KIONGOZI MKRISTO ASIYEWAJIBIKA AJITATHMINI NDANI YA KWARESIMA
Mwanasheria na Mhadhiri
wa kimataifa kuhusu Afrika P.L.O Lumumba aliwahi kusema kuwa moja ya matatizo
makubwa Afrika ni kwamba Viongozi wengi wa Afrika hawana sifa ya kuwa Viongozi.
Kwa miaka miwili sasa anaisifia Tanzania kuwa ni kinara cha kuigwa Afrika.
Muda huu wa Kwaresima
wale wote wenye nyadhifa za uongozi wa dini na serikalini wajihoji kuhusu
majukumu waliyopokea. Musa alilelewa kwenye ikulu ya Farao, mfalme wa Misri kwa
muda wa miaka 40. (Mdo 7: 20 -23) Kwa miaka 40 alifanya kazi ya kuchunga kondoo
wa Baba Mkwe wake Yethro huko Midiani (Mdo 7:30).
Akiwa na umri wa karibu
wa miaka 80 Mungu alimpa kazi mpya ya kuongoza watu na kuwatoa Utumwani (Mdo
7:30 - 34). Musa alimwambia Mungu ‘Kwanini umenitwisha mzigo wa watu hawa juu
yangu’ (Hesabu 11:11-12).
Kiongozi anabeba Taifa
lote kichwani mwake, Musa alihoji kila mara ‘nipate wapi nyama ya kuwapa watu
wote hawa’ (Hes 11:13). Sehemu nyingine alihoji ‘nipate wapi maji ya kuwapa
watu wote hawa wanywe’ Musa alikiri mbele ya Mungu ‘mimi siwezi kuwachukua watu
wote hawa peke yangu’ (Hes 11:14). Kazi ya uongozi wa aina yeyote ile ni mzigo.
Musa angelipendelea kuishi kwenye raha za ikulu ya Farao lakini ‘alipokuwa mtu
mzima’ akatoka ikulu kwenda kuona ndugu zake ‘akatazama mateso na mizigo yao’(Kut
3:11).
Musa alipenda kubaki jangwani
na kuchunga kondoo bila bugudha yeyote lakini ‘nitakutuma sasa uende kwa Farao,
kuwatoa watu wangu’ (Kut 3:10). Mungu alimtuma Musa kwenda kutatua matatizo ya
wananchi ‘kilio cha wana wa Israeli kimenifikia, nimeyaona mateso yao’ (Kut
3:9). Nenda ‘kawatoe watu wangu’. Kazi ya kiongozi ni kuwapeleka wananchi
kwenye ‘nchi njema, pana na iliyojaa maziwa na asali’ (Kut 3:8). Kila mara
kiongozi atafute maslahi mapana ya nchi yake. Kiongozi awafikishe wananchi
kwenye nchi njema yenye neema na ustawi.
Tatizo kubwa kwetu kila
mtu akipata nafasi ya uongozi anaanza kutafuta maslahi binafsi. Kiongozi
anaanza kuwaneemeshe ndugu na jamaa zake. Kiongozi anaanza kuiba mali ya wananchi
kujitajirisha. Hivi karibuni tumeona huko Zimbabwe na Afrika ya Kusini. Yesu
alisema ‘Njoni kwangu mnaoteseka na kusumbuka nami nitawapumzisha’. Tuliwahi kuona huko Filipini wakati wa Rais
Markus na mke wake Imelda. Dhambi ya Mfalme Ahabu na mkewe Jezebel inaendelea
mpaka leo.
Kinachosikitisha sana ni
kwamba baadhi ya hawa viongozi wanaofanya haya ni wakristo wabatizwa. Hata
Viongozi wa kanisa wameingia mtego wa dhambi ya Ahabu na Jezebel. Viongozi
wengi wa kanisa hawana tena roho ya kinabii. Viongozi hawa wanajilimbikizia
mali binafsi na kuwasahahu maskini na wanyonge.
Uongozi mbaya
huliteketeza Taifa. Wimbi la wakimbizi toka Ethiopia kwenda Afrika Kusini ni
kwa sababu wanakimbia hali mbaya ya nchini kwao. Sijasikia watanzania
wanakimbia kwenda Ulaya. Ulaya na Amerika zilijengwa kwa jasho la watu wengi
waliopita wakazifanya nchi zao ziwe za maziwa na asali. Kwa mantiki hiyo viongozi
lazima wajenge nchi zao ziwe nchi za Maziwa na asali. Viongozi wa kanisa pia
wajenge makanisa yao yawe ya Maziwa na Asali.
Kiongozi lazima atafute maslahi mapana ya nchi yake.
Kama kiongozi anatafuta
maslahi mapana ya Taifa lake na kusikiliza kero za wananchi wake basi Mungu
alisema ‘Mimi nitakuwa pamoja nawe’(Kut 3:12). Wote wanaopinga Uongozi kwa hila
na wivu wanastahili adhabu. Aliwapa ukoma Miriamu na Haruni.(Kut 12: 1-9) Wana
wa Kora pia walipewa adhabu( Kut 16: 1-35)
Wakati wa kwaresima kila
mtu ajiulize Je mimi ni kiongozi bora? Au ni mfuasi wa Mfalme Ahabu na mkewe
Jezebel? Au tunataka kufanana na Musa?
Tuzinde Mgassa OSB
Sakarani Tanga 0717312239
Comments
Post a Comment