TAIFA LINAKOSA DIRA KWASABABU YA KUZIKA AZIMIO LA ARUSHA- ASKOFU NYAISONGA

Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam.
BAADA ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kutoa Ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2018 unaobebwa na kauli mbiu “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu” (Mt. 28:19), Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda Mhashamu Gervas Nyaisonga amesema kuwa, ujumbe huo umeandikwa kulingana na nyakati za sasa ambapo taifa linahitaji kurejea Azimio la Arusha ili kuleta ustawi wa watu wote bila ubaguzi na bila kuchochea matabaka.
“Ujumbe huo umeandikwa ili kutafakari kwa kina mambo makubwa matatu:
Kwanza, Mwaka huu wa Jubilei ya miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania (1868-2018).
Pili, Mwaka wa 50 tangu Kanisa la Tanzania lilipounga mkono siasa ya Azimio la Arusha zilizosisitiza udugu, kumegeana, kuhudumiana na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Kanisa liliona azimio la Arusha lilikuwa linadai kudhihirisha imani kwa matendo (Yak. 2: 14-17).
Tatu, Kuhamasisha maandalizi ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa mwaka 2019,” amesema Askofu Nyaisonga.
Akizungumzia Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Askofu Nyaisonga amesema kuwa, Ujumbe  huo unaweka wazi uzito wa sadaka ya wamisionari wa kwanza walioleta imani ya kikristo mwaka 1860 kule Zanzibar na mwaka 1868 Bara.
Wamisionari wa kwanza walikuwa Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu na baadaye kidogo walifuatiwa na Wamisionari wa Afrika (White Fathers) na Wabenediktini. Kisha hapo yakaja mashirika mengine mengi kama vile Wakonsolata, Wakapuchini, n.k. Wamisionari wote hawa walielewa vizuri maneno yafuatayo ya Yesu:
‘Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi (Yn. 20:21).“Enendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi wangu mkiwabatiza kwa jina la Baba… (Mt. 28:19-20).
Maandiko Matakatifu yana ujumbe kama huo: “Pigeni tarumbeta katika Sayuni…takaseni kusanyiko kuu…’ (Yoel. 2: 1, 15-17 na Isaya 58: 1).
Ameeeleza kuwa, Wamisionari walielewa maana ya maneno ya Yesu kwao wenyewe na kwa watu wengine. Kuhusu nafsi zao walijua kuwa wakimtii Yesu Kristo watapata mara mia yale waliyoyatolea sadaka (Mt. 19:29). Kuhusu watu wengine walielewa kuwa kila mtu ana wajibu kwa mwenzake. Walitaka kuepuka jibu baya la Kaini kuwa mimi sio mlinzi wa ndugu yangu (Mwa. 4:9).
“Kwa wamisionari lengo lilikuwa uinjilishaji wa mwanzo. Kwetu sisi wamisionari wa nyakati hizi za utandawazi wa habari na elimu kuna nyongeza ya umisionari. Kwa upande mmoja tunafungwa na uinjilishaji wa mwanzo kwani bado wapo watu wanaopishana na Injili kwa kukosa wainjilishaji. Kwa upande mwingine tunaitwa kwenye uinjilishaji wa kuwasaidia wakristo kuuishi ukristo wao katika nyakati hizi za mwendo kasi na kazi katika tafsiri mpya ya ukweli na uwazi.
Ninakiri kuwa yapo mazuri mengi yanayoashiria kufanikiwa kwa umisionari. Hata hivyo, yapo yenye dosari. Hatuwezi kukwepa kusikia maneno ya nabii Yoeli: “Nirudieni kwa mioyo yenu…rarueni mioyo yenu…mkamrudie Bwana…tafuteni rehema…mpatanishwe na Mungu…” Tujifunge mikanda kazi haijaisha,” amesisitiza

