Ndoa zaidi ya 200 zafungwa Parokiani Mwambani Mbeya
PAROKIA ya Mwambani katika Jimbo Katoliki
Mbeya imefanikiwa kutoa Sakramenti Takatifu ya Ndoa kwa wanandoa 222 kwa muda
wa mwezi mmoja na siku nane hali iliyotoa hamasa kwa waamini jimboni humo
kushiriki Sakramenti hiyo.
Tukio hilo la kipekee limetokea katika
Kanisa la Mtakatifu Karoli Lwanga Parokia ya Mwambani Jimbo Katoliki Mbeya
katika wilaya ya Songwe mkoani Songwe
ambapo wanandoa vijana kwa wazee
wameamua kuuaga ukapera mbele ya maelfu ya wakazi wa wilaya hiyo.
Akizungumza katika sherehe ya ndoa
hizo iliyobebwa na kauli mbiu “kama kweli unanipenda tufunge ndoa! Tufunge ndoa
kama unanipenda”, paroko wa Parokia ya Mwambani padri Laulian Mwambala
amewapongeza waamini walioitikia wito
huo na kufanya maamuzi ya kuishi kikristo kwa mujibu wa sheria na taratibu za
Kanisa.
Padri Mwambala amesema zoezi zima
limehusisha ndoa 222 lakini kutokana na
uhitaji na maombi ya baadhi ya Makatekista kuomba ndoa nyingine
zikafanyikie katika vigango wamelazimika kuanza kufungisha ndoa 152 kwa siku moja.
Amesema ndoa nyingine zimetafutiwa
kufungwa katika Vigango vya Parokia hiyo na kufafanua kuwa Oktoba 25 zimefungwa
ndoa 49 katika Kigango cha Mbala, Oktoba 28 imefungwa ndoa moja katika Kigango
cha Mkwajuni, Oktoba 29 zimefungwa ndoa
9 katika Kigango cha Saza, Novemba 4 imefungwa ndoa moja katika Kigango cha
Mkwajuni na Mwambani ndoa moja, Novemba 5 zimefungwa ndoa saba katika Kigango
cha Maleza, Novemba 11 imefungwa ndoa moja katika Kigango cha Mkwajuni na ndoa
moja imefungwa Novemba 12 katika Kigango cha Mbangala na hivyo kufikisha idadi
ya ndoa 222 ambazo tayari zimefungwa tangu Oktoba 22 hadi Novemba 12,2017.
Paroko huyo amefafanua kuwa kadiri
ya ratiba bado ndoa nne katika kigango cha Kalanda zitakazofungwa Novemba,19 na
ndoa mbili katika Kigango cha Mkwajuni zinazotarajiwa kufungwa Novemba 25,2017
na hivyo kufikisha idadi ya Ndoa 228 kufungwa kwa muda wa miezi miwili tukio
ambalo halijawahi kutokea katika historia tangu kuanzishwa kwa Parokia ya
Mwambani.
Amebainisha kuwa siri ya
kufikia mafanikio hayo ni baada ya
kutembelea familia na kubaini kuwa watu
walio wengi wanaishi bila kufunga ndoa kutokana na kuhofia gharama za kufanya
sherehe.
“Jamii nyingi hutumia gharama
kubwa kwa ajili ya maandalizi ya sherehe
za Ndoa jambo ambalo ni la kidunia, watu wengi hawaelewi muunganiko kati ya
Sakramenti ya ndoa na sherehe, wale wote
walioamua kufunga ndoa wamefungua ukurasa mpya katika maisha yao,” amesema
padri Mwambala.
Aidha padri Mwambala amefafanua kuwa ndoa yenye
mke na mume mwema inaleta afya njema
kwa kila mwanandoa na watoto hivyo wanapaswa kuepuka
maneno makali, chuki na ugomvi ambayo ni sumu
na chanzo cha kutenganisha
familia na matokeo ya malezi mabaya kwa familia.
“Upendo wa kweli ndio mzizi wa kila
kitu, ndoa siyo tamasha la masikitiko bali ni tamasha la
furaha ,wanandoa mnayo majukumu ya kuifanya ndoa kuwa chanzo cha furaha
na amani siku zote na siyo kuifanya iwe kama kiwanda cha
kutengenezea sumu, watoto wafurahie kuwepo kwa baba
na mama wenye kuishi ndoa kwa malezi mazuri
yanayotawaliwa na amani ya kweli,” amewaasa.
Ameongeza, “kwa wote mlioamua
kufunga ndoa leo, mabadiliko yaanze leo katika kuonesha matendo mazuri kwa
kuitana majina mazuri na maneno matamu matamu kila wakati kama
baby, honey, laazizi wangu, jembe
langu, na kila mara ifanyeni ndoa yenu kuwa mpya.”
Ameelezea pia kuwa manufaa ya kuishi viapo na kauli nzuri katika ndoa
ndiyo siri kubwa kupata viongozi wazuri
katika Kanisa na jamii kwa ujumla
na kwamba shahada ya ndoa ni msaada mkubwa katika kudai haki na hasa mirathi baada ya mwanandoa mmoja
kufariki.
“Kupitia tendo hili takatifu,
ninawaalika wale wanaoishi uchumba sugu wabadilike na kutambua umuhimu wa
ndoa na hasa katika dunia ya sasa ambayo
inakumbana na changamoto nyingi.”
Hata hivyo KIONGOZI limezungumza
na baadhi ya waamini waliofunga ndoa siku hiyo kwa nyakati tofauti
ambapo Deogratias Ganji na Gregoli Pesambili wameelezea furaha yao na kwamba
wamejiona wameuvaa utu mpya na kuuacha wa zamani ambao ulikuwa wa kuwanyanyasa, kuwatesa na
kuwapiga hovyo wenzi wao.
“Lakini leo tumekuwa ni kama
tumeanza upya na kupitia baraka tulizopata na ujumbe tuliopewa tunajiona
tumekuwa wapya kabisa na tunazifurahia ndoa zetu tofauti na hali ilivyo kuwa
awali na tunajiona tulikuwa wakosefu kwa
wake zetu lakini tumeungama na kuwaomba wasamehe yale yote tuliyokuwa tunawakosea
awali tufungue ukurasa mpya wa baba na mama mwema,”walisema kwa furaha wanandoa hao kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo wamewashukuru pamoja na
kuwapongeza mapadri kwa juhudi zao bila kukata tamaa kwa kuwatembelea mara kwa
mara licha ya kukutana na changamoto za hapa na pale hadi kufanikisha zoezi
hilo muhimu katika maisha yao. Wameahidi kuwa mabalozi na walimu kwa
wengine ambao bado hawapo tayari kufunga
ndoa.
Comments
Post a Comment