Gumzo kuhusu Kanisa kumzika Hayati Kingunge latolewa ufafanuzi
n Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam
Baada
ya Taifa la Tanzania kumpoteza mwanasiasa mkongwe Mzee Kingunge Ngombale Mwiru
Febriari 2 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar
es Salaam kumekuwepo na gumzo la jamii kulishutumu Kanisa Katoliki kumzika kwa
madai kuwa Hayati Kingunge aliikana imani Katoliki katika enzi za uhai
wake.
Akizungumza na Gazeti kiongozi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu
Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Euzebius Nzigilwa amesema kuwa, Kanisa lipo
wazi kutoa huduma zote za kiroho kwa mtu yeyote aliye tayari kushika mafundisho
ya imani Katoliki.
“Ni kweli Mzee Kingunge enzi za uhai wake kuna masuala
mbalimbali ambayo yalimsababisha aasi imani Katoliki lakini wakati akiwa
mgonjwa alijirudi na kuonesha nia na utayari wa kumrudia Mungu wake.
Mda wa kumrudia Mungu wakati mwingine hautabiriki na yeye
alikuwa na viashiria vya imani na kwamba alitaka kurudi kwenye imani Katoliki.
Viashiria hivyo ni kutubu na kuomba Sakramenti ya Upako wa
wagonjwa na Kanisa lipo kwa ajili ya mtu anayetubu.
Kanisa halihukumu ila Kanisa lipo kwa ajili ya
kumpatia mwanadamu huduma za kiroho katika safari yake ya kwenda Mbinguni.
Mzee Kingunge mwishoni kabisa mwa maisha yake ameonesha nia
yake na heshima kwa Kanisa ingawa kuonesha nia ni kitu kingine na
kutekeleza mashari ni kitu kingine,” ameeleza Askofu Nzigilwa.
Amesema kuwa, Upako wa wagojwa ni Sakramenti inayomsaidia
mwanadamu kuendelea na safari ya maisha na kumpa nguvu. Padri humuombea neema
ya Mungu na kumpaka Mafuta Matakatifu mgonjwa aliye katika hatari ya kifo kwa
ajili ya neema ya roho na mwili. (Yak 5:14-15, Mk 6:13).
Kuhusu kuzikwa, Askofu Nzigilwa amesema kuwa, kwa upande wa
Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam si kawaida Katekista kuendesha ibada ya
mazishi kutokana na mazingira na uwepo wa mapadri ingawa kwa mazingira ya watu
wanaoishi vijijini ni kawaida.
“Mtu aliyeasi imani akionesha nia ya kurudi Kanisa
linafungua milango na kumpokea ingawa lazima apewe masharti kwa kuzingatia
kanuni na taratibu za Kanisa Katoliki.
Mzee Kingunge alionesha nia lakini kuna baadhi ya vipengele
alikuwa hajakamilisha akafariki. Ndiyo maana nimeeleza kuwa, kuwa na nia ni
kitu kingine na kutimiza masharti kulingana na taratibu za Kanisa ni kitu
kingine.
Kwasababu hakupata nafasi ya kutekeleza kanuni na taratibu
mbalimbali kwa kufariki, basi ilibidi azikwe na Katekista kuonesha kuwa bado
ana pungufu flani hivyo hapati ile huduma kamili ya Kanisa anapata huduma ndogo
(minimum service) .
Angekuwa ametimiza kila kitu angezikwa kwa Ibada ya Misa
Takatifu na maadhimisho yote anayopaswa kupatiwa Mkristo kamili wa Kanisa
Katoliki,” ameeleza Askofu Nzigilwa.
Amewaasa waamini wote wa Kanisa Katoliki kujitahidi kishika
imani kwa nia na matendo kulingana na taratibu za Kanisa.
Kifo cha hayati Mzee Kingunge kitupe fundisho la kuwa tayari
kwa ujio wa Bwana.
Mzee angefariki ghafla na kukosa nafasi ya kuonesha nia
asingepata hata hiyo huduma ndogo ya Kanisa (minimum service) ingekuwa kitu
kingine kabisa,” amesisitiza Askofu Nzigilwa.
Akizungumza na Gazeti Kiongozi Monsinyori Deogratius mbiku
ambaye ni ndugu yake Hayati Kingunge na ndiye aliyempatia huduma ya kiroho kwa
mara ya mwisho na kuzungumza naye ameliambia gazeti hili kuwa, Hayati Kingunge
alikuwa anasumbuliwa na falsafa ya wakomunisti.
Mahojiano kati ya Gazeti Kiongozi na Monsinyori mbiku
Je, Hayati Kingunge alikuwa Mkristo?
Monsinyori Mbiku: Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa mkristo
Mkatoliki aliyebatizwa akapata Sakramenti ya komunio ya Kwanza