TEC YAPONGEZWA NA SERIKALI UKUZAJI ELIMU NCHINI
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara
Mhandisi Stella Manyanya amelipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa
juhudi, maarifa na busara kuamua kuwekeza katika sekta ya elimu hivyo kuwa chachu
ya ukombozi wa Mtanzania.
Waziri Manyanya ameyasema hayo kwenye
mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (RUCU) yaliyofanyika hivi
karibuni kwenye viwanja vya chuo hicho na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza
la Chuo Kikuu Katoliki Ruaha, Askofu wa Jimbo Katoliki Njombe Mhashamu Alfred
Maluma, wahitimu wa fani mbalimbali kutoka chuoni hapo na wageni waalikwa
kutoka sehemu mbalimbali.
Manyanya amesema kuwa Kanisa Katoliki
kupitia Baraza la Maaskofu limekuwa mdau mkubwa wa elimu kabla na hata baada ya
Uhuru, pia mshiriki mkubwa wa Serikali katika kuchangia ukuaji wa Elimu nchini
na siyo katika elimu peke yake bali hata katika afya na huduma nyingine za
kijamii.
“Napenda pia kutumia fursa hii
kulipongeza Kanisa Katoliki kwa juhudi kubwa hasa katika kukuza na kuendeleza
elimu hapa Tanzania. Limekuwa mdau mkubwa wa elimu, afya na mjenzi wa amani kwa
njia ya mahubiri yake, nalipongeza sana Baraza la Maaskofu kwa juhudi, maarifa
na busara za kuamua kuwekeza katika sekta ya elimu," amesema Mhandisi Manyanya.
Mhandisi Manyanya amesema kuwa, elimu
ni nyenzo kuu katika vita dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini, pia kiini cha
maendeleo ya nchi yoyote duniani.
"Leo wahitimu wanatunukiwa vyeti
mbalimbali kuashiria kuwa wamehitimu viwango mbalimbali vya taaluma, ni imani
yangu kuwa wahitimu hawa wamepata nyenzo za kutosha kuwawezesha kumudu na
kuzikabili changamoto za ulimwengu wa sasa hasa katika kujenga Tanzania ya
viwanda."
Vile vile Mhandisi Manyanya amesema
kuwa utandawazi ni moja ya changamoto hizo kwa sababu umewaingiza katika
mwingiliano wa mataifa katika nyanja za uchumi, siasa na utamaduni. Hivyo
wanapoingia katika ushirikiano wa kiuchumi na nchi mbalimbali duniani ambazo
nguvu kazi imekuwa huru kuhama toka nchi moja hadi nyingine, changamoto mbele yao
ni ajira.
" Watanzania wanapaswa kuwa
wameandaliwa kikamilifu kumudu ushindani huo katika soko la kimataifa la ajira
ili wasije kufanywa vibarua ndani ya nchi yao, lakini pia wengine waweze kwenda
nchi jirani na hata kwingineko na kukubalika kwa uwezo wao, mimi naamini kuwa
wahitimu tunaowatunuku leo vyeti wameiva kitaaluma na changamoto hizi
wakazikabili."
Amewataka wahitimu hao kutambua kuwa
elimu waliyoipata imewaongezea uwezo mkubwa wa kufikiri zaidi kukabiliana na
changamoto mbalimbali zilizo mbele yao na kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi kwenye
mahafali hayo Makamu Mkuu wa Chuo hicho Pd. Dk. Cephas Mgimwa amesema kuwa chuo
hicho kilianzishwa kwa juhudi za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa
msaada wa serikali mwaka 2005 kuanzia kudahili wanafunzi 524 kwa kozi za cheti
na shahada katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Kwa mujibu wa Dk. Mgimwa idadi ya
wanafunzi kwa kozi mbalimbali imeongezeka hadi kufikia 5,212 kwa mwaka wa
masomo 2017/2018 kati ya wanafunzi wote waliodahiliwa asilimia 43% ni wanawake
na asilimia 57% ni wanaume.
