Mchezo wa kamari na upatu ni hatari sana kwa maisha ya watu!

Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II “Consulta Nazionale Antiusura, CNA”, inayoundwa na wajumbe 300 kutoka sehemu mbali mbali za Italia, imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwa faragha. Tukio hili limetanguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baadaye, wajumbe wamepata pia nafasi ya kusali kwenye kaburi la Mtakatifu Yohane Paulo II ili kumwomba, ulinzi na tunza yake katika mapambano dhidi ya mchezo wa kamari na upatu, unaowatumbukiza watu wengi katika majanga ya kiuchumi, ugonjwa wa sonona, msongo wa mawazo na mfadhaiko wa akili. Ni mchezo wenye madhara makubwa kwa waathirika, familia na jamii katika ujumla wake! Monsinyo Alberto D’Urso, Rais wa Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II anasema, wameomba kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwa faragha, ili kumshirikisha uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi na hasa maskini wanaotumbukizwa katika majanga ya maisha kutokana na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka!
Monsinyo Alberto D’Urso, anaendelea kufafanua kwamba, kuna umati mkubwa wa watu wanaojitolea ili kuwasaidia waathirika pamoja na familia zao kuondokana utegemezi huu ambao ni hatari sana kwa utu na heshima yao. Kwa hakika, hawa ni watu wanaotafuta faraja, amani na utulivu wa ndani kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba wa maskini na faraja kwa watu waliokata tamaa! Baba Mtakatifu Francisko amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini na huduma hasa kwa maskini na wale wanaokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbali mbali!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Vatican News!

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI