoamini serikali na wasiyoamini serikali lazima mbinu zifanyike za kuleta suluhisho.
Kama ni maandamano ya amani yafanyike na sauti za wanaoandamana zisikilizwe na pia wanaoandamana wasikilize sauti za wanaoiamini na kuikubali serikali.

Amesema wanapaswa kuketi chini wajadiliane na kufikia mwafaka kwani bila hivyo mambo yanaweza kuharibika na kuathiri maisha ya watu kwa pande zote mbili za bara na visiwani,” amesema.


               

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU