Yesu hana mbadala wake: Askofu Nyaisonga
Padri
Albert Twenya wa Jimbo Katoliki Sumbawanga na Sista Priscilla Ndegeya wa
shirika la masista wa Maria Mtakatifu Malkia wa Afrika wamezikwa Novemba 9
mwaka huu, huku wakiacha simanzi kubwa wa waamini wa Jimbo hilo.
Akiongoza ibada ya mazishi
iliyotanguliwa na Misa Takatifu ya kuwaombea marehemu hao, Askofu Gervasi
Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda amempa
pole Askofu Damian Kyaruzi, mapadri, watawa na waamini wa Jimbo Katoliki
Sumbawanga kwa msiba huo akiwataka kuhuzunika kwa imani wakipokea mapenzi ya
Mungu kwa unyenyekevu.
“Yesu hana mbadala wake na hivyo kila
tunachokifanya katika imani yetu tuzidi kushikamana naye tukiwa hapa duniani
kwa kufuasa mafundisho ya Mama Kanisa na kuiishi imani kila mmoja kwa nafasi
yake,” amesema Askofu Nyaisonga.
Amewataka waamini kuiishi misingi ya
Imani ya Kanisa Katoliki na kufuata mwongozo wa kiliturujia kadiri ya
mafundisho ya Mama Kanisa kwani Yesu Kristo hana mbadala wake .
Marehemu Padri Albert Twenya amefariki dunia
Novemba 7 mwaka huu mjini Sumbawanga
kutokana na maradhi ya mda mrefu akiwa na miaka 59 ya kuzaliwa na miaka 34 ya upadri.
Sista Priscilla Ndegeya amefariki
dunia Novemba 6 mwaka huu akiwa na umri wa miaka 89 ambapo wote kwa pamoja
wamezikwa katika makaburi ya mapadri na watawa Katandala jimboni Sumbawanga.
Ibada hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na mamia ya
waamini akiwemo Askofu Damian Kyaruzi wa Jimbo Katoliki Sumbawanga na Abate
Pambo Martin Mkorwe OSB wa Abasia ya Roho Mtakatifu Mvimwa.
Raha ya milele uwape ee Bwana na
mwanga wa milele uwaangazie wapumzike kwa amani, amina!
Comments
Post a Comment