Kardinali Pengo awapongeza waamini Kiwalani

Na Philipo Josephat, DSM

ASKOFU Mkuu  wa Jimbo Kuu Katoliki Dar  es  Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewapongeza  waamini, viongozi  na  watu  binafsi  wa Parokia  ya Mt. Kamili  Yombo  Kiwalani kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba  mpya  na  ya kisasa  ya  mapadri  parokiani  hapo.
Akizungumza  mara baada ya uzinduzi wa  nyumba hiyo, Kardinali Pengo amesema yeye binafsi  alitumia miezi 6 kukamilisha ujenzi  wa gereji yake ya kuhifadhia magari, lakini anashangaa moyo wa  waamini wa Kiwalani  wa  kujitoa kuijenga  nyumba  nzuri  na  ya ghorofa  kwa  muda mfupi.
Amewapongeza wote walioshiriki kwa hali na mali katika mchakato mzima mpaka uzinduzi wa nyumba ya mapadri, huku akiwaasa kuendelea na moyo wa upendo na kumshirikisha Mwenyezi Mungu.
Kardinali  Pengo  ametoa vyeti kwa watu binafsi waliochangia kukamilika kwa nyumba hiyo kwa niaba  ya viongozi wa parokia ambapo  vyeti  vingine vitatolewa  hapo  baadaye kwa  makundi  mbalimbali.
Awali, katika mahubili yake kwa vijana waliopokea Sakramenti ya kipaimara, Kardinali Pengo amewataka  vijana hao kumtangaza  Kristo  ya kuwa amefufuka  kweli.
“Mkristo  yeyote anapokuwa  hana  Yesu  kwenye  moyo  wake, ni msingi mkubwa  wa  kuwa na  wasiwasi,  hivyo maisha yenu yote yaongozwe na  kulindwa na ukweli kwamba Yesu  yupo  rohoni  mwenu kwa  njia  ya roho  anayetenda kazi,” amesema.
Mwenyekiti wa parokia hiyo, Robert Bamwebuga na viongozi wa  walei  parokia wamemshukuru Kardinali Pengo  kwa  kuitikia  wito wa  kufika parokiani hapo kwa ajili  ya  kutoa sakramenti ya  kipaimara kwa  vijana 109 pia kuzindua nyumba ya mapadri.
Kwa  upande  wake  Mwenyekiti wa  Kamati  ndogo  ya ujenzi ambayo  ilisimamia  ujenzi  wa nyumba  hiyo, Justus Bashara,  amesema nyumba  hiyo  imegharimu takribani  shilingi Mil. 187 mpaka kukamilika kwake. Amewashukuru wote waliojitoa kwa  ajili  ya  ujenzi  huo.

Paroko  wa parokia  ya  Mt. Kamili padri Festo Liheta ametoa shukrani  za  dhati  kwa  waamini  wote tangu  mwanzo  wa  ujenzi  hadi kukamilika kwake, pia amemshukuru  Askofu  Mkuu  Mwadhama  Polycarp Kardinali Pengo kwa kufika  parokiani hapo.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU