TEC, Kwaya ya Vijana Michungwani kuunusuru Muziki Mtakatifu
“MUZIKI wetu ni lazima uwe mtakatifu kwa sababu ni sehemu
ya liturujia. Tangu zamani mafundisho mengi yamewekwa kwenye muziki. Hii
itukumbushe kuwa sisi tumeitwa na kutumwa kuinjilisha na kutakatifuza, tuweze
kuwagusa watu ili wamgeukie Mungu. Lakini kwa sasa uwanja wa muziki mtakatifu
umevamiwa sana, ikiwa ni mbinu za shetani kushambulia yaliyo mema. Lazima vita
hii tuishinde”.
Ni maneno aliyowahi kusema Askofu
Salutaris Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, na Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia
TEC.
Kwa muda mrefu sasa Gazeti Kiongozi
limekuwa likichapisha makala mbalimbali kuhusu muziki mtakatifu, ili kuendeleza
tunu hizo ya pekee kwa Kanisa, na kuwakumbusha watunzi wa kileo kufuata
miongozo inayotoa mwelekeo sahihi wa utume wa uimbaji. Moja ya miongozo hiyo ni
Hati ya Liturujia (Sacrosanctum Concilium), ambayo ni maelekezo yaliyotolewa na
mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani.
Aidha, katika toleo lililopita
tuliangazia sababu za kwa nini waamini wanapenda nyimbo za zamani iwe katika
Adhimisho la Misa Takatifu au kwa kusikiliza. Nilitaja baadhi ya sababu kuwa ni
Kushirikishwa kikamilifu, kwamba kazi ya muziki mtakatifu ni kuwasaidia waamini
wasali vizuri, hii haina maana kwamba waamini wawe mabubu tu katika
maadhimisho. Bali washiriki kuitikia, kuimba nyimbo wanazozifahamu au hata zile
wasizofahamu ili mradi ziwe zinashikika kirahisi.
Pili Muziki wenye sala na tafakari,
Moja ya mambo ambayo watunzi wa mwanzo hapa nchini walifaulu basi ni kutunga
wakiwa katika hali ya sala.
Kumbe, kutokana na sababu mbalimbali
na maombi ya wadau wengi wa muziki mtakatifu, kuna kila sababu ya kuhifadhi
nyimbo zile za zamani ili ziwe kama hazina, funzo au darasa, na ukumbusho wa
mchango mkubwa uliofanywa na watunzi wa zamani ambao kwa kiasi kikubwa
walijitahidi kutunga wakiwa katika hali ya sala na tafakari. Pia iwe msaada kwa
watunzi wanaochipukia ili wajifunze mema yaliyofanywa na watunzi waliopita.
Kutokana na hitaji hilo, Kurugenzi ya
Mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeanza mchakato
wa kuzikusanya nyimbo hizo za zamani zenye mafundisho, kisha kuzirekodi katika
mfumo wa DVD ambapo waamini wataweza kujipatia kwa urahisi pale wanapohitaji.
Na kwa kuanza, Kurugenzi hiyo imeandaa
mkusanyiko wa nyimbo za zamani za Mama Bikira Maria, katika DVD iliyoimbwa na
Kwaya ya Vijana ya Mtakatifu Cesilia, Parokia ya Mtakatifu Antony Maria Claret,
Michungwani-Kimara, Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam. Albamu hiyo yenye
mkusanyiko wa nyimbo 10 inayoitwa NIONGOZE MAMA WA YESU inazinduliwa Jumapili
ya 33 A, yaani Novemba 19, 2017 ambapo waamini wote nchini wataweza kuipata kwa
urahisi na kuenzi tunu za muziki mtakatifu.
Zoezi la ukusanyaji wa nyimbo za
zamani ni endelevu. Kurugenzi, ikishauriana na wadau wa muziki mtakatifu,
wanaliturujia na wote wenye mapenzi mema, itaendelea kuzikusanya nyimbo za
vipindi mbalimbali vya Kanisa, kisha kuzirekodi kwa ruhusa maalum, ili
kukabiliana na changamoto ya kupotea kwa nyimbo zile zilizopendwa, ambazo kwa
sasa hazipewi kipaumbele katika maadhimisho mbalimbali.
Hii ni fursa kwa waamini na wadau
wote wa muziki mtakatifu, kujipatia albamu hiyo kisha kuitazama na kutafakari
zawadi ya Mama Bikira Maria katika maisha yetu ya kikristo hasa katika familia
zetu.
Kwaya ya Vijana ya Mtakatifu Cesilia
Michungwani, licha ya kuundwa na vijana, imekuwa ikijitahidi kuenzi nyimbo za
zamani katika maadhimisho ya Misa Takatifu, hali inayowafanya waamini wajisikie
kuwa sehemu ya Misa kwani inawawezesha kushiriki kikamilifu kuziimba nyimbo
hizo. Hii ni moja ya sababu iliyofanya
ichaguliwe kushiriki katika kurekodi albamu hiyo, huku sababu nyingine ikiwa ni
namna wanavyofuata maelekezo ya Liturujia katika Misa.
Haya ni miongoni mwa matunda ya
uongozi thabiti, ushirikiano na hamasa ya Paroko wa Parokia ya Mt. Antony Maria
Claret, Padri Wolfgang Silayo CMF, ambaye amekuwa daima mdau na mfuatiliaji wa
nyimbo za zamani zinazoimbika kwa urahisi na waamini wote, zinazomuingiza
muumini katika tafakari ya kina, huku maneno yake yakiwa ni mafundisho tosha.
Uzinduzi wa albamu hii ndiyo mwanzo
wa kuendeleza jitihada za wadau wa muziki mtakatifu nchini, za kuhifadhi vizuri
matini na rekodi za muziki mtakatifu zilizofanywa na watangulizi wa muziki huo.
Kwa wauzaji wa jumla na reja reja, au
kama unataka kuwa wakala majimboni, piga 0657835343
Comments
Post a Comment