KUELEKEA MAHAFALI YA 19: SAUT YAJIVUNIA ELIMU BORA



CHUO KIKUU cha Mtakatifu Agustino (SAUT) cha jijini Mwanza kimeendelea kusifiwa kwa kutoa elimu bora hasa kwa njia ya vitendo kwa wananchi ndani na nje ya Tanzania.
Hayo yamebainika zikiwa zimesalia siku chache kabla ya chuo hicho kusherehekea mahafali yake ya 19 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998.
Afisa Uhusiano wa chuo hicho Living Komu akizungumza na gazeti la Kiongozi amesema kuwa SAUT ni chuo cha kujivunia kwa wanafunzi wote waliopita hapo kwa maana ni chuo kitoacho wanafunzi bora kitaaluma na kimaadili.
‘Ili uweze kutambulika na kuheshimiwa ni lazima uwe na nidhamu njema na pia taaluma iliyotukuka, hivyo kama chuo kinajitahidi na kimeweza kufanya kadri ya uwezo wake kuzalisha wanafunzi wenye vigezo bora vya kuuzika katika soko la ajira ya sasa na hata baadaye ndani na nje ya Tanzania,’ amesema Komu.
Amewakumbusha wanafunzi wote ambao wanakwenda kuhitimu katika mahafali ya 19 kuwa ni vyema watumie elimu na nidhamu waliyofunzwa hapo chuoni na kuwa kioo kizuri katika jamii.
Pia ameongeza kwa kusema kuwa wanafunzi wanaokwenda kuhitimu waendelee kupitia katika mitandao mbalimbali ya chuo kwa ajili ya kufuatilia taarifa zitolewazo kuelekea katika mahafali hayo ili kuwa na taarifa kamili na kufahamu utaratibu mzima.
Hata hivyo ameongeza kuwa wanafunzi wanaoendelea na masomo yao katika chuo hicho waendelee kusoma kwa bidii na juhudi zote na pia kuendeleza nidhamu ya chuo ili kutekeleza malengo na madhumuni ya maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) walipoanzisha chuo hicho kwa lengo la kutoa vijana wenye elimu njema na nidhamu bora.
Ametumia fursa hiyo pia kuwakaribisha ndugu na jamaa katika maonesho ya SAUT jamii (Community Day) yanayojumuisha wanafunzi na walimu wa vitivo vyote vya chuo hicho ambapo maonesho hayo huwa ya kitaaluma na huwa na mafunzo kwa jamii nzima ambapo yanatarajiwa kufanyika tarehe 6 Disemba 2017.
Hata hivyo chuo hicho kikuu cha SAUT kimewakaribisha wananchi katika mahafali yake ya 19 yatakayofanyika chuoni hapo tarehe ya 8 na 9 Disemba ambapo kinategemea wageni zaidi ya 6,000 kuhudhuria sherehe hizo ambazo zimechochewa na muamko wa wahitimu wengi wanaomaliza katika chuo hicho.
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino kinamilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambapo chuo hicho kimefanikiwa kuzalisha idadi kubwa ya wanafunzi wa ndani na nje ya nchi kwa kutoa elimu bora na endelevu kwa jamii bila ubaguzi.
Katika mahafali yake ya 19 tangu kuanzishwa kwake, takribani wanafunzi 2000 watatunukiwa shahada, astashahada na shahada ya uzamivu katika vitivo mbalimbali.


Na George Alexander, Mwanza


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU