ASKOFU MAPUNDA AWATAKA WAAMINI KUTOTEGEMEA WAFADHILI
|
ASKOFU wa
Jimbo Katoliki Singida Mhashamu Edward Mapunda amewataka wakatoliki nchini
kuondokana na tabia ya kutegemea wafadhili wakati wa utekelezaji na
ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka kujitegemea zaidi.
Askofu Mapunda ametoa wito huo kwenye
misa takatifu aliyoiongoza wakati wa maadhimisho ya sherehe za Jubilei ya miaka
50 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni iliyofanyika katika
viwanja vya Kanisa la Parokia hiyo mjini Manyoni.
Amesisitiza kwamba suala la kujitegemea
halina budi kupatiwa kipaumbele katika shughuli za kukamilisha ujenzi wa
majengo ya makanisa pamoja na vigango.
Akifafanua zaidi Askofu Mapunda ameweka
bayana kuwa jukumu la kukamilisha ujenzi wa makanisa ni la waamini wenyewe na
wenye moyo ambapo hata hivyo amewatoa hofu waamini wa Manyoni kwa kuweka wazi
kuwa anaamini kabisa waamini wa Manyoni ni waumini wenye moyo wa dhati wa
kukamilisha majengo hayo.
Hata hivyo, Askofu Mapunda
amewatahadharisha waamini wa Jimbo hilo kwamba suala la kujitegemea lina
umuhimu wake na kwa hali hiyo hawana ujanja wa kulikwepa jukumu hilo la
kuondokana na utegemezi kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili mapadri
zikiwemo za kutokuwa na vyombo vya usafiri.
Naye Paroko wa Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, Jimbo Katoliki
Singida, Padri Thomasi Wambura amesema
mwaka jana ulikuwa mwaka wa Jubilei ya Miaka 100 wa Mapadri Tanzania, mwaka huu nao
wanaadhimisha miaka 50 ya Jubilei ya Parokia yao na mwaka ujao wa 2018
wataadhimisha Jubilei ya miaka 150 tangu ukristo ulipoingia nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Padri Wambura waamini
wote wana wajibu wa kuyatekeleza yale yote waliyoaswa na Askofu kama mchungaji
wao Mkuu, lakini hakusita kusisitiza kwamba wajibu walionao ni kuyatekeleza
yale waliyoyapata katika ukrito.
Kwa upande wao baadhi ya waamini wa
Kanisa hilo akiwemo Elizabeth Mkyalu
wameshauri kwamba fedha zilizochangwa na waamini hazina budi kuanza
shughuli zilizokusudiwa za ujenzi wa majengo hayo huku wakionya tabia ya
kusubiri wafadhili kwamba kwa namna moja au nyingine hukwamisha miradi
iliyoanzishwa pale wanapojitoa au kutochangia.
Comments
Post a Comment