KALENDA YA LITURUJIA NI KWA AJILI YA WAKRISTO WOTE
Kalenda ya Liturujia ni kwa ajili ya
Mapadri na watawa? La, hasha! Hiyo siyo kweli. Kalenda ya Liturujia inaandaliwa
ili kila Mkristo aweze kuitumia. Kalenda ya Liturujia ni kwa ajili ya kutumia Wakristo
wote wakatoliki.
Kalenda ya Liturujia
Kalenda ya Liturujia ni mwongozo wa
kiliturujia ambao hutolewa na Idara ya Baba Mtakatifu huko Vatikano – Roma,
Idara inayosimamia Liturujia Takatifu; mwongozo huo unawekwa katika lugha ya Kiswahili
na Idara ya Liturujia ili kuwawezesha Wakristo wakatoliki nchini waweze
kutumia. Kalenda hiyo huandaliwa kila mwaka kwa ajili ya Maadhimisho
ya Misa na kwa ajili ya kusali Sala ya Kanisa.
Kalenda ya Liturujia siyo ya
kutundikwa ukutani, bali inaandikwa kwa mtindo wa kijitabu kidogo chenye kurasa
takriban 150 ili kwamba Mkristo akishajipatia anaweza kuiweka mfukoni na
kusafiri nayo kwa urahisi. Kwa kuwa inatoa mwongozo wa kuadhimisha Misa na
kusali Sala ya Kanisa, baadhi ya waamini wamekuwa na fikra kwamba inatengenezwa
kwa ajili ya Mapadri ambao wanaadhimisha Misa na kwa ajili ya watawa kwa ajili
ya kusali Sala ya Kanisa. Hizo si fikra sahihi; siyo Mapadri na watawa peke yao
wanaosali Misa.
Siku ya Dominika kila Mkristo
anawajibika kwenda kanisani kumwabudu Mungu kwa kushiriki Misa na wenzake. Miaka
ya nyuma Wakristo wengi walifikiri kusali Masifu yaani Sala ya Kanisa ilikuwa
wajibu wa Mapadri na watawa peke yao. Wakati huo Sala hiyo iliitwa na wengine
eti ni sala ya watawa. Polepole
mawazo hayo yamesahihishwa, na waamini wengi wanatambua kwamba hiyo ni Sala
rasmi ya Kanisa zima. Katika parokia
nyingi sasa Wakristo husali Masifu ya Asubuhi pamoja kabla ya kuanza
kuadhimisha Misa. Ili waweze kujiandaa vizuri kwa kushiriki kusali Masifu ya
Asubuhi na kushiriki Misa, Kalenda ya Liturujia ni msaada mkubwa.
Yaliyomo
ndani
Ukiwa na Kalenda ya Liturujia mwanzoni
kabisa kuna Maelezo ya msingi kuhusu Sherehe na Sikukuu ambazo tarehe zake
hubadilika kila mwaka. Tofauti na Sherehe ambazo tarehe zake zimepangwa,
hazibadiliki, kama Noeli(25.12), Bikira
Maria Mama wa Mungu (1.1), Mtakatifu Yosefu mume wa Mama Bikira Maria(19.3),
Kutangazwa kuzaliwa kwa Bwana 25.3), na nyinginezo, Kalenda ya Liturujia inatoa orodha ya Sherehe na Sikukuu ambazo tarehe zake
hubadilika kila mwaka kama Dominika ya I ya Majilio, Familia Takatifu,
Jumatano ya Majivu, Pasaka, Pentekoste na Sikukuu nyingine. Hapana budi
kila Mkristo afahamu tarehe za Sikukuu hizo ambazo tarehe zake hubadilika mwaka
hata mwaka.
Kalenda ya Liturujia hukuletea tofauti
kati ya Sherehe, Sikukuu na Kumbukumbu. Baada ya maelezo kuhusu ya
Maadhimisho hayo mbalimbali, hufuata Kanuni za jumla mintarafu Mwaka wa Kanisa
na Kalenda. Mkristo anapata pia maelezo kuhusu aina mbalimbali za kuadhimisha
Ekaristi
Takatifu. Katika sehemu hiyo kuna maelezo ya Misa anapoongoza Askofu,
Misa ya Parokia, Misa katika Shirika au Jumuiya ya waamini, Misa ambayo Mapadri
wengi hushirikiana pamoja na maelezo mengine muhimu. Mkristo akijisomea hayo
yote huelimika vizuri kuhusu Liturujia.
Baada ya maelezo kuhusu Misa
mbalimbali, Kalenda ya Liturujia hutoa maelezo kuhusu Sala ya Kanisa. Jambo linaloulizwa mara nyingi na baadhi ya
waamini kuhusu kufunga, Kalenda hutoa pia maelezo ya Siku hizo za kufunga.
Baada ya maelezo hayo ndipo hutoa maelezo
ya kiliturujia ya siku kwa siku kuanzia Dominika
ya kwanza ya Majilio mpaka Jumamosi
ya Juma la Mwisho katika Dominika
za Mwaka. Kila siku Mkristo hupata vifupisho vya Masomo ya siku hiyo. Anachotakiwa
ni kuwa na Biblia na kutoka Kalenda ya Liturujia atasoma Masomo ya kila siku. Isitoshe,
Mkristo hufahamishwa kuhusu rangi ya
mavazi ya Misa ya siku, iwapo siku hiyo huadhimishwa Misa ya Dominika
iliyopita, au Kumbukumbu, au Sikukuu.
Muhimu kwa
kila Mkristo
Licha ya kuwajuza mambo muhimu katika
ujumla wake, Kalenda ya Liturujia inaongeza taarifa muhimu sana kwa ajili ya
Kanisa Katoliki la Tanzania
katika kila Jimbo. Hapana shaka taarifa hizo ni muhimu kwa kila Mkristo.
Kumbukumbu muhimu ya kwanza ni tarehe
ya kutabaruku
Kanisa kuu la Jimbo. Tarehe ya kutabaruku Kanisa kuu ni muhimu kwa kila
Mkristo jimboni kukumbuka kwani Kanisa kuu la Jimbo ni ishara ya umoja wa Jimbo, ni kanisa la Askofu na ndipo aishipo. Siku hiyo,
katika Kanisa kuu inaadhimishwa Misa kuu ya Kutabaruku Kanisa, Misa ambayo ina hadhi ya Sherehe. Kwa ngazi ya Sikukuu, kila
parokia jimboni huadhimisha Misa ya kutabaruku Kanisa, wakimwombea Askofu,
Mapadri na wasaidizi wengine wa Askofu. Wakristo wakiifahamu tarehe hiyo
wataweza kujiandaa kushiriki Misa hiyo kwa ajili ya kuwaombea wachungaji wao
ngazi ya Jimbo. Wakristo wajue kwamba siku hiyo ni sikukuu ya Jimbo lao.
Tarehe muhimu ya pili ni ile ya kuwekwa
wakfu Askofu – jimbo na
Askofu msaidizi. Kila Askosfu huikumbuka tarehe ya kuwekwa kwake wakfu
akimshukuru Mungu. Hapana budi Wakristo jimboni kuifahamu tarehe hiyo ili
waweze kuadhimisha Ekaristi kwa nia ya kumwombea Askofu wao. Wale wanaoweza
kufika Uaskofuni huweza kuungana na Askofu wao katika Adhimisho hilo la
kumshukuru Mungu likiongozwa na Askofu mwenyewe. Hata hivi Mkristo popote anapokuwa, akiwa na
Kalenda yake ya Liturujia, ataweza kumwombea Askofu katika siku hiyo. Pamoja na
kumwombea, ataweza pia kumtumia kadi ya pongezi.
Pengine tarehe ya kuwekwa wakfu Askofu
hutofautianana na tarehe ya kusimikwa na kukabidhiwa Jimbo. Tarehe ya kusimikwa
Askofu ni muhimu pia; huandikwa katika
Kalenda ya Liturujia. Hapana shaka Wakristo watapenda kumshukuru Mungu kwa
kumpata mchungaji wanapokumbuka siku aliposimikwa na kukabidhiwa Jimbo.
Tarehe nyingine ambayo ni muhimu kwa Wakristo
kuikumbuka ni tarehe ya kufariki Askofu
katika jimbo. Hapana budi waamini kukumbuka tarehe aliyofariki mchungaji
wao ili waweze kumwombea kwa Misa siku hiyo. Kila parokia wanatakiwa
kuadhimisha Ekaristi kwa ajili kumwombea Askofu wao hasa tarehe ile aliyofariki.
Hatima
Kila Mkristo mwenye Kalenda ya
Liturujia akifuatia kalenda yake siku kwa siku atafahamu tarehe hizo muhimu na
kujiweka tayari kushiriki Misa siku hizo muhimu. Wakristo wasisubiri kutangaziwa
kila kitu na uongozi wa parokia, lakini wakiwa na Kalenda ya Liturujia, na
kuitumia siku kwa siku wataweza kujiandaa kushiriki Misa vizuri.
Mahali pengine Mkristo aliweza
kumkumbusha padri kuhusu tarehe muhimu alipoangalia Kalenda yake. Tunawahimiza
Wakristo kujinunulia Kalenda ya Liturujia. Tena ni muhimu sana kila
jumuiya, na uongozi wa Vikundi mbalimbali vya kitume kuwa na Kalenda ya
Liturujia . Piga simu kwa mwandishi wa makala hayo.
Comments
Post a Comment