Kanisa liwe mfano wa kuigwa kufuata sheria za kodi-Katibu Mkuu TEC
IMEELEZWA kuwa Kanisa Katoliki nchini linapaswa kuonyesha mfano katika
kufuata taratibu zote za kodi kwa kuwa sheria za kodi zinazosimamiwa nchini
zilikuwepo kwa muda mrefu ila zilikuwa hazisimamiwi na kufuatiliwa.
Hayo
yameelezwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padri Raymond
Saba wakati akifungua semina ya siku nne kwa wahasibu na wasimamizi wa miradi
wa majimbo katoliki mbalimbali nchini, inayofanyika katika Kituo cha
Kurasini-Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Semina
hiyo inayolenga kuwajengea uwezo wa usimamizi wa fedha na miradi washiriki hao
imeandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki
(AMECEA) kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Padri
Saba amesema kuwa majimbo hayana budi kufuata utaratibu wa kujisajili, kuhakiki
mahesabu, na kuongeza kuwa uhakiki huo ni lazima uanze katika ngazi za parokia.
“Kama
Kanisa tunapaswa kuwa mstari wa mbele kufuata sheria za kodi za nchi. Sheria na
taratibu hizi siyo ngeni, zilikuwepo katika nchi yetu ila zilikuwa hazisimamiwi
vizuri na kufuatiliwa” ameeleza Padri Saba
Kwa
upande wake Naibu Katibu Mkuu wa AMECEA Padri Chrisantus Ndaga amewaambia
wahasibu hao kuwa semina hiyo inapaswa iwajengee uwezo utakaosaidia taasisi
mbalimbali zilizoko majimboni na kugusa ngazi ya chini katika parokia.
“Semina
hii iwasaidie na ninyi mkaandae semina kama hizi huko majimboni. Tukumbuke kuwa
mambo haya ya fedha na miradi yanagusa taasisi ambazo majimboni kwetu ziko
nyingi. Kwa hiyo sisi tunalo jukumu la kufikisha ujuzi huu katika ngazi ya
chini kabisa, ikiwezekana hata katika jumuiya ndogo ndogo” amesema Padri Ndaga.
Na Pascal Mwanache, Dar es salaam
Comments
Post a Comment