WASIMAMIZI WA MIRADI WATAKIWA KUWA WABUNIFU
RAI imetolewa kwa watekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo nchini kuwa na ubunifu ili kwendana na soko la ushindani katika
nyanja za kitaifa na kimataifa.
Katibu Mkuu wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba ameyasema hayo
mwanzoni mwa juma wakati akifungua Mkutano wa siku mbili ambao pamoja na mambo
mengine, ulilenga kujadili kwa pamoja mafanikio, changamoto na kupanga shughuli
za mwaka 2018 uliowakutanisha watendaji wakuu wa Mradi wa Uendelezaji wa Utu wa
Mwanadamu (IHDP).
Katika mkutano huo
uliofanyika Kurasini jijini Dar es Salaam, Padri Saba ameeleza bayana kuwa
licha ya kuridhishwa na shughuli zinazofanyika chini ya mradi huo katika wilaya
mbalimbali nchini hasa kuwainua watu kiuchumi pamoja na kuwapatia mbinu
mbalimbali za kufuatilia rasilimali fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya
miradi maendeleo, lakini amebainisha kuwa ubunifu zaidi unatakiwa hasa kwa
kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa na wananchi kupitia vikundi vyao vya
Benki za Kijamii Vijijini vinavyoendeshwa chini ya Mahusiano ya Dini Mbalimbali
(IR-VICOBA).
“Tupende kujifunza
kutoka kwa wenzetu wanaotekeleza miradi kama yetu ili tuweze kuwa na ufanisi
zaidi kwani hakuna dhambi kuwa na wivu wa maendeleo,” amesema Katibu Mkuu huyo
wa TEC na kuongeza kuwa “ Nimebahatika kutembelea baadhi ya wilaya
zinazotekeleza mradi huu ikiwemo Mbozi na Kasulu na kwakweli watu wanatoa
ushuhuda mzuri sana kwa jinsi walivyofanikiwa
kupitia miradi yetu ya Mahusiano ya Dini Mbalimbali, hili ni jambo jema
na niwapongeze sana kwa hilo.”
Aidha Katibu Mkuu
huyo wa TEC amewataka washiriki wa Mkutano huo kuwa na nidhamu ya fedha
inayotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuwa na
vielelezo sahihi juu ya matumizi yake.
Amesema
wafadhili wanapotoa fedha yao kwa ajili
ya miradi ya maendeleo wanataka itumike kwa kunufaisha walengwa na kwamba
kinyume chake ni kuchafua jina la taasisi inayokuwa imeingia mkataba na wafadhili
hao.
“Tutambue thamani
ya fedha tunayopewa na wafadhili…Hakuna njia ya mkato…tunapokubali fedha yao
kwa kuingia kwenye makubaliano (mkataba)lazima tukubali pia masharti
wanayoyatoa juu ya matumizi ya fedha zao,” amesisitiza.
Mradi wa
Utekelezaji wa Utu wa Mwanadamu unafanya kazi kupitia Idara ya Haki, Amani na
Uadilifu Katika Uumbaji ambayo ipo chini ya Kurugenzi ya Hadhi ya Ubinadamu (Human Dignity) ya Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na unatekeleza shughuli zake kupitia Kamati za Mahusiano ya Dini
Mbalimbali katika wilaya za Kasulu, Mbozi, Njombe, Ludewa, Karatu, Babati ,
Temeke na Mtwara chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Makanisa ya Norway
(NCA).
Miradi
inayotekelezwa kupitia miradi hiyo ni pamoja na kuwainua watu kiuchumi kupitia
Benki za Kijamii Vijiji (IR-VICOBA), Ufuatiliaji wa Rasilimali za Umma
zinazotolewa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Maendeleo (PETS) na Masuala
Mtambuka yanayohusisha mahusiano ya dini mbalimbali na usaidizi wa kisheria.
Comments
Post a Comment