Kongamano la Ekaristi Takatifu Kanda ya Mashariki kufanyika Zanzibar 2019
MAASKOFU wa Kanisa Katoliki Kanda ya
Mashariki nchini wamesema ili kuendeleza Ibada na heshima kwa Ekaristi Takatifu
wameridhia kufanya Kongamano la Ekaristi Takatifu kila baada ya miaka mitatu
ambapo mwaka 2019 Kongamano hilo litafanyika katika Jimbo Katoliki Zanzibar.
Wamesema hayo katika kilele cha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kanda ya
Mashariki lililofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Msimbazi, Jimbo Kuu
Katoliki Dar es Salaam.
Akisoma maazimio ya Kongamano hilo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar
es Salaam Mwadhama Polycap Kardinali Pengo amesema kuwa, Kongamano hilo la
Ekaristi Takatifu limekuwa ni neema na baraka kwa waamini wote walioshiriki
Kongamano hilo na Kanisa kwa ujumla.
“Katika kuendeleza neema na baraka
hizo za Mungu kwa taifa sisi Maaskofu wa
Kanda ya Mashariki baada ya kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa waamini,
makleri na wanakongamano wote, tumekubaliana tuwe na Adhimisho la Kongamano la
Ekaristi katika Kanda ya Mashariki kila baada ya miaka mitatu.
Kongamano la pili la Ekaristi Takatifu
katika Kanda ya Mashariki litafanyika Jimbo Katoliki Zanzibar Juni 2019.
Tumepanga 2019 badala ya 2020 kwasababu mwaka 2020 kutakuwa na vuguvugu za
Uchaguzi Mkuu katika taifa letu,” amesema Kardinali Pengo.
Aidha, Ili kuendeleza ibada na heshima kwa Ekaristi Takatifu maaskofu hao
wameazimia kuwepo na kuendelezwa kwa makanisa ya kuabudu daima Ekaristi
Takataifu (Perpetual Adoration chapels) ambamo Ekaristi Takatifu itawekwa na
kuabudiwa kwa masaa 24 kila siku.
Makanisa hayo yajengwe kwenye majimbo yote ya Kanda ya Mashariki na
waamini wanaombwa kujitokeza kwa wingi kwenda kuabudu Ekaristi Takatifu
ili kujichotea neema ya ukombozi.
Wameazimia kuwa, ili kuendeleza malezi ya kiimani kwa watoto na kuwezesha
kutambua na kuthamini nafasi ya Ekarist i Takatifu katika maisha ya kikristo
washiriki wa kongamano hilo wameazimia kuzifanya familia na parokia zao kuwa
vituo vya katekesi na mafundisho endelevu na kina ya imani kuhusu Ekaristi Takatifu kwa watoto
wao.
“Tunatoa mwito kwa mapadri, watawa, makatekista, wazazi na walezi wote
kusitawisha utume wa Utoto Mtakatifu na kuwawezesha watoto wote kuwa washiriki
wa Shirika hilo la Utoto Mtakatifu
ambalo ni chombo muhimu cha kukuza imani na moyo wa umisisonari kwa watoto
wetu.
Wanandoa wanaojiandaa kupokea sakramenti ya ndoa na wale ambao tayari
wameshaipokea Sakramenti hiyo wapewe katekesi na mafundisho ya kina kuhusu
Ekaristi Takatifu ili watambue kuwa furaha na upendo wa ndoa zao zinategemea
moja kwa moja muungano wao na Yesu wa Ekaristi. Bila Ekaristi Takatifu hakuna
uhai wa kimungu ndani ya familia,” amesisitiza Kardinali Pengo.
Ili kuwezesha waamini kuwa na ibada za mara kwa mara za Ekaristi Takatifu,
parokia zote katika Kanda ya mashariki zinapaswa kuwa na utaratibu wa kufanya
ibada na kuabudu Ekaristi Takatifu mara moja kwa juma. Waamini wajitokeze kwa
wingi kushiri ibada hizo.
Kilele cha Kongamano hilo kilikuwa cha namna yake ambapo palikuwa na
maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo Kuu Katoliki
Dar es Salaam ambapo Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar aliongoza
maandamano kutoka Parokia ya Magomeni hadi Msimbazi, Askofu Anthoni Banzi wa
Jimbo Katoliki Tanga aliongoza maandamano ya Ekaristi Kutoka Kanisa la
Mtakatifu Josefu ( Posta ) hadi Msimbazi.
Askofu wa Jimbo Katoliki Mahenge Mhashamu Agapiti Ndorobo aliongoza
maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka Parokia ya Buguruni hadi Msimbazi na
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Euzebius Nzigilwa
aliongoza maandamao ya Ekaristi Takatifu kutoka Parokia ya Kurasini hadi
Msimbazi ambapo waamini wote walikutana kwa Adhimisho la kilele cha Kongamano
hilo.
Kongamano hilo lilianza November 10-12 mwaka huu lilihudhuriwa na maelfu
ya waamini wakiwemo maaskofu, mapadri na waamini walei kutoka majimbo
yanayounda Kanda hiyo ya Mashariki ambayo ni Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam,
Ifakara, Tanga, Morogoro, Zanzibar na Mahenge. Mkuu wa Kanda hiyo ya Mashariki
ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo.
Comments
Post a Comment