KARDINALI PENGO AZINDUA PAROKIA MPYA MISUGUSUGU.
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo amewaongoza waamini wa Misugusugu na wageni waalikwa
kutoka parokia tofauti za Jimbo hilo kwenye sherehe za kuzindua parokia mpya ya
Mt. Polycarp Misugusugu, sanjari na uzinduzi wa nyumba ya mapadri iliyojengwa
parokiani hapo pia usimikaji wa msalaba wa kumbukumbu juu ya kilima kilichopo
pembezoni mwa parokia hiyo.
Katika mahubiri yake kwenye ibada hiyo ya misa takatifu, Kardinali
Pengo amesema kuwa kwa kiburi cha Adam na Eva maisha yetu yametuwia magumu lakini
bado Mungu anatupenda kwa upendo wake mkuu kwetu, akamtuma mwanaye Yesu Kristo aje kutukomboa kupitia
kwa mama yetu Bikira Maria aliyekuwa mtii na mnyenyekevu mbele za Mungu, hivyo
kila mkristo adumu katika upendo kila wakati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Parokia hiyo mpya, Adolf Mrema amesema, ‘Ni furaha iliyopitiliza kwa
hatua tuliyoifikia kwa sababu tutakuwa na uhakika wa kufanya adhimisho la
Ekaristi Takatifu ambayo ndiyo nguvu yetu, kwani bila Ekaristi hatuwezi kufanya
chochote.’’
Aidha Mwenyekiti huyo wakati wa kusoma historia kwa Mwadhama
Kardinali Pengo amesema ukatoliki katika eneo la Misugusugu ulianza na familia
tano mwaka 1971 zikiongozwa na marehemu Mzee Nemes Daud Luzua aliyehamia katika
kijiji cha Misugusugu akitokea Matombo Morogoro. Mzee Nemes aliungana
na familia za marehemu Mzee Athanas Masenga aliyehamia toka parokia ya Lugoba,
pamoja na familia za marehemu Mzee Arbogast Matembele, Amandus Mponda na Gustav
Mtumbuka aliyehamia Misugusugu akitokea Kipatimu. Familia zote hizi tano
zilikuwa zikikutana nyumbani kwa Mzee Nemes kwa sala chini ya mti wa
mkorosho tangu mwaka 1971 na wakati huo
hapakuwa na kigango wala Jumuiya na waamini wengi katika familia hizi hawakuwa
wamebatizwa wala kufunga ndoa.
Misugusugu ilitangazwa kuwa kigango mwaka 1980 chini ya parokia
ya Tumbi/Kibaha, na sasa ni parokia rasmi na vigango vya Zogowale, Ngeta na
Makazi mapya vimewekwa chini ya parokia hii na idadi ya Kanda ni mbili
ikijumuisha jumuiya 22.
Parokia ya Mt. Polycarp inaongozwa na Paroko Joseph
Kazikunema, ambapo kwa mujibu wa taarifa, uzinduzi wa Parokia hiyo umeleta
neema kubwa ikiwemo watoto 130 kubatizwa, ndoa 27 kubarikiwa na Mapadri kutembea
nyumba kwa nyumba kuwafahamu waamini na kuamsha uhai wa imani.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na kwaya mashuhuri ya
Mwenyeheri Anwarite toka parokia ya
Makuburi, huku Mwadhama akizindua DVD mpya ya kwaya ya Mt. Polycarp Misugusugu
waliyo itoa hivi karibuni.
Na Philipo Josephat, DSM
Comments
Post a Comment