Wasomi kuweni wazalendo-Askofu Mapunda
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Singida Mhashamu Edward Mapunda amewaasa
wahitimu wa vyuo vyote nchini kuhakikisha kuwa elimu wanayoipata katika ujuzi
mbalimbali inawasaidia watanzania wote kwa ujumla, hasa kujali utu wa binadamu
na kumkomboa katika changamoto zake.
Askofu Mapunda amesema kuwa jambo la msingi wanalopaswa
kuzingatia wasomi hao ni kuhakikisha elimu wanayopata vyuoni inajenga heshima kwa wanadamu wote, utu na
iwasaidie watu kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha.
Askofu Mapunda amesema hayo hivi karibuni katika mahafali
ya tano ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Augustino Jordan kilichopo mkoani
morogoro, ambapo jumla ya wahitimu 1,305 wamehitimu katika kozi mbalimbali.
Askofu Mapunda amesisitiza kuwa wahitimu wanapaswa
kuzingatia elimu wanayopewa ili iwe chachu ya kuwatumikia watanzania bila
kutanguliza ubinafsi na iondoe ukoma wa watu.
“Elimu yetu itusaidie kuwatumikia watanzania, tusijitahidi
tu kukesha usiku kucha kusoma tu bila kujali mahitaji ya mtanzania, sasa kama
sisi tunasoma halafu watu wanaendelea kuwa wakoma haina maana. Kusoma kwetu
kunatusaidia nini kama hatujibidiishi kuondoa umasikini, magonjwa na ujinga?”
amehoji Askofu Mapunda.
Askofu Mapunda ametoa wito kwa wahitimu kujiepusha na
masuala ya rushwa na ufisadi miongoni mwao, kwa sababu rushwa ni adui wa haki
na hata maandiko matakatifu yanasema wala rushwa hawataingia mbinguni kwa
sababu wana mikono michafu.
Hata hivyo wahitimu hao wameshauriwa kutumia elimu zao kwa
faida ya wote ambapo wanapaswa kutafakari kuwa taaluma zao ni kwa maendeleo ya
taifa, si kwa ajili ya kujimilikishia mali, wasitumie vyeo vyao kwa ubinafsi na
kusababisha mafarakano ya kuporomosha haki na kuhatarisha amani.
Wakati huohuo, Askofu Mapunda amesema kuwa kazi ya wasomi
ni kutenda haki na kujenga dunia ya wenye haki na watu wenye amani ambapo sifa
ya mtu msomi ni kusema ukweli na kusimamia maslahi ya wengine, japo hali hii
inagubikwa na mfumo wa ubinafsi na rushwa na kusababisha kasoro ndani ya taifa.
“Nawaalika ndugu zangu tuliobahatika kwenda shule
tuyashike haya ili elimu yetu iwe na faida, kama huyu msomi aliyesoma ni
mwizimwizi tu, analiibia taifa lake elimu hii ni ya nini? kama hana desturi ya
kusema ukweli ni muongomuongo tu, elimu hiyo ni ya nini? tujibiidishe kumpa
Mungu utukufu,” amesema Askofu Mapunda.
Aidha kiongozi huyo wa kiroho amewaasa wahitimu kuwa
waadilifu na watiifu katika nafasi mbalimbali watakazofanyia kazi, ikiwa ni
pamoja na kuitii serikali kwa lengo la kuwatumikia watanzania katika utatuaji
wa changamoto zao kwa maendeleo ya taifa.
Comments
Post a Comment