Azimio la Arusha
Akielezea umuhimu wa Azimio la Arusha ASkofu Nyaisonga amesema kuwa, Kanisa liliona kwenye dira ya Azimio la Arusha tunu za kikristo zinazolenga ustawi wa watu wote bila ubaguzi na bila kuchochea matabaka. Ndio maana Kanisa halikuona haya kuunga mkono yale yalionekana kukubaliana na ukristo.
“Kanisa halitaona haya hata sasa kusifia tunu za kiutu zilizokuwemo kwenye Azimio lile ambalo liliaga dunia likiwa na umri wa miaka 24 tu (1967-1991) na sasa imetimia miaka 27 tangu liage dunia.
Kila asiyeona ulazima wa kumjali mnyonge, kumtetea, kumpigania, kumgawia rasilimali, na hata kufa kwa ajili yake hawezi kudhihirisha imani yake kwa matendo kadiri ya mafundisho ya Kristo na mitume. Azimio la Arusha lilijaribu kutuelekeza kwenye tunu hizo ambazo kila kukicha zinapuuzwa.
Kuna dalili kadhaa zinazonesha kuwa baadhi watu wameanza kugutuka kuwa tulifanya kosa kuzika Azimio la Arusha kwenye kaburi la kina kirefu. Tayari zinapendekezwa sera na sheria ambazo kwa undani zinadokeza kusudi la kumjali mnyonge, kumwinua mdogo anayejaribu kuinuka na kumtendea kwa haki aliyefanikiwa.
Tuendelee na kazi ya kurekebisha mapungufu kama ubinafsi uliokithiri, uhujumu wa uchumi unaofanya maisha ya watu wengi kuwa magumu zaidi, dhuluma, n.k.” amesisitiza.
Aidha, kwenye ujumbe wa Kwaresima wa Papa Fransisko wa mwaka huu anatumia maneno ya Yesu kuwa, “Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapunguka” (Mt. 24:12).
Papa anazitaja baadhi ya dalili za kupunguka kwa upendo kama ifuatavyo: tamaa ya fedha (1Tim. 6:10), kumkana Mungu na sakramenti zake, ugomvi, ulegevu wa imani, kutekwa nyara na anasa za dunia, ghasia, kujaribu kutokomeza vitisho au upinzani. Mfano mmoja wa vitisho vya watu ni watoto ambao hawajazaliwa.
Amesema kuwa watu wengine wanakusudia kuharibu ujauzito kwani wanaona watoto wao ni vitisho kwa hali au hadhi zao. Mabaya mengine ni ya kimataifa kama vita, wakimbizi, mauaji ya watu ya kiholela, n.k. Haya yote ndio uasi unaofanya upendo upoe na kufifia.

Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa
Askofu Nyaisonga amesema kuwa, tafakari hiyo inakuja mwaka huu wakati uchaguzi utafanyika mwaka kesho kwa sababu inajulikana kuwa mambo muhimu huhitaji maandalizi ya muda mrefu.
Kupata viongozi wazuri wa wananchi ni jambo muhimu sana. Wananchi wakipuuza shughuli hiyo muhimu, huliacha taifa likiyumbayumba kwenye bahari chafu ya utandawazi kama melikebu iliyokosa nahodha na tena iliyo na hitilafu kwenye injini yake. Matokeo yake huwa ni hasara kubwa au kuangamia.
“Tuna mifano mingi ya jinsi viongozi wa serikali za mitaa wasio na sifa za uongozi wanavyojichukulia sheria mikononi na kuwatesa watu kwenye ngazi za vijiji.
Kuna watu huwekwa mahabusu au kunyang’anywa mali zao kwa amri za wenyeviti na watendaji wa vitongozi au vijiji bila hata uongozi wa wilaya kujua. Tena baadae kesi hizo hufutwa bila mchakato stahiki wa kisheria. Watu wanateswa na wenye mamlaka  kwa sababu hawana maarifa ya sheria za kujitetea. Matendo hayo yanaitia dosari serikali katika ujumla wake.
Kutokana na hayo yote, wakati huu wa Kwaresima taifa linakumbushwa kuwa nafasi ya uongozi wa watu ni nafasi nyeti inayotaka udhati wa haki na ari ili watu wa Mungu wapate utulivu na ustawi.
Ni vyema  kila mwenye sifa ya kugombea nafasi hizo ajiandae kimwili na kiroho. Ni vyema kila mwenye haki ya kupiga kura, ajiandae vema kimwili na kiroho ili isije ikawa kwa uzembe wa wachache taifa au jamii ikajikuta matatani.
Tayari tuna viongozi wanaotuongoza hadi sasa. Tunawashukuru kwani tunaonja utulivu. Bila shaka huduma zenu zinatupa matumaini,” amesisitiza.
Amewaasa wananchi waendelee kujiandaa kupata viongozi watakaofaa huku akisisitiza, “Tusiuze haki zetu za kiraia kwa kunaswa na rushwa za masafa marefu na hata zile za papo kwa papo. Kama viongozi waliopo wanafaa na wana dira inayoweza kutusogeza mbele zaidi tusisite kuwapa nafasi hiyo. Na wao wasisite kuomba na kukubali utume huo.
Kama kuna sababu za wao kutoendelea kutuongoza, tuwasaidie wahitimishe vizuri ngwe yao. Huduma yao haitasahaulika kwani walitutoa mahali na watatufikisha mahali pengine.
Mwenyezi Mungu atujalie heri na baraka za Kwaresima hii. “Basi, nendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mt. 28:19-20).”


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU