TEC YAPONGEZWA NA SERIKALI UKUZAJI ELIMU NCHINI




NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya amelipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa juhudi, maarifa na busara kuamua kuwekeza katika sekta ya elimu hivyo kuwa chachu ya ukombozi wa Mtanzania.
Waziri Manyanya ameyasema hayo kwenye mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (RUCU) yaliyofanyika hivi karibuni kwenye viwanja vya chuo hicho na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Katoliki Ruaha, Askofu wa Jimbo Katoliki Njombe Mhashamu Alfred Maluma, wahitimu wa fani mbalimbali kutoka chuoni hapo na  wageni waalikwa kutoka sehemu mbalimbali.
Manyanya amesema kuwa Kanisa Katoliki kupitia Baraza la Maaskofu limekuwa mdau mkubwa wa elimu kabla na hata baada ya Uhuru, pia mshiriki mkubwa wa Serikali katika kuchangia ukuaji wa Elimu nchini na siyo katika elimu peke yake bali hata katika afya na huduma nyingine za kijamii.
Napenda pia kutumia fursa hii kulipongeza Kanisa Katoliki kwa juhudi kubwa hasa katika kukuza na kuendeleza elimu hapa Tanzania. Limekuwa mdau mkubwa wa elimu, afya na mjenzi wa amani kwa njia ya mahubiri yake, nalipongeza sana Baraza la Maaskofu kwa juhudi, maarifa na busara za kuamua kuwekeza katika sekta ya elimu," amesema Mhandisi Manyanya.
Mhandisi Manyanya amesema kuwa, elimu ni nyenzo kuu katika vita dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini, pia kiini cha maendeleo ya nchi yoyote duniani. 
"Leo wahitimu wanatunukiwa vyeti mbalimbali kuashiria kuwa wamehitimu viwango mbalimbali vya taaluma, ni imani yangu kuwa wahitimu hawa wamepata nyenzo za kutosha kuwawezesha kumudu na kuzikabili changamoto za ulimwengu wa sasa hasa katika kujenga Tanzania ya viwanda."
Vile vile Mhandisi Manyanya amesema kuwa utandawazi ni moja ya changamoto hizo kwa sababu umewaingiza katika mwingiliano wa mataifa katika nyanja za uchumi, siasa na utamaduni. Hivyo wanapoingia katika ushirikiano wa kiuchumi na nchi mbalimbali duniani ambazo nguvu kazi imekuwa huru kuhama toka nchi moja hadi nyingine, changamoto mbele yao ni ajira.
" Watanzania wanapaswa kuwa wameandaliwa kikamilifu kumudu ushindani huo katika soko la kimataifa la ajira ili wasije kufanywa vibarua ndani ya nchi yao, lakini pia wengine waweze kwenda nchi jirani na hata kwingineko na kukubalika kwa uwezo wao, mimi naamini kuwa wahitimu tunaowatunuku leo vyeti wameiva kitaaluma na changamoto hizi wakazikabili."
Amewataka wahitimu hao kutambua kuwa elimu waliyoipata imewaongezea uwezo mkubwa wa kufikiri zaidi kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizo mbele yao na kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi kwenye mahafali hayo Makamu Mkuu wa Chuo hicho Pd. Dk. Cephas Mgimwa amesema kuwa chuo hicho kilianzishwa  kwa juhudi za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa msaada wa serikali mwaka 2005 kuanzia kudahili wanafunzi 524 kwa kozi za cheti na shahada katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Kwa mujibu wa Dk. Mgimwa idadi ya wanafunzi kwa kozi mbalimbali imeongezeka hadi kufikia 5,212 kwa mwaka wa masomo 2017/2018 kati ya wanafunzi wote waliodahiliwa asilimia 43% ni wanawake na asilimia 57% ni wanaume.
Kozi zinazotolewa katika chuo zipo kwenye Vitivo na taasisi, vitivo ni vinne ambavyo ni Sanaa na Sayansi ya Jamii, Sheria, Biashara na Sayansi ya Menejimenti, Mawasiliano na Teknolojia.
Kwa upande wa taasisi zipo mbili katika ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu.
Aidha idadi ya programu zinazotolewa zimeongezeka kutoka 2 mwaka 2005 hadi kufikia 27 mwaka 2017/2018 ambazo zimeendeshwa kwa kuzingatia majukumu makuu ya vyuo vikuu ambayo ni kufundisha, kutafiti na kusaidia jamii.
Chuo hicho pia kinatafuta uwezekano wa kuwa na mfumo unaowezesha wahitimu kusoma ngazi zote za kozi husika kutoka astashahada hadi shahada ya uzamivu.
"Hivi leo tunashuhudia kuhitimu jumla ya wanafunzi 1,776 ambazo ni asilimia 93% ya wanafunzi wote waliodahiliwa kwa mwaka wa masomo 2017/18 kati yao wahitimu 1,776 watatunukiwa vyeti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na stashahada, stashahada na shahada za uzamili," amesema Dk. Mgimwa.
Akizungumzia watumishi na mazingira ya kazi, Dk. Mgimwa amesema kuwa chuo kwa sasa kina idadi ya watumishi 260 ambao 156 ni wanataaluma na 104 ni wafanyakazi katika utawala (administration) na kuna mpango wa kuongeza idadi ya watumishi kulingana na kasi ya ukuaji, na katika kutekeleza hilo chuo kimepeleka watumishi 22 masomoni ili kukuza taaluma zao na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Kuhusu ujenzi wa kampasi na ongozeko la programu, chuo kina mpango mkakati mpya 2016/2026  wa miaka kumi ukiwa na maeneo ya vipaumbele kama vile ujenzi wa shule (shools) katika maeneo yanayomilikiwa na chuo kama vile Igumbilo, Mgera, Mwangata na Mawelewele.
Dk. Mgimwa ameendelea kusema kuwa " Katika kufanikisha lengo la Baraza la Maaskofu Katoliki kuanzisha vyuo pale ambapo bado huduma ya elimu haijafika, RUCU kupitia mpango mkakati huo kimenunua na kuendelea kununua ardhi ndani na nje ya nchi, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Dodoma, Dar es Salaam, Katavi, Songwe,Morogoro, Kibaha na Tunduma, na nchi ya jirani zikiwa ni pamoja na Malawi na Zambia."
Katika kipindi kijacho chuo kimepanga kuendelea kuboresha miundombinu yake ili kukidhi mahitaji ya chuo kikuu kamili RUCU, na hii itahusu kuanzisha na kuboresha sera, miongozo na kanuni za utendaji pia kutafuta na kuwekeza maeneo mbalimbali ili kujihakikishia uendelevu wa progamu za chuo na kuajiri na kuendeleza wafanyakazi wa taaluma mbalimbali na utawala kulingana na uzito wa kazi zinazoendana na ukuaji wa chuo.
Chuo pia kimeishukuru serikali kwa misaada mbalimbali kwani misaada hiyo imehusisha ujengaji wa uwezo wa kiutendaji wa wafanyakazi (capacity building) utoaji wa miongozo ya ubora wa progamu (quality assurance), uwezeshwaji wa udahili na uhisani kwa wanafunzi wengi wa chuo hicho pia uhusishwaji wa chuo katika masuala ya elimu.

 Na Getruda Madembwe, Ruaha

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU