WASIMAMIZI WA MIRADI WATAKIWA KUWA WABUNIFU

Na Dalphina Rubyema, DSM

RAI imetolewa kwa watekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kuwa na ubunifu ili kwendana na soko la ushindani katika nyanja za kitaifa na kimataifa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba ameyasema hayo mwanzoni mwa juma wakati akifungua Mkutano wa siku mbili ambao pamoja na mambo mengine, ulilenga kujadili kwa pamoja mafanikio, changamoto na kupanga shughuli za mwaka 2018 uliowakutanisha watendaji wakuu wa Mradi wa Uendelezaji wa Utu wa Mwanadamu (IHDP).
Katika mkutano huo uliofanyika Kurasini jijini Dar es Salaam, Padri Saba ameeleza bayana kuwa licha ya kuridhishwa na shughuli zinazofanyika chini ya mradi huo katika wilaya mbalimbali nchini hasa kuwainua watu kiuchumi pamoja na kuwapatia mbinu mbalimbali za kufuatilia rasilimali fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi maendeleo, lakini amebainisha kuwa ubunifu zaidi unatakiwa hasa kwa kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa na wananchi kupitia vikundi vyao vya Benki za Kijamii Vijijini vinavyoendeshwa chini ya Mahusiano ya Dini Mbalimbali (IR-VICOBA).
“Tupende kujifunza kutoka kwa wenzetu wanaotekeleza miradi kama yetu ili tuweze kuwa na ufanisi zaidi kwani hakuna dhambi kuwa na wivu wa maendeleo,” amesema Katibu Mkuu huyo wa TEC na kuongeza kuwa “ Nimebahatika kutembelea baadhi ya wilaya zinazotekeleza mradi huu ikiwemo Mbozi na Kasulu na kwakweli watu wanatoa ushuhuda mzuri sana kwa jinsi walivyofanikiwa  kupitia miradi yetu ya Mahusiano ya Dini Mbalimbali, hili ni jambo jema na niwapongeze sana kwa hilo.”
Aidha Katibu Mkuu huyo wa TEC amewataka washiriki wa Mkutano huo kuwa na nidhamu ya fedha inayotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuwa na vielelezo sahihi juu ya matumizi yake.
Amesema wafadhili  wanapotoa fedha yao kwa ajili ya miradi ya maendeleo wanataka itumike kwa kunufaisha walengwa na kwamba kinyume chake ni kuchafua jina la taasisi inayokuwa imeingia mkataba na wafadhili hao.
“Tutambue thamani ya fedha tunayopewa na wafadhili…Hakuna njia ya mkato…tunapokubali fedha yao kwa kuingia kwenye makubaliano (mkataba)lazima tukubali pia masharti wanayoyatoa juu ya matumizi ya fedha zao,” amesisitiza.
Mradi wa Utekelezaji wa Utu wa Mwanadamu unafanya kazi kupitia Idara ya Haki, Amani na Uadilifu Katika Uumbaji ambayo ipo chini ya Kurugenzi ya  Hadhi ya Ubinadamu (Human Dignity) ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na unatekeleza shughuli  zake kupitia Kamati za Mahusiano ya Dini Mbalimbali katika wilaya za Kasulu, Mbozi, Njombe, Ludewa, Karatu, Babati , Temeke na Mtwara chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Makanisa ya Norway (NCA).
Miradi inayotekelezwa kupitia miradi hiyo ni pamoja na kuwainua watu kiuchumi kupitia Benki za Kijamii Vijiji (IR-VICOBA), Ufuatiliaji wa Rasilimali za Umma zinazotolewa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Maendeleo (PETS) na Masuala Mtambuka yanayohusisha mahusiano ya dini mbalimbali na usaidizi wa kisheria.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU