KUELEKEA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA ASK. MKUDE ATAHADHARISHA
‘Haki itendeke kwa wote’
Na Pascal Mwanache, Morogoro
NCHI inapojiandaa kutekeleza haki
ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote kuchagua viongozi wa serikali za mitaa,
vijiji na vitongoji hapo 2019 wito umetolewa kwa vyombo husika kuwa walinzi wa
watanzania wote kwa haki bila kuminya haki za watu wengine.
Wito huo umetolewa na Askofu wa
Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude katika Misa Takatifu ya
Jumatano ya Majivu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mt. Patriki Morogoro.
Askofu Mkude amesema kuwa kila mmoja anapaswa kujitathmini iwapo amekuwa mlinzi
wa mwingine au amewatendea mema wale tu waliokuwa upande wake.
“Tunapojiandaa na uchaguzi mdogo
katika serikali za mitaa tujiulize, mtazamo wetu juu ya jirani upoje? Tumekuwa
walinzi kweli. Tumekuwa walinzi wa watanzania wote? au tunakwenda na mawazo
gani, kwamba ndugu kwangu mimi ni yule ninayetoka naye mtaa mmoja, au familia
moja tu? Mwingine siyo ndugu yangu? Kama
mkiwapenda wale wanaowapenda tu basi hamna mastahili, maana hata wapagani
hufanya hivyo” amesema.
Akifafanua juu ya ujumbe wa
kwaresima uliotolewa na Maaskofu, Askofu Mkude amesema kuwa mmaskofu wanataka kila
muumini ajibu swali aliloulizwa Kaini kuwa ‘ndugu yako yuko wapi na ana hali
gani.
“Maaskofu wanataka kuona kuwa kila
mmoja ajione mlinzi kwa ndugu yake, hususani ndugu aliyeumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu. Tunapowaona ndugu zetu wakiwa kwenye mahangaiko je tunaridhika au
tunaumia na kutusumbua ili tufanye kitu kwa ajili yao?” amehoji.
Pia Askofu Mkude amewataka waamini
kujikubali kuwa wao ni wamisionari, ambapo Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya
Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, kila muumini anapaswa ajitathmini.
“Maaskofu katika umoja wetu
tumewaandikia barua ya pekee katika kipindi hiki cha kwaresima. Barua
inatuelekeza kuwa, Kanisa lote la Tanzania linatafakari upendo wa Mungu
ulivyokuja na kutua Bagamoyo kwa njia ya Shirika la Roho Mtakatifu mwaka 1868. Zamu yetu imefika kushika na
kuendeleza mwanga wa upendo wa Yesu ulioletwa nchini miaka 150 iliyopita”
ameeleza.
Aidha ameongeza kuwa mwanga huo
hautakiwi kuzimika na kufia mikononi mwa waamini, hivyo ni lazima wawe
wamisionari, wawaendee watu na kuwafikishia mwanga huu.
“Wale wakatoliki waliolegea katika
imani yao, na wale wanaotafsiri vibaya Biblia wakawapotosha watu wanahitaji nao
kujua mwanga halisi na Bwana halisi Yesu Kristo. Umisionari haukuisha katika
kipindi hiki cha miaka 150, ni lazima uendelee” amesema.
Comments
Post a Comment