NCHI YETU BADO INAHITAJI NGUVU ZA KUJENGA UCHUMI-ASK. NGALALEKUMTWA
n Na Getrude Madembwe, Iringa.
ASKOFU
wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amesema kwamba bado
nguvu inahitajika katika kuimarisha uchumi wa wananchi.
Askofu Ngalalekumtwa amezungumza hayo hivi karibuni wakati
wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu
alipotembelea wilaya ya Mafindi kugagua miradi mbalimbali wilayani humo.
“Uchumi wetu bado una shida sana nakaa na watu maeneo mengi
nazunguka hasa vijijini unaona jinsi watu wanavyohangaika kufanya shughuli ili
waweze kuwasomesha watoto wao.
Suala la muhimu wataalamu wa masuala ya kilimo na mifugo
watoe elimu ili kipato cha mwananchi kiongezeke,” amesema Askofu Ngalalekumtwa.
Aidha akizungumzia ujumbe wa kwaresma 2018 uliotolewa na
Maaskofu Katoliki Tanzania, Mhashamu Ngalalekumtwa amesema ni kawaida kwa
maaskofu hao kutoa ujumbe huo kila mwaka.
“Kila mwaka tunapenda watu wajue sisi viongozi wao wa kiroho
tunakazia mambo gani. Huwa tunasisitiza masuala yanayolenga kujenga haki,
upendo na umoja na haya yakiwepo ndipo maendeleo ya kweli yatapatikana,”
amesema Askofu Ngalalekumtwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri
David amesema kwamba kwamba katika halmashauri yake ukusanyaji wa mapato
unaongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2017 hadi Januari 2018 halamshauri
hiyo imekusanya bilioni 7.900 ikiwa ni asilimia 78% ya malengo na jitihada
walizojipangia.
Bw. David amesema kwamba mwaka 2015 hadi 2016 halmashauri
hiyo imekusanya bilioni 11.700 na mwaka 2016 -2017 wamekusanya bilioni 13.8
sawa na ongezeko la asilimia 22%.
“ Halmashauri yetu inatoa mchango mkubwa katika
ukusanyaji wa kodi tukishirikiana na mamlaka ya ukusanyaji wa mapato (TRA) na
mapato yetu yanaongezeka kila mwaka, ni jitihada za serikali ukusanyaji
wa mapato kutoka sekta mbalimbali kama vile viwanda na mazao ya misitu,”
amesema Bw. David.
Makamu wa Rais Suluhu ameipongeza halmashauri hiyo kwa
ukusanyaji mzuri wa mapato, wazalishaji wa chakula na ameahidi kuwa pembejeo za
kilimo zitapatikana kwa wakati na bei rahisi.
Aidha Bw. David amesema kuwa vyanzo vya ndani
ukusanyaji wa mapato pia umeongezeka kwani mwaka 2015 -2016 wamekusanya bilioni
4.396, mwaka 2016 – 2017 wamekusanya bilioni 4.882 na mwaka 2017 hadi Januari
2018 halmashauri imekusanya bilioni 2.289.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mufindi amesema kuwa halmashauri
yake imejiwekea mikakati mbalimbali katika ukusanyaji wa kodi na
wameimarisha vizuizi vya maliasili, wameziba mianya ya rushwa, pia halmashauri
hiyo ina asilimia 70% ya viwanda vinavyosaidia kuongeza mapato.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa
ambalo litakuwa na maabara 3 za sayansi, chumba kimoja cha kompyuta na vyumba
vya 5 madarasa mkondo wa kidato cha 5 na 6 katika shule ya sekondari ya Mgololo
iliyopo wilayani humo, mkurugenzi wa Halamashauri ya Mufindi Profesa Riziki
Shemdoe amesema kwamba mradi huo hadi ukamilike utagharimu Tsh. Milioni 450 na
umefadhiliwa na kiwanda cha Karatasi Mufindi (Mufindi Paper Milling MPM).
“Mradi huu unafadhiliwa na kiwanda cha karatasi
Mufindi na ulianza rasmi mwaka 2016 tunatarajia utakamilika ifikapo Aprili 2018
na utagharimu kiasi cha Tsh.Milioni 450, hadi sasa tumetumia Tshs. Milioni 325”
amesema Profesa Shemdoe.
Katika ziara yake Makamu wa Rais amefungua zahanati ya
Kising’a iliyopo katika halmashauri ya Iringa ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi
wakishirikiana na Asasi group Company waliochangia Milioni 125.
Katika Wilaya ya Kilolo Mama Samia amesema serikali itajenga
barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa Km. 35 iliyopo wilayani humo, pia
amefungua jengo la Utawala na madarasa 3 yaliyojengwa na halmashauri hiyo na
nguvu za wananchi wa maeneo hayo.
Akitoa majuisho kwenye ukumbi wa siasa ni Kilimo
uliopo katika halmashauri ya Iringa, Makamu wa Rais Suluhu amesema kwamba
amefurahiswa na utunzwaji wa mazingira katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa
Iringa na ametahadharisha kwamba kama watu wataendelea kukata miti hovyo bila
kupanda huenda hali ya hewa iliyopo itatoweka siku zijazo.
“Maeneo ya Mkoa huu yana sura 2, sura ya kwanza
mmetunza mazingira vizuri na sura ya pili inaonyesha kuna uharibifu wa vyanzo
vya maji kuna maumbile ya mabonde na milima, ongezeko la watu linakua , watu
wakae lakini wasifanye shughuli zozote kwenye vyanzo vya maji” amesema Makamu
wa Rais na kuongeza kuwa
“ Iringa ya miaka 10 hadi 15 iliyopita si kama ya
sasa, joto laanza, kateni miti na mpande miti, msiharibu pia vyanzo vya maji,
sharia ile watu wakae mita 60 kutoka vyanzo vya maji ifuatwe, msiharibu
kiharibu mnakumfuru Mungu”.
Ameutaka mkoa kuwa na mkakati katika suala la
kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI, ina asilimia 11% kitaifa Mkoa wa
Iringa unashika nafasi ya pili.
Makamu wa Rais amekuwa na ziara ya siku 5 mkoani Iringa na
amefungua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo mkoani humo.
Comments
Post a Comment