‘Msiwabague mnaowatumikia’
·
SFUCHAS yaendelea kuwezesha jamii maskini Tanzania
Na
Pascal Mwanache, Ifakara
WANATAALUMA
na wadau wa maendeleo nchini wametakiwa kuiga mfano wa jitihada zinazofanywa na
Kanisa Katoliki nchini za kutoa huduma za kijamii kwa watu wote hasa wa
vijijini bila kujali dini, kabila au ukanda.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe katika Mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu
Kishiriki cha Sayansi za Afya cha Mtakatifu Fransisko Ifakara (SFUCHAS)
yaliyofanyika Novemba 11 chuoni hapo ambapo takribani wataalamu wa Sayansi za
Afya 256 wamehitimu.
Dkt. Kebwe amesema kuwa SFUCHAS
imekua mstari wa mbele katika kutatua changamoto za uhaba wa wataalamu wa afya
nchini kwa kuwa wataalamu wengi wanaozalishwa na chuo hicho wanakuwa tayari
kufanya kazi katika maeneo ya vijijini ambako kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu
wa afya.
“Huu ni mwendelezo wa kazi
iliyofanywa na wamisionari. Itakumbukwa kuwa wakoloni waliweka huduma za jamii
sehemu walizokuwa na maslahi nazo. Lakini ninyi mnafanya kinyume, mnatoa huduma
bila ubaguzi, kwa watu wote na maeneo yote” ameeleza Dkt. Kebwe.
Ameweka wazi kuwa SFUCHAS
inafanya kazi kubwa ya kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa afya
vijijini ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya wataalamu wa afya hasa wafamasia na madaktari wapo Dar es
salaam. Amewahimiza wahitimu waendelee kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya kazi
kwa bidii ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, na kuakisi malezi
bora waliyoyapata chuoni hapo.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo
Katoliki Ifakara Mhashamu Salutaris Libena amesema kuwa mafanikio ya chuo hicho
ni mwendelezo wa jitihada za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) za
kuwekeza katika chuo hicho kitaaluma na kimiundombinu.
Askofu Libena ambaye aliongoza
Misa Takatifu iliyotangulia mahafali hayo amewataka wahitimu hao wakawe
wawakilishi wema kwa kuiishi taaluma na viapo vyao na kuzingatia maadili na
kumpendeza Mungu.
“Tumekusanyika ili tuwatume
vijana wetu hawa. Mahafali maana yake ni kuutangazia ulimwengu kuwa huyu anayetunukiwa
cheti au zawadi hana deni pale chuoni. Tunawatuma kwenda duniani kote kwenda
kutoa huduma kwa watu wote kama mlivyofundishwa mkiwa chuoni” ameeleza Askofu
Libena.
Sherehe za mahafali ya chuo
hicho zimeenda sambamba na uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi
na Chuo cha Meno (Dental School) na kuweka jiwe la msingi katika jengo liitwalo
Askofu Agapiti Ndorobo.
Kwa mujibu wa taarifa fupi
iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia Mipango, Fedha na
Utawala Padri Archilleus Ndege, jengo la Askofu Agapiti Ndorobo linajengwa kwa
lengo la kufanikisha mafunzo ya wataalamu wa afya maeneo ya vijijini ili
wakishahitimu wawe tayari kufanya kazi maeneo ya mbali na miji.
Jengo hilo lina vyumba vikubwa
kumi na nne ambavyo vitatumika kwa shughuli za kumbi za kufundishia, maabara 2
na darasa la kufundishia teknolojia ya habari na mawasiliano-TEHAMA. Aidha
taarifa hiyo imeeleza kuwa ekari kumi zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa mabweni
ya ghorofa 4 mawili yenye vyumba 72 kila moja, jengo la maktaba, jengo la
utawala, madarasa, shule ya meno, mgahawa pamoja na maduka.
Comments
Post a Comment