MAANDALIZI YA SIKU YA WANAWAKE YAPAMBA MOTO DODOMA
n Na Dotto
Kwilasa, Dodoma.
KATIKA
kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambayo hufanyika kila
mwaka tarehe nane mwezi machi mwaka huu ,wananchi wa mkoa wa Dodoma hasa
wanawake wametakiwa kujitokeza kwa wingi kusherekea siku hiyo muhimu kwao.
Kauli mbiu katika maadhisho hayo kwa mwaka huu ni ‘Kuelekea
uchumi wa viwanda , Tuimarishe usawa wa jinsia ili kuwawezesha wanawake
vijijini.’
Akizungumza hivi karibuni kwenye kikao cha kamati ya maandalizi
ya Mkoa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Rachel Mutoka amesema katika
maadhisho hayo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo kutoa msaada wa
kisheria, kupima afya kwa hiari na kupanda miti.
Mbali na hayo Mutoka amesema wanawake wanatakiwa kujitokeza
ili kufanikisha maadhimisho hayo na kuweza kupata msaada wa kisheria
ambao utawasaidia kutatua migogoro katika jamii ikiwemo ya ndoa na
mirathi.
Akifafanua zaidi alisema mnamo tarehe mbili mwezi wa
tatu mwaka huu shughuli itakayofanyika ni kutembelea wodi ya wazazi
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kufanya usafi.
“Tunatarajia kufanya mambo mbalimbali zaidi kwa maendeleo ya
wanawake ambapo tarehe tano mwezi wa tatu tutatembelea kituo cha watoto yatima
katika kijiji cha matumaini na gereza la wanawake Isanga na tarehe sita mwezi
huo tutatembelea kituo cha wazee na Cheshire,” ameeleza.
Siku ya wanawake Duniani nchini Tanzania ilianza kuazimishwa
mwaka 1996 , ambapo maadhimisho hayo yamekuwa yakiandaliwa kitaifa na katika
ngazi ya Mkoa.
Comments
Post a Comment