MAADHIMISHO MAZITO NA MATAKATIFU SANA YA PASAKA
Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Pasaka kwa namna ya
pekee sana katika Liturujia yake, wala hakuna sherehe nyingine yenye
maadhimisho mazito kama hayo tunayoadhimisha Pasaka.
Uzito wa Maadhimisho ya Pasaka
unatokana na matendo makubwa yanayoadhimishwa katika sherehe hiyo yaani mateso,kifo
na hatimaye ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu.Pamoja na kuadhimisha matendo hayo yaliyo kilele cha
ukombozi,kanisa huadhimisha matendo makubwa ambayo Yesu aliyafanya kabla ya
kuanza kwake mateso,ambayo ni kula Karamu ya mwisho na mitume wake na katika
nafasi hiyo aliweka Sakramenti za Ekaristi,Daraja takatifu na amri ya mapendo.Kanisa
huadhimisha matendo hayo makuu ya Pasaka katika Siku tatu kuu za Pasaka.
Licha ya kujiandaa kwa mfungo wa siku arobaini Juma
moja kabla ya kuadhimisha ufufuko wa Bwana, kanisa linaanza rasmi kuadhimisha
mateso ya Bwana katika Dominika ya Matawi ya Mateso ya Bwana.Kutokana
na uzito wa kuadhimisha mateso na kifo cha Bwana, kanisa limetoa jina maalum
kwa juma hilo kwamba ni Juma Kuu au Juma Takatifu.Juma hilo
huitwa JumaKuu au Juma Takatifu kwa sababu kilele cha Juma hilo ni kuadhimisha SIKU
TATU KUU ZA PASAKA.Siku tatu kuu za Pasaka huanza Alhamisi Kuu jioni
kwa kuadhimisha Misa ya Karamu ya Bwana na kufikia kilele siku ya Dominika ya Pasaka.
Padri Paul Chiwangu,TEC
Comments
Post a Comment