‘Msiwabague mnaowatumikia’


·     



SFUCHAS yaendelea kuwezesha jamii maskini Tanzania

Na Pascal Mwanache, Ifakara
WANATAALUMA na wadau wa maendeleo nchini wametakiwa kuiga mfano wa jitihada zinazofanywa na Kanisa Katoliki nchini za kutoa huduma za kijamii kwa watu wote hasa wa vijijini bila kujali dini, kabila au ukanda.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe katika Mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Afya cha Mtakatifu Fransisko Ifakara (SFUCHAS) yaliyofanyika Novemba 11 chuoni hapo ambapo takribani wataalamu wa Sayansi za Afya 256 wamehitimu.
Dkt. Kebwe amesema kuwa SFUCHAS imekua mstari wa mbele katika kutatua changamoto za uhaba wa wataalamu wa afya nchini kwa kuwa wataalamu wengi wanaozalishwa na chuo hicho wanakuwa tayari kufanya kazi katika maeneo ya vijijini ambako kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu wa afya.
“Huu ni mwendelezo wa kazi iliyofanywa na wamisionari. Itakumbukwa kuwa wakoloni waliweka huduma za jamii sehemu walizokuwa na maslahi nazo. Lakini ninyi mnafanya kinyume, mnatoa huduma bila ubaguzi, kwa watu wote na maeneo yote” ameeleza Dkt. Kebwe.
Ameweka wazi kuwa SFUCHAS inafanya kazi kubwa ya kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa afya vijijini ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya wataalamu wa afya  hasa wafamasia na madaktari wapo Dar es salaam. Amewahimiza wahitimu waendelee kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, na kuakisi malezi bora waliyoyapata chuoni hapo.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Ifakara Mhashamu Salutaris Libena amesema kuwa mafanikio ya chuo hicho ni mwendelezo wa jitihada za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) za kuwekeza katika chuo hicho kitaaluma na kimiundombinu.
Askofu Libena ambaye aliongoza Misa Takatifu iliyotangulia mahafali hayo amewataka wahitimu hao wakawe wawakilishi wema kwa kuiishi taaluma na viapo vyao na kuzingatia maadili na kumpendeza Mungu.
“Tumekusanyika ili tuwatume vijana wetu hawa. Mahafali maana yake ni kuutangazia ulimwengu kuwa huyu anayetunukiwa cheti au zawadi hana deni pale chuoni. Tunawatuma kwenda duniani kote kwenda kutoa huduma kwa watu wote kama mlivyofundishwa mkiwa chuoni” ameeleza Askofu Libena.
Sherehe za mahafali ya chuo hicho zimeenda sambamba na uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi na Chuo cha Meno (Dental School) na kuweka jiwe la msingi katika jengo liitwalo Askofu Agapiti Ndorobo.
Kwa mujibu wa taarifa fupi iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala Padri Archilleus Ndege, jengo la Askofu Agapiti Ndorobo linajengwa kwa lengo la kufanikisha mafunzo ya wataalamu wa afya maeneo ya vijijini ili wakishahitimu wawe tayari kufanya kazi maeneo ya mbali na miji.
Jengo hilo lina vyumba vikubwa kumi na nne ambavyo vitatumika kwa shughuli za kumbi za kufundishia, maabara 2 na darasa la kufundishia teknolojia ya habari na mawasiliano-TEHAMA. Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa ekari kumi zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya ghorofa 4 mawili yenye vyumba 72 kila moja, jengo la maktaba, jengo la utawala, madarasa, shule ya meno, mgahawa pamoja na maduka.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU