Kardinali Pengo awapongeza waamini Kiwalani
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es
Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewapongeza waamini, viongozi na
watu binafsi wa Parokia
ya Mt. Kamili Yombo Kiwalani kwa kufanikisha ujenzi wa
nyumba mpya na ya
kisasa ya mapadri
parokiani hapo.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa nyumba hiyo, Kardinali Pengo amesema yeye
binafsi alitumia miezi 6 kukamilisha
ujenzi wa gereji yake ya kuhifadhia
magari, lakini anashangaa moyo wa
waamini wa Kiwalani wa kujitoa kuijenga nyumba
nzuri na ya ghorofa
kwa muda mfupi.
Amewapongeza
wote walioshiriki kwa hali na mali katika mchakato mzima mpaka uzinduzi wa
nyumba ya mapadri, huku akiwaasa kuendelea na moyo wa upendo na kumshirikisha
Mwenyezi Mungu.
Kardinali Pengo
ametoa vyeti kwa watu binafsi waliochangia kukamilika kwa nyumba hiyo
kwa niaba ya viongozi wa parokia
ambapo vyeti vingine vitatolewa hapo
baadaye kwa makundi mbalimbali.
Awali,
katika mahubili yake kwa vijana waliopokea Sakramenti ya kipaimara, Kardinali
Pengo amewataka vijana hao
kumtangaza Kristo ya kuwa amefufuka kweli.
“Mkristo yeyote anapokuwa hana
Yesu kwenye moyo
wake, ni msingi mkubwa wa kuwa na
wasiwasi, hivyo maisha yenu yote
yaongozwe na kulindwa na ukweli kwamba
Yesu yupo rohoni
mwenu kwa njia ya roho
anayetenda kazi,” amesema.
Mwenyekiti
wa parokia hiyo, Robert Bamwebuga na viongozi wa walei
parokia wamemshukuru Kardinali Pengo
kwa kuitikia wito wa
kufika parokiani hapo kwa ajili
ya kutoa sakramenti ya kipaimara kwa
vijana 109 pia kuzindua nyumba ya mapadri.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Kamati
ndogo ya ujenzi ambayo ilisimamia
ujenzi wa nyumba hiyo, Justus Bashara, amesema nyumba hiyo
imegharimu takribani shilingi
Mil. 187 mpaka kukamilika kwake. Amewashukuru wote waliojitoa kwa ajili
ya ujenzi huo.
Paroko wa parokia
ya Mt. Kamili padri Festo Liheta
ametoa shukrani za dhati
kwa waamini wote tangu
mwanzo wa ujenzi
hadi kukamilika kwake, pia amemshukuru
Askofu Mkuu Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo kwa kufika
parokiani hapo.
Comments
Post a Comment