KUELEKEA MAHAFALI YA 19: SAUT YAJIVUNIA ELIMU BORA
CHUO KIKUU cha Mtakatifu Agustino
(SAUT) cha jijini Mwanza kimeendelea kusifiwa kwa kutoa elimu bora hasa kwa
njia ya vitendo kwa wananchi ndani na nje ya Tanzania.
Hayo yamebainika zikiwa zimesalia
siku chache kabla ya chuo hicho kusherehekea mahafali yake ya 19 tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1998.
Afisa
Uhusiano wa chuo hicho Living Komu akizungumza na gazeti la
Kiongozi amesema kuwa SAUT ni chuo cha kujivunia kwa wanafunzi wote waliopita
hapo kwa maana ni chuo kitoacho wanafunzi bora kitaaluma na kimaadili.
‘Ili uweze kutambulika na kuheshimiwa
ni lazima uwe na nidhamu njema na pia taaluma iliyotukuka, hivyo kama chuo
kinajitahidi na kimeweza kufanya kadri ya uwezo wake kuzalisha wanafunzi wenye
vigezo bora vya kuuzika katika soko la ajira ya sasa na hata baadaye ndani na
nje ya Tanzania,’ amesema Komu.
Amewakumbusha wanafunzi wote ambao
wanakwenda kuhitimu katika mahafali ya 19 kuwa ni vyema watumie elimu na
nidhamu waliyofunzwa hapo chuoni na kuwa kioo kizuri katika jamii.
Pia ameongeza kwa kusema kuwa
wanafunzi wanaokwenda kuhitimu waendelee kupitia katika mitandao mbalimbali ya
chuo kwa ajili ya kufuatilia taarifa zitolewazo kuelekea katika mahafali hayo
ili kuwa na taarifa kamili na kufahamu utaratibu mzima.
Hata hivyo ameongeza kuwa wanafunzi
wanaoendelea na masomo yao katika chuo hicho waendelee kusoma kwa bidii na
juhudi zote na pia kuendeleza nidhamu ya chuo ili kutekeleza malengo na
madhumuni ya maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)
walipoanzisha chuo hicho kwa lengo la kutoa vijana wenye elimu njema na nidhamu
bora.
Ametumia fursa hiyo pia kuwakaribisha
ndugu na jamaa katika maonesho ya SAUT jamii (Community Day) yanayojumuisha
wanafunzi na walimu wa vitivo vyote vya chuo hicho ambapo maonesho hayo huwa ya
kitaaluma na huwa na mafunzo kwa jamii nzima ambapo yanatarajiwa kufanyika
tarehe 6 Disemba 2017.
Hata hivyo chuo hicho kikuu cha SAUT
kimewakaribisha wananchi katika mahafali yake ya 19 yatakayofanyika chuoni hapo
tarehe ya 8 na 9 Disemba ambapo kinategemea wageni zaidi ya 6,000 kuhudhuria
sherehe hizo ambazo zimechochewa na muamko wa wahitimu wengi wanaomaliza katika
chuo hicho.
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino
kinamilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambapo chuo hicho kimefanikiwa
kuzalisha idadi kubwa ya wanafunzi wa ndani na nje ya nchi kwa kutoa elimu bora
na endelevu kwa jamii bila ubaguzi.
Katika mahafali yake ya 19 tangu
kuanzishwa kwake, takribani wanafunzi 2000 watatunukiwa shahada, astashahada na
shahada ya uzamivu katika vitivo mbalimbali.
Na George Alexander,
Mwanza
Comments
Post a Comment