Ask. Ngalalekumtwa aongoza maelfu ya waamini kumzika Padri Mahimbi Iringa
Askofu wa Jimbo
Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalaekumtwa mwanzoni mwa juma ameongoza
maelfu ya waombolezaji kumzika Padri Vedasto Mahimbi ambaye alifariki kwa ajali
ya gari Januari 31 mwaka huu katika eneo la Lwangwa karibu na Parokia ya Kifanya
Jimbo Katoliki Njombe.
Misa hiyo Takatifu imefanyika katika
Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Tosamaganga ikiongozwa na Askofu wa
Jimbo Katoliki Njombe Mhashamu Alfred Maluma huku homilia ikitolewa na Mhashamu
Ngalalekumtwa ambaye amewata waombolezaji hao wakumbuke kwamba maandiko
Matakatifu yanaagiza na kuonya wanadamu wasilale kwenye usingizi wa dhambi.
“Siri ya Mungu ni agizo tukae katika
mazingira ya kukesha. Kila mmoja wetu lazima atambue hilo na kukaa tayari.
Tunapaswa kuwa na
hekima yenye utambuzi na uadilifu, hekima ambayo huratibu mwenendo na mahusiano
yetu yawe ya haki na upendo,”ameasa Askofu Ngalalekumtwa.
Mwenyekiti wa Umoja
wa Madri Jimboni humo , Padri Leonard Maliva amemuelezea marehemu Padri Vedasto
kuwa ni mtu mchangamfu na hata tabasamu lake lilionyesha kwamba alikuwa ni mtu
wa watu na aliupenda upadri wake.
“Daima tutamkumbuka Padri Vedasto,
alikuwa na karama ya pekee hata waliosoma naye, waliohudumiwa naye kamwe
hawataweza kumsahau kwa upendo wake kwa watu wote.
Padri Maliva ambaye pia ni paroko wa
Parokia ya Isimani amewataka wombolezaji hao kumuenzi Padri Vedasto kwa kutenda
mema na kuyafuata yale mema yote ambayo yeye (Padri Veda) alikuwa akiyatenda.
Akisoma wasifu wa Marehemu Padri
Mahimbi, Paroko wa Parokia ya Mbarali Padri Romanus Mihali, Padri Mahimbi alizaliwa
tarehe 24.10.1971 Kihesa Iringa kwa Wazazi Evaristo na Mama Ferdinanda
Sekibabage, alibatizwa 27.11.1977 katika Parokia ya Itengule na Padri Benedict
Nganung’a.
Alipata Sakramenti Takatifu ya Komunio
ya Kwanza na Kipaimara 21.09.1980 na Mhashamu Baba askofu Mario A. Mgulunde.
ELIMU.
Padri Mahimbi alipata
elimu ya Msingi katika shule Kichangani- Kihesa Iringa mwaka 1980 hadi 1986.
Mwaka 1987 alijiunga na masomo katika Seminari ndogo ya maandalizi Tosamaganga.
Mwaka 1988 hadi 1991
alipata elimu ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne katika Seminari Ndogo
ya Mafinga.
Mwaka 1992 hadi 1994
alisoma kidato cha tano hadi sita katika shule ya wavulana Songea. Na mwaka
1994 hadi 1995 alifanya mwaka mmoja wa kichungaji katika parokia ya Kihesa.
Mwaka 1995 – 1997
alipata elimu ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Peramiho. Mwaka 1997 hadi 2000 alipata elimu ya Teolojia
katika Seminari Kuu ya Peramiho. Mwaka 2010 alitunukiwa Shahada ya Uzamili ya
Falsafa Chuo Kikuu cha Urbaniana Roma Italia.
Mwaka 2012
alitunukiwa shahada ya Uzamivu ya Falsafa katika Chuo Kikuu cha Urbaniana Roma Italia.
DARAJA
Daraja Takatifu la
Ushemasi alipata 28.12.2001 na Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa katika
Kanisa Kuu la Kiaskofu Kihesa Iringa na Daraja Takatifu la Upadri 03.07. 2002 na Mhashamu Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Kihesa Iringa.
UTUME.
Septemba 2002- 2004
Paroko Msaidizi katika Parokia ya Mgololo. Julai 2004 – Julai 2007 Jalimu na
Mlezi katika Seminari Kuu ya Peramiho. Mwaka 2012 -2018 alirudi tena Seminari
Kuu ya Peramiho kuwa Jalimu na Mlezi.
KIFO.
Padre Vedasto Mahimbi
amefariki Januari 31, 2018 kwa ajali ya gari katika eneo la Lwangwa karibu na
parokia ya Kifanya Jimbo Katoliki Njombe.
Raha ya Milele Umpe
Ee Bwana na Mwanga wa Milele umwangazie, apumzike kwa amani, amina.
Na Getrude Madembwe, Iringa.
rip
ReplyDelete