Oktoba 7 kilele jubilei miaka 150 ya uinjilishaji
n Na Pascal Mwanache, Dar
HATIMAYE
ratiba ya kilele cha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara
imetolewa, huku siku ya kilele ikitajwa kuwa ni Oktoba 7, 2018 na maadhimisho
hayo yanatarajiwa kufanyika Bagamoyo.
Akitoa ratiba hiyo kama ilivyopendekezwa na Maaskofu, Katibu
Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padri Raymond Saba amesema kuwa
katika Mkutano wa Maaskofu wamepitisha siku ya Oktoba 7 kuwa kilele cha jubilei
hiyo.
“Kwa hiyo tunategemea watu kutoka majimbo mbalimbali
wawasili Bagamoyo Oktoba 5, huku Oktoba 6 ikiwa ni siku maalum kwa ajili ya
semina, maungamo na kuabudu Ekaristi. Kilele kitakuwa Oktoba 7 na Oktoba 8 watu
wataanza kurejea nyumbani kwao” ameeleza Padri Saba wakati akiwasilisha ratiba
hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Jubilei hiyo.
Aidha Padri Saba amesema kuwa Maaskofu wameichagua na
kuipitisha Dominika ya nne ya Kwaresima kuwa ni siku maalum ya uchangiaji wa
maandalizi ya jubilei hiyo, ambapo sadaka itakayotolewa katika makanisa yote
nchini itakuwa ni mchango kwa ajili ya maandalizi ya jubilei hiyo.
Kamati ya Maandalizi ya Jubilei hiyo imeanza kukutana na
kupeana majukumu mbalimbali yenye lengo la kufanikisha jubilei hiyo.
Comments
Post a Comment