‘KUTOSALI ROZARI NI KUKOSA DIRA’

Na Doreen Aloyce, Dodoma

PAROKO wa Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Kizota Jimbo Kuu Katoliki Dodoma  Padri Joby Tharayil amewataka waamini nchini kusali Rozari Takatifu  kwa Imani kuu, jambo ambalo litawasaidia kuishi maisha ya amani huku  shetani akikosa nafasi kwenye familia zao.
Ameyasema hayo katika adhimisho la Misa ya kuadhimisha mwezi wa Rozari Takatifu yaliyoanza kwa maandamano na mafundisho ya jumuiya hadi jumuiya iliyoenda sambamba na uzinduzi wa ofisi mpya ya Parokia.
Padri Joby amesema kuwa ni jambo la kumshukuru Mungu kuadhimisha mwezi wa Rozari katika Parokia yake kwani tangu mafundisho yaanze kutolewa kuhusu umuhimu wa kusali Rozari waamini wamekuwa na mwitikio mkubwa huku kwa kiasi kikubwa wakitambua umuhimu wake tofauti na hapo awali.
“Katika Parokia yetu tuliweka mikakati ya kuwafundisha waamini wetu juu ya umuhimu wa kusali Rozari kwa Imani japo ilikuwa kazi ngumu kwani wengi wanasali kwa mazoea na wengine hawajui kabisa, ila tuliendelea kuwafundisha kuanzia watoto mpaka wazee na kweli tumefanikiwa wanajua kusali na wametambua umuhimu wake, nawaomba tusiwe wavivu, “ amesema Paroko Joby.
“Wapo waamini ambao wamekuwa wakisali  Rozari Takatifu kwa mazoea huku wakiwaza mambo yao mengine ya kifamilia na changamoto za maisha  kwa sababu ya kutojua umuhimu wake jambo ambalo linasababisha kuendelea kuangamizwa na Shetani.
Pale waamini wanaposali Rozari Takatifu kwa Imani wanajifunika na ulinzi wa Mungu kwenye maisha yao, shetani hapati nafasi magonjwa na mikosi havitawafika bali watafanikiwa kwenye shughuli zao,wenye shida zitatatuliwa  na kuendelea kutafakari maisha ya baadaye.”
Vile vile Ameongeza kuwa kwa sasa Dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, watu wanapenda mambo ya kidunia zaidi kuliko Mungu na matokeo yake Imani yao kuwa haba na kuanza kutangatanga kwenye madhehebu mengine hata kwenda kwa waganga wa kienyeji na hatimaye kuangamia.
Amewataka waamini kutambua kuwa pale wanapojikita kumuomba Mungu wanatengeneza maisha mazuri ya mbinguni, hivyo wajiepushe na mambo ya kidunia kwa kutaka kupata vitu ambavyo havitawafikisha popote.
Katika hatua nyingine amewashukuru waamini wa parokia hiyo kwa ushirikiano waliouonesha kukamilisha Ofisi ya Parokia yenye vyumba vitano  iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 35 ndani ya miezi mitatu.
“Parokia hii ina miaka miwili tangu kuanzishwa kwake lakini tumekuwa na mafanikio makubwa kupitia umoja wa waamini kuanzia watoto hadi wazee  ambao wamekuwa wakijitoa kwa moyo wote  ukilinganisha kwamba ni familia 586 wanafanya kazi, kama familia moja nawaomba waendelee na jitihada hizo,” amesema Paroko Joby.

Hata hivyo amesema wana mpango wa kujenga Kanisa kubwa la kihistoria pamoja na kuanzisha Miradi mbalimbali ikiwemo ya maduka kwani Kanisa lililopo kwa sasa ni dogo kadri parokia inavyozidi kukua.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI