Kongamano la Ekaristi Takatifu Kanda ya Mashariki kufanyika Zanzibar 2019

Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam
MAASKOFU wa Kanisa Katoliki Kanda ya Mashariki nchini wamesema ili kuendeleza Ibada na heshima kwa Ekaristi Takatifu wameridhia kufanya Kongamano la Ekaristi Takatifu kila baada ya miaka mitatu ambapo mwaka 2019 Kongamano hilo litafanyika katika Jimbo Katoliki Zanzibar.
Wamesema hayo katika kilele cha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kanda ya Mashariki lililofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Msimbazi, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.
Akisoma maazimio ya Kongamano hilo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mwadhama Polycap Kardinali Pengo amesema kuwa, Kongamano hilo la Ekaristi Takatifu limekuwa ni neema na baraka kwa waamini wote walioshiriki Kongamano hilo na Kanisa kwa ujumla.
 “Katika kuendeleza neema na baraka hizo za Mungu kwa taifa  sisi Maaskofu wa Kanda ya Mashariki baada ya kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa waamini, makleri na wanakongamano wote, tumekubaliana tuwe na Adhimisho la Kongamano la Ekaristi katika Kanda ya Mashariki kila baada ya miaka mitatu.
Kongamano la pili la Ekaristi Takatifu  katika Kanda ya Mashariki litafanyika Jimbo Katoliki Zanzibar Juni 2019. Tumepanga 2019 badala ya 2020 kwasababu mwaka 2020 kutakuwa na vuguvugu za Uchaguzi Mkuu katika taifa letu,” amesema Kardinali Pengo.
Aidha, Ili kuendeleza ibada na heshima kwa Ekaristi Takatifu maaskofu hao wameazimia kuwepo na kuendelezwa kwa makanisa ya kuabudu daima Ekaristi Takataifu (Perpetual Adoration chapels) ambamo Ekaristi Takatifu itawekwa na kuabudiwa kwa masaa 24 kila siku.
Makanisa hayo yajengwe kwenye majimbo yote ya Kanda ya Mashariki na waamini wanaombwa kujitokeza kwa wingi kwenda kuabudu Ekaristi Takatifu ili  kujichotea neema ya ukombozi. Wameazimia kuwa, ili kuendeleza malezi ya kiimani kwa watoto na kuwezesha kutambua na kuthamini nafasi ya Ekarist i Takatifu katika maisha ya kikristo washiriki wa kongamano hilo wameazimia kuzifanya familia na parokia zao kuwa vituo vya katekesi na mafundisho endelevu na kina  ya imani kuhusu Ekaristi Takatifu kwa watoto wao.
“Tunatoa mwito kwa mapadri, watawa, makatekista, wazazi na walezi wote kusitawisha utume wa Utoto Mtakatifu na kuwawezesha watoto wote kuwa washiriki wa Shirika hilo la  Utoto Mtakatifu ambalo ni chombo muhimu cha kukuza imani na moyo wa umisisonari kwa watoto wetu.
Wanandoa wanaojiandaa kupokea sakramenti ya ndoa na wale ambao tayari wameshaipokea Sakramenti hiyo wapewe katekesi na mafundisho ya kina kuhusu Ekaristi Takatifu ili watambue kuwa furaha na upendo wa ndoa zao zinategemea moja kwa moja muungano wao na Yesu wa Ekaristi. Bila Ekaristi Takatifu hakuna uhai wa kimungu ndani ya familia,” amesisitiza Kardinali Pengo.
Ili kuwezesha waamini kuwa na ibada za mara kwa mara za Ekaristi Takatifu, parokia zote katika Kanda ya mashariki zinapaswa kuwa na utaratibu wa kufanya ibada na kuabudu Ekaristi Takatifu mara moja kwa juma. Waamini wajitokeze kwa wingi kushiri ibada hizo.
Kilele cha Kongamano hilo kilikuwa cha namna yake ambapo palikuwa na maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam ambapo Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar aliongoza maandamano kutoka Parokia ya Magomeni hadi Msimbazi, Askofu Anthoni Banzi wa Jimbo Katoliki Tanga aliongoza maandamano ya Ekaristi Kutoka Kanisa la Mtakatifu Josefu ( Posta ) hadi Msimbazi.
Askofu wa Jimbo Katoliki Mahenge Mhashamu Agapiti Ndorobo aliongoza maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka Parokia ya Buguruni hadi Msimbazi na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Euzebius Nzigilwa aliongoza maandamao ya Ekaristi Takatifu kutoka Parokia ya Kurasini hadi Msimbazi ambapo waamini wote walikutana kwa Adhimisho la kilele cha Kongamano hilo.
Kongamano hilo lilianza November 10-12 mwaka huu lilihudhuriwa na maelfu ya waamini wakiwemo maaskofu, mapadri na waamini walei kutoka majimbo yanayounda Kanda hiyo ya Mashariki ambayo ni Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Ifakara, Tanga, Morogoro, Zanzibar na Mahenge. Mkuu wa Kanda hiyo ya Mashariki ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU