CARITAS MBEYA YAWAWEZESHA MABINTI WALIOTELEKEZWA
WITO umetolewa kwa wazazi na jamii kwa
ujumla kuwatia moyo na kuwapatia stadi za maisha ikiwemo elimu ya
ujasiriamali wasichana wadogo wanaopewa ujauzito na kutelekezwa badala ya
kuwaacha wakikata tamaa ya maisha.
Ushauri huo umetolewa na mfuatiliaji wa
vikundi vya mabinti walea pekee kutoka Idara ya CARITAS na Maendeleo,
Jimbo Katoliki Mbeya anayeshughulikia maeneo ya Jiji la Mbeya, Magdallena
Mwashala alipokuwa akizungumza na KIONGOZI mara baada ya
kumtembelea mmoja wa mabinti walea pekee kujua maendeleo yake katika maeneo ya
Tambukareli, Kata ya Itezi jijini Mbeya.
Magdallena amesema kuwa msichana Jane
Ndangali ni miongoni mwa wanakikundi cha Amka ambaye alijikuta amejiingiza
katika mahusiano na kuzalishwa watoto wawili na baadaye kutelekezwa na
mwenzi wake, lakini baada ya kuhamasishwa kujiunga katika kikundi
amefanikiwa kupewa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali, utunzaji wa fedha,
kuishi katika maadili mema, kujua haki zake na za mtoto pamoja na stadi za
maisha.
Amesema baada ya kupatiwa mafunzo msichana
huyo amekuwa miongoni mwa wanakikundi cha Amka walioweza kupata mafanikio
makubwa yakiwemo ya kutunza familia yake bila kumtegemea mtu yeyote.
"Unaweza kukata tamaa ya kuishi baada ya
kuona kila kukicha ni matatizo na vifo vinaendelea kuisonga familia
yenu na hatimaye ukajikuta unatumbukia katika mikono
unayodhani ni ya watu salama na wasamaria wema kumbe la hasha,
unajiingiza katika matatizo zaidi lakini jamii inapaswa kukusaidia kwa kuwa
jirani nawe na kukushauri na hata kukusaidia kwa hali na mali na ndivyo Caritas
tunavyofanya katika kuisaidia jamii," amesema Magdallena.
Ameongeza,"vijana wanapojikuta wameingia
katika matatizo na makundi yasiyofaa hawapaswi kutelekezwa bali kuwasogelea,
kukaa na kuzungumza nao na wanaweza kubadilika kuwa vijana wema na wa
mfano wa kuigwa katika jamii."
"Ndivyo ilivyomtokea Jane Ndangali
msichana mwenye umri wa miaka 26 baada ya kutelekezwa, kwa sasa anailea vyema
familia yake kwa kufanya bishara za viazi mviringo na kufyatua matofari,
anapanga tanuru yeye mwenyewe na kuchoma na kuuza na amejenga
nyumba yake ya kuishi na familia yake," amefafanua Magdallena.
Akizungumza na Kiongozi, msichana huyo
ameishukuru Idara ya Caritas na Maendeleo Jimbo Katoliki Mbeya kwa
kumfuata na kumshawishi kujiunga katika kikundi na baadaye kupatiwa
mafunzo yaliyomsaidia kufikia hatua aliyopo.
Hata hivyo Jane ametoa ushauri kwa wasichana
wenzake kuwa wanapokumbwa na matatizo wasijifiche na badala yake watafute
ushauri kwa watu mbalimbali ikiwemo kujiunga katika vikundi hali
inayowasaidia badala ya kujitenga na matokeo yake wanaweza kuathirika
zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha
mabinti walea pekee cha Tupendane kilichopo Mtaa wa Gombe Kaskazini, Kata ya
Uyole, jijini Mbeya, Happy John amempongeza msichana mwenzao kwa
hatua aliyoifikia na kwamba wao wanatamani kufikia hatua hiyo.
"Na sisi katika kikundi chetu tunafyatua matofari,
tupanga tanuru, kuchoma na kuuza matofari pamoja na kutengeneza nguo aina
ya batiki, lakini tunawashauri wasichana wenzetu waache kukata tamaa na
maisha. Pia jamii isipende kuwatenga vijana wanaowaona wanapotea na
badala yake wajenge utamaduni wa kuwasogelea na kuzungumza nao ikiwemo kuwatia
moyo," amesema.
Na Thompson Mpanji, Mbeya
Comments
Post a Comment