Wasomi kuweni wazalendo-Askofu Mapunda

Na Angela Kibwana, Morogoro

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Singida Mhashamu Edward Mapunda amewaasa wahitimu wa vyuo vyote nchini kuhakikisha kuwa elimu wanayoipata katika ujuzi mbalimbali inawasaidia watanzania wote kwa ujumla, hasa kujali utu wa binadamu na kumkomboa katika changamoto zake.
Askofu Mapunda amesema kuwa jambo la msingi wanalopaswa kuzingatia wasomi hao ni kuhakikisha elimu wanayopata vyuoni  inajenga heshima kwa wanadamu wote, utu na iwasaidie watu kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha.
Askofu Mapunda amesema hayo hivi karibuni katika mahafali ya tano ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Augustino Jordan kilichopo mkoani morogoro, ambapo jumla ya wahitimu 1,305 wamehitimu katika kozi mbalimbali.
Askofu Mapunda amesisitiza kuwa wahitimu wanapaswa kuzingatia elimu wanayopewa ili iwe chachu ya kuwatumikia watanzania bila kutanguliza ubinafsi na iondoe ukoma wa watu.
“Elimu yetu itusaidie kuwatumikia watanzania, tusijitahidi tu kukesha usiku kucha kusoma tu bila kujali mahitaji ya mtanzania, sasa kama sisi tunasoma halafu watu wanaendelea kuwa wakoma haina maana. Kusoma kwetu kunatusaidia nini kama hatujibidiishi kuondoa umasikini, magonjwa na ujinga?” amehoji Askofu Mapunda.
Askofu Mapunda ametoa wito kwa wahitimu kujiepusha na masuala ya rushwa na ufisadi miongoni mwao, kwa sababu rushwa ni adui wa haki na hata maandiko matakatifu yanasema wala rushwa hawataingia mbinguni kwa sababu wana mikono michafu.
Hata hivyo wahitimu hao wameshauriwa kutumia elimu zao kwa faida ya wote ambapo wanapaswa kutafakari kuwa taaluma zao ni kwa maendeleo ya taifa, si kwa ajili ya kujimilikishia mali, wasitumie vyeo vyao kwa ubinafsi na kusababisha mafarakano ya kuporomosha haki na kuhatarisha amani.
Wakati huohuo, Askofu Mapunda amesema kuwa kazi ya wasomi ni kutenda haki na kujenga dunia ya wenye haki na watu wenye amani ambapo sifa ya mtu msomi ni kusema ukweli na kusimamia maslahi ya wengine, japo hali hii inagubikwa na mfumo wa ubinafsi na rushwa na kusababisha kasoro ndani ya taifa.
“Nawaalika ndugu zangu tuliobahatika kwenda shule tuyashike haya ili elimu yetu iwe na faida, kama huyu msomi aliyesoma ni mwizimwizi tu, analiibia taifa lake elimu hii ni ya nini? kama hana desturi ya kusema ukweli ni muongomuongo tu, elimu hiyo ni ya nini? tujibiidishe kumpa Mungu utukufu,” amesema Askofu Mapunda.
Aidha kiongozi huyo wa kiroho amewaasa wahitimu kuwa waadilifu na watiifu katika nafasi mbalimbali watakazofanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kuitii serikali kwa lengo la kuwatumikia watanzania katika utatuaji wa changamoto zao kwa maendeleo ya taifa.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU