Nchi za AMECEA zaaswa kujitathmini kama zimefikia madhumuni ya waasisi
n Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam
Nchi
wanachama wa Umoja wa Mabaraza ya maaskofu Afrika Mashariki na Kati (AMECEA)
zimepewa changamoto ya kujitathmini kama zimefikia malengo ya umoja huo tangu
miaka ya 1960-2018.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa AMECEA Padri
Dr. Ferdinand Lugonzo katika semina ya siku nne kwa wahasibu na wasimamizi wa
miradi wa majimbo katoliki mbalimbali nchini, inayofanyika katika Kituo cha
Kurasini-Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Padri Lugonzo amesema kuwa, AMECEA ilizaliwa kwa lengo la
kuwa na mbinu za pamoja za kichungaji kwa maslahi ya watu wa kanda hiyo
ya AMECEA.
Miongozo ya Mababa waanzilishi wa AMECEA ilikuwa kuimarisha
na kuendelea katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha Imani Katoliki na
maendeleo ya jamii katika kanda hiyo.
Pia lengo jingine lilikuwa ni kuwa na Mpango Mkakati
wa muda mrefu uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa AMECEA (Plenary)
uliofanyika Julai 1961 Msimbazi, Dar es Salaam ukiwa na dhamira kuu ya
“Kesho ya Kanisa la Afrika.”
“Katika mkutano huo mkuu (1961) palikuwa na ajenda
saba ambazo ninapenda leo mzipitie muone kama mwaka huu 2018 tumefikia wapi
kama TEC na kama majimbo ya Tanzania na parokia zenu.
Ajenda ya kwanza ilikuwa Kanisa na Vyombo vya habari:
Uanzishwaji wa vituo vya televisheni, radio na uchapishaji wa magazeti. Je,
Tanzania imefikia wapi na inatumiaje hivi vyombo kufikisha lengo msingi la
AMECEA? Je, hali ya mada hii katika nchi wanachama wa AMECEA imefika wapi?
Ajenda ya pili ilikuwa, Mafunzo ya Kiroho kwa Mapadri wa
majimbo, ya tatu Mahitaji ya Kituo cha uchungaji na malezi
endelevu, .
Ajenda ya nne ilikuwa ni uwezekano wa kuwa na Chuo
Kikuu cha AMECEA au angalau Chuo Kikuu kishiriki. Ya tano ni kuwa na
Programu ya Kujitegemea .
Agenda ya sita ilikuwa Muelekeo wa Shule za
Kikatoliki na Elimu Katoliki (haja ya kuwa na silabasi ya dini ya
kikristo) na ya saba ni Haki na Masuala ya Amani katika ukanda wa AMECEA.
Jukumu kubwa la AMECEA ni kuhamasisha na kuwezesha familia
ya Mungu kuwa na moyo wa uinjilishaji na maendeleo mfungamano.
Kuwa manabii wa kumshuhudia Kristo katika ukanda wa AMECEA,
kuwa mashahidi na manabii wa Kristo, kwa kukuza umoja, haki, amani .
Tufikiri na kutenda zaidi ya kile kilichopo kuanzia ngazi
ya Baraza yaani taifa, kushuka kwenye majimbo na parokia zetu na kukabiliana
na masuala pana ambayo yana umuhimu na kuligusa bara letu na Kanisa
la kiulimwengu.
‘Tufikiri kiulimwengu tutende kiafrka kwa kuchukua mada za
kiulimwengu na kuzifanyia kazi katika mazingira yetu kama vile nyaraka
mbalimbali za Kanisa, masuala ya umoja wa mataifa nk,” amesisitiza Padri
Lugonzo.
Amesisitiza mapadri, maaskofu na waamini kufanyia kazi
masuala ya kimataifa yanayogusa ukanda wa AMECEA akitolea mfano wa majimbo
mangapi, parokia, jumuiya ndogondogo na familia wanajua waraka wa ‘LAUDATI SI’
wa Papa Fransisko ambao ni waraka kuhusu Mazingira na mabadiliko tabia nchi.
Amesisitiza umuhimu wa kujua mada za kimataifa na mada za
kiulimwengu kuanzia ngazi ya taifa, majimbo, parokia na familia ili kuzifanyia
kazi katika mazingira ya kiafrika.
Padri Lugonzo ametoa mada pia kuhusu utawala wa
mali za Kanisa na rasilimali.
Akisisitiza juu ya uelewa wa jinsi Kanisa linavyofanya
kazi kwa kuhusisha utume wa Kanisa, Ushirikiano, Miundo mbinu na Utawala.
“Lengo kuu la Kanisa ni kuinjilisha na kwa wale watawala
wenye mamlaka wanapaswa kutoa ushirikiano na watendaji ili kufanikisha shughuli
za Kanisa. Bila ushirikiano katika shughuli za maendeleo tutakwama mahali.
Katika kusimamia rasilimali za Kanisa na kupata maendeleo
yenye tija lazima kutumia wataalamu kwa kuweka watu stahiki katika kazi stahiki
awe mlei ama mkleri ilimradi awe na taaluma na uzoefu wa kazi ili tupate
ufanisi,” amesisitiza Padri Lugonzo.
Ameziasa taasisi za Kanisa na idara zake kuwa na miongozo,
kanuni na sera hasa kanuni za fedha, uchungaji nk. ili kuwe na utaratibu
unaoeleweka kuanzia ngazi ya taifa, majimbo na parokia na waamini wajue na
kuelewa kanuni hizo.
Amesema miongozo na kanuni hizo ziwe wazi na siyo za
mtu mmoja.
Amesema kuwa, Kanisa halifanyi kazi na mtu mmoja, hivyo
katika kumiliki rasilimali lazima kuwe na sera ambayo si ya mtu binafsi bali ya
taasisi ili kuepuka changamoto ya kufanya kazi kiholela na kukwama pale
mtendaji anapoondoka.
Ametaka Baraza la Maaskofu ambalo linashikilia ngazi ya
kitaifa kuwezesha ofisi za majimbo na vitengo vyake kuwa na miongozo stahiki
inayoongoza idara zao na kuwa na wataalamu wa kuendesha shughuli za maendeleo.
“Tuwe na ushirikiano wa ofisi za taifa, majimbo na parokia
ili kuwa na mifumo rasmi inayoongoza hususani kwenye fedha na umiliki
rasilimali zote za Kanisa.
“Mfuate sera na miongozo ya nchi ili kukwepa matatizo.
Makanisa yetu, shule, ardhi, hospitali nk. ziwe na vibali vya umiliki (umiliki
wa halali) ili kukwepa changamoto za kunyang’anywa ardhi na huko ndiko kufanya
kazi kwa kutumia taaluma,” amesisitiza.
Hata hivyo amesisitiza kuwa, katika nyanja zote za Kanisa,
cheo ama kazi mtu anayopewa lazima atangulize moyo wa kujitoa kufanya
huduma na uinjilishaji kwasababu Kanisa Katoliki lipo kwa ajili ya huduma na
uinjilishaji.
Viongozi pia wameaswa kuajiri watu sahihi katika kazi sahihi
kulingana na taaluma na uwezo wao ili kuzuia kufanya kazi chini ya kiwango.
Yapo mengi ya kujitathmini yakiwemo maendeleo ya jumuiya
ndogondogo ambayo ni uhai wa Kanisa, kupambana na umasikini na maradhi ukiwemo
ugonjwa wa ukimwi , kuzifanya familia za kiafrika kuwa chombo za uinjilishaji
nk.
Ikumbukwe kuwa nchi wanachama wa AMECEA ni Elitrea,
Ethiopia, Tanzania, Uganda, Zambia, Sudani, Kenya, Uganda na Malawi.
Comments
Post a Comment