KUWENI WATU WA TOBA NA MSAMAHA: ASKOFU NZIGILWA


Na Philipo Josephat, DSM

ASKOFU Msaidizi  wa  Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa amewataka  waamini  wote kuyajongea  maisha  ya toba  na msamaha na  kufungua  vifungo  vya  visasi kwa  kumuomba  Mungu awasimamie katika maisha hayo.
Askofu  Nzigilwa  ameyasema  hayo katika mahubili kwenye adhimisho la Misa Takatifu  ya kutoa  sakramenti ya kipaimara  kwa  vijana 120 wa  parokia  ya Mt. Karoli Lwanga iliyoko  Yombo  Dovya jijini  Dar es Salaam.
“Kristo  ametutangazia ya kuwa  viwete  wanaweza  kutembea, vipofu  wapate  kuona na viziwi  wapate  kusikia kwa  uponyaji  kupitia  mwanga  wa  msamaha. Nawaomba tujenge utamaduni wa kusameheana,” amesema.
Ameongeza kuwa, mtu akimuingia  Kristo kwa   uthabiti ni lazima ataona  mabadiliko  ndani ya nafsi yake.
Amewataka waimarishwa  wa  kipaimara wawe  mabalozi  wa upendo  mahiri popote  watakapo  kwenda  kwa kuiishi  imani ya Kristo “Mkayatumie  vizuri  mapaji  ya Roho  Mtakatifu  kwa  kuiishi  na kuishika  imani, nanyi  wazazi  muwalee vizuri  watoto hawa kwa  kuwafundisha  na kuwakumbusha yaliyo  mema na  kuwashirikisha  kazi  mbalimbali za Kanisa, ’’amesema Askofu Nzigilwa.
Kwa  upande wake  Mwenyekiti   wa parokia  hiyo, Rosemary Kasongo amewaomba wazazi  na wasimamizi  wa  watoto waimarishwa waendelee kuwa  bega kwa bega  na watoto ili  wasipotee kwasababu  mara nyingi  watoto  wanapokuwa wamepokea  sakramenti  hiyo hupotea  ndani  ya  Kanisa na huonekana  pale  tu  wanapohitaji  kufunga  ndoa.
Katika  hatua nyingine  waamini  wa vigango  vya Mbutu na Ngobanya katika  Parokia  ya  Kimbiji jijini Dar es Salaam wameshindwa  kujizuia  kudondosha  machozi  baada ya  Paroko  Msaidizi wa parokia  hiyo Padri  Justus Lugayimkamu  kuwaaga  katika  parokia  hiyo ambapo mwezi huu anatarajia kuhamishwa  na kupelekwa  mahali  atakapopangiwa kufanya utume.

Padri  Lugayimkamu amehudumu kama  Paroko  Msaidizi  parokiani  Kimbiji kwa miaka  mitatu na  ushirikiano  mzuri  aliokuwa  nao kwa  waamini umewafanya  watoe  machozi.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI