Papa Francisko: Tarehe 23 Februari 2018 ni Siku ya Kufunga na Kusali
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4 Februari 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ametangaza kwamba, tarehe 23 Februari 2018, Ijumaa ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wafunge na kusali, kwa ajili ya kuombea amani duniani. Lakini kwa namna ya pekee, kuombea amani huko DRC na Sudan ya Kusini ambako watu wanateseka sana kutokana na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii na kinzani mbali mbali.
Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika hata waamini wa dini mbali mbali kuungana naye kutekeleza dhamana na wajibu huu wa kimaadili kadiri ya taratibu, sheria na kanuni za dini zao, lakini watu wote kwa pamoja, waweze kumlilia Mwenyezi Mungu ili amani ya kweli iweze kupatikana katika maeneo haya ambayo watu wake wanateseka sana kwa vita. Anasema, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, daima anasikiliza kilio cha watoto wake, wanaomkimbilia kwa machozi na mateso makubwa wakiomba msaada wake, ili kuwaponya waliopondeka moyo na kuzingaga jeraha zao.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao, ili hatimaye, kuweza kusikiliza kilio cha mateso na mahangaiko ya wananchi wa DRC na Sudan ya Kusini. Anawataka wajiulize swali la msingi, Je, wao wanaweza kufanya nini ili kudumisha amani na utulivu! Jibu la kwanza kwa hakika anasema Baba Mtakatifu ni kusali na kila mmoja kujizatiti kuachana kabisa na vitendo vinavyochochea: vita, ghasia na mipasuko ya kijamii. Hii inatokana na ukweli kwamba, ushindi unaopatikana kwa njia vita na ghasia ni ushindi batili, lakini kushikamana kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani, ni msaada mkubwa na mafao ya wengi!
Baba Mtakatifu Francisko amechukua fursa hii kwa ajili ya kuonesha uwepo wake wa karibu, kwa familia ya Mungu nchini Madagascar, ambayo hivi karibuni, imekumbwa na tufani kali ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao; makazi ya watu kuharibiwa vibaya sana na hivyo, kusababisha wimbi kubwa la watu wasiokuwa na makazi ya kudumu. Kwa watu wote hawa, Baba Mtakatifu amewaombea msaada na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Vatican News!
Comments
Post a Comment