ASK.KILAINI:VURUGU SI SULUHU.
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki
Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini ametoa wito kwa watanzania kutojihusisha na
vurugu na vita visiwani Zanzibar, huku akiwaonya wanasiasa kutowashinikiza
wananchi katika kufanya maamuzi.
Ameeleza
hayo hivi karibuni na kuonyesha kusikitishwa na vitendo vinavyoashiria uvunjifu
wa amani Zanzibar, ikiwa ni pamoja na matukio ya milipuko ya mabomu na uchomaji
wa nyumba na ofisi.
“Tunapiga
magoti mbele ya Mungu kuomba amani na hata mara moja haiwezekani kukubaliana na
vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani. Tunasikitika na hatukutarajia kuona
matukio kama hayo yakitokea nchini mwetu, ambacho ni kisiwa cha amani Sisi kama
viongozi wa dini hatuingilii siasa ila tuna wajibu wa kushauri juu ya mwenendo
wan chi.” ameeleza Askofu Kilaini.
Askofu
Kilaini pia amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na wanasiasa katika kufanya
vurugu, na kusisitiza kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayopata suluhu kwa
kufanya vurugu, na badala yake amewaomba wadumu katika amani na maelewano kwa
kuwa hatma ya nchi yao ipo mikononi mwa wananchi wenyewe.
“Tunaomba
amani itawale huko Zanzibar, na inapotokea tofauti basi watafute namna ya
kwenda bila kuleta vurugu. Vurugu na vita siyo suluhisho katika kutatua
migogoro, hivyo katika kutoelewana ni lazima wafike mahali watafute suluhu kwa
amani. Watambue kuwa wote ni ndugu, wakianza mafarakano hakuna atakayepona”
amebainisha Askofu Kilaini.
Aidha
amewataka wananchi wote kuwa wazalendo na mabalozi wa amani na kuwaomba wapinge
hali ya vurugu inayohatarisha usalama na utulivu nchini, kwa kuwa wao ndiyo
wahanga wakubwa wa ukosefu wa amani. Ameleza kuwa ni jambo la busara kujifunza
kupitia katika nchi ambazo zilijiingiza katika vurugu kama njia ya kutafuta
suluhu na badala yake zikaingia kwenye machafuko yasiyokwisha.
“Vitendo
vya milipuko ya mabomu ni dalili za ugaidi, hivyo basi kila mtanzania anapaswa
kupinga aina yoyote ya vurugu. Tutafute suluhu kwa amani, vurugu haiwezi kuleta
amani. Hakuna nchi yoyote duniani iliyopata suluhu kwa vurugu. Tujifunze kwa
nchi ambazozilijiingiza katika vurugu na mpaka leo hawajapata muafaka”
ameongeza.
Pia
amezitaka pande zozote zinazokinzana kutafuta suluhu na kudai haki kwa amani.
Ameeleza kuwa vurugu ni kielelezo cha kupotea kwa utu, hivyo kila mmoja ana
wajibu wa kulinda amani.
Hivi
karibuni kumekuwa na matukio ya milipuko ya mabomu na uchomaji wa ofisi
Zanzibar, ambapo nyumba anayoishi Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar
Makame iliopo Kijichi nje kidogo ya mji wa Unguja imeshambuliwa kwa kulipuliwa
kwa bomu.
Paschal Mwanache,TEC
Comments
Post a Comment