Kozi zinazotolewa katika chuo zipo
kwenye Vitivo na taasisi, vitivo ni vinne ambavyo ni Sanaa na Sayansi ya Jamii,
Sheria, Biashara na Sayansi ya Menejimenti, Mawasiliano na Teknolojia.
Kwa upande wa taasisi zipo mbili
katika ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili na shahada
ya uzamivu.
Aidha idadi ya programu zinazotolewa
zimeongezeka kutoka 2 mwaka 2005 hadi kufikia 27 mwaka 2017/2018 ambazo
zimeendeshwa kwa kuzingatia majukumu makuu ya vyuo vikuu ambayo ni kufundisha,
kutafiti na kusaidia jamii.
Chuo hicho pia kinatafuta uwezekano wa
kuwa na mfumo unaowezesha wahitimu kusoma ngazi zote za kozi husika kutoka
astashahada hadi shahada ya uzamivu.
"Hivi leo tunashuhudia kuhitimu
jumla ya wanafunzi 1,776 ambazo ni asilimia 93% ya wanafunzi wote waliodahiliwa
kwa mwaka wa masomo 2017/18 kati yao wahitimu 1,776 watatunukiwa vyeti
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na stashahada, stashahada na shahada za uzamili,"
amesema Dk. Mgimwa.
Akizungumzia watumishi na mazingira ya
kazi, Dk. Mgimwa amesema kuwa chuo kwa sasa kina idadi ya watumishi 260 ambao
156 ni wanataaluma na 104 ni wafanyakazi katika utawala (administration) na
kuna mpango wa kuongeza idadi ya watumishi kulingana na kasi ya ukuaji, na
katika kutekeleza hilo chuo kimepeleka watumishi 22 masomoni ili kukuza taaluma
zao na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Kuhusu ujenzi wa kampasi na ongozeko
la programu, chuo kina mpango mkakati mpya 2016/2026 wa miaka kumi ukiwa
na maeneo ya vipaumbele kama vile ujenzi wa shule (shools) katika maeneo
yanayomilikiwa na chuo kama vile Igumbilo, Mgera, Mwangata na Mawelewele.
Dk. Mgimwa ameendelea kusema kuwa
" Katika kufanikisha lengo la Baraza la Maaskofu Katoliki kuanzisha vyuo
pale ambapo bado huduma ya elimu haijafika, RUCU kupitia mpango mkakati huo
kimenunua na kuendelea kununua ardhi ndani na nje ya nchi, Njombe, Mbeya, Ruvuma,
Dodoma, Dar es Salaam, Katavi, Songwe,Morogoro, Kibaha na Tunduma, na nchi ya
jirani zikiwa ni pamoja na Malawi na Zambia."
Katika kipindi kijacho chuo kimepanga
kuendelea kuboresha miundombinu yake ili kukidhi mahitaji ya chuo kikuu kamili
RUCU, na hii itahusu kuanzisha na kuboresha sera, miongozo na kanuni za
utendaji pia kutafuta na kuwekeza maeneo mbalimbali ili kujihakikishia uendelevu
wa progamu za chuo na kuajiri na kuendeleza wafanyakazi wa taaluma mbalimbali
na utawala kulingana na uzito wa kazi zinazoendana na ukuaji wa chuo.
Chuo pia kimeishukuru serikali kwa
misaada mbalimbali kwani misaada hiyo imehusisha ujengaji wa uwezo wa
kiutendaji wa wafanyakazi (capacity building) utoaji wa miongozo ya ubora wa
progamu (quality assurance), uwezeshwaji wa udahili na uhisani kwa wanafunzi
wengi wa chuo hicho pia uhusishwaji wa chuo katika masuala ya elimu.
Na Getruda Madembwe, Ruaha
Comments
Post a Comment