Mama ajifungua watoto watano, wote wafariki
n Na Doreen Aloyce, Katavi
Hivi
karibuni mama mmoja kwa jina la Spora Yohana (30) Mkazi wa kijiji cha
Wachawaseme kata ya Utende Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi amejifungua watoto
watano ambao wote wamefariki dunia baada ya kukosa msaada wa wataalamu wa Afya.
Akizungumza na gazeti hili Spora (mama wa watoto hao)
amesema kuwa,
alijifungua watoto watano wa kiume watatu na wawili wa kike
kabla ya wakati maana amejifungua wakiwa na miezi nane badala ya tisa.
“Nilijifungulia nyumbani majira ya saa kumi na moja asubuhi
nilipoanza kusikia maumivu makali na hatimaye kuanza kujifungua mmoja baada ya
mwingine na mpaka kufikia saa mbili nilimaliza na kujiandaa kupelekwa kwenye
Zahanati.
Sikuenda hospitalini mapema kutokana na kwamba sikutarajia
kujifungua kwani muda wake ulikuwa bado hivyo alidhani ni maumivu ya
kawaida ambayo nimekuwa nikiyapata siku zote kutokana na tumbo langu kuwa
kubwa.
Baada ya kujifungua, watoto wangu wakaugua wote kwa pamoja
na kupoteza maisha tukiwa kwenye jitihada za kuwakimbiza hospitalini,” amesema
Spora.
Akizungumza kwa unyonge Spora kuhusiana na tukio hilo
amesema kwamba amesikitishwa na tukio hilo kwa jinsi alivyohangaika kubeba
mimba iliyosababisha tumbo kuwa kubwa kuliko kawaida ijapokuwa alikuwa
akifurahia kuhisi watoto wake wakicheza ingawa alikuwa hafahamu kuwa amebeba
watoto watano.
“Nimebeba mimba ya watoto watano, nimejifungua watoto
watano. Ingawa wamefariki mimi ni mama wa watoto watano hivyo siko tayari
kubeba ujauzito tena. Nawaombea tu kwa Mungu watoto wangu wapumzike kwa amani,”
amesema Spora.
Mganga Mkuu wa Zahanati hiyo Daktari Lucia Kafumu
ameeleza kuwa mama huyo walimpokea majira ya saa nne asubuhi akiwa amejifungua
watoto wake ambao walipoteza maisha kabla ya kufika hospitali na kupatiwa
huduma ya afya.
Amesema kuwa kutokana na miezi ya watoto hao kama
wangepatiwa huduma wakiwa kwenye zahanati wangeweza kuokoa maisha yao huku
akisema changamoto kubwa ni elimu kwa wananchi kwani bado wana mila potofu za
kuwaamini waganga wa kienyeji na wakunga jambo ambalo linasababisha vifo kwa
akina mama wengi.
Amewataka wananchi hususani wajawazito kuwa na kasumba ya
kufika kwenye zahanati kwa ajili ya kupata huduma stahiki za afya na kupunguza
vifo vya mama na mtoto.
Comments
Post a Comment