ASKOFU MAPUNDA AWATAKA WAAMINI KUTOTEGEMEA WAFADHILI

Na Rodrick Minja, Manyoni.

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Singida Mhashamu Edward Mapunda amewataka wakatoliki nchini kuondokana na tabia ya kutegemea wafadhili wakati wa utekelezaji na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka kujitegemea zaidi.
Askofu Mapunda ametoa wito huo kwenye misa takatifu aliyoiongoza wakati wa maadhimisho ya sherehe za Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la Parokia hiyo mjini Manyoni.
Amesisitiza kwamba suala la kujitegemea halina budi kupatiwa kipaumbele katika shughuli za kukamilisha ujenzi wa majengo ya makanisa pamoja na vigango.
Akifafanua zaidi Askofu Mapunda ameweka bayana kuwa jukumu la kukamilisha ujenzi wa makanisa ni la waamini wenyewe na wenye moyo ambapo hata hivyo amewatoa hofu waamini wa Manyoni kwa kuweka wazi kuwa anaamini kabisa waamini wa Manyoni ni waumini wenye moyo wa dhati wa kukamilisha majengo hayo.
Hata hivyo, Askofu Mapunda amewatahadharisha waamini wa Jimbo hilo kwamba suala la kujitegemea lina umuhimu wake na kwa hali hiyo hawana ujanja wa kulikwepa jukumu hilo la kuondokana na utegemezi kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili mapadri zikiwemo za kutokuwa na vyombo vya usafiri.
Naye Paroko wa Parokia  ya Kupaa Bwana Manyoni, Jimbo Katoliki Singida, Padri Thomasi Wambura  amesema mwaka jana ulikuwa mwaka wa Jubilei ya Miaka 100  wa Mapadri Tanzania, mwaka huu nao wanaadhimisha miaka 50 ya Jubilei ya Parokia yao na mwaka ujao wa 2018 wataadhimisha Jubilei ya miaka 150 tangu ukristo ulipoingia nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Padri Wambura waamini wote wana wajibu wa kuyatekeleza yale yote waliyoaswa na Askofu kama mchungaji wao Mkuu, lakini hakusita kusisitiza kwamba wajibu walionao ni kuyatekeleza yale waliyoyapata katika ukrito.

Kwa upande wao baadhi ya waamini wa Kanisa hilo akiwemo Elizabeth Mkyalu  wameshauri kwamba fedha zilizochangwa na waamini hazina budi kuanza shughuli zilizokusudiwa za ujenzi wa majengo hayo huku wakionya tabia ya kusubiri wafadhili kwamba kwa namna moja au nyingine hukwamisha miradi iliyoanzishwa pale wanapojitoa au kutochangia.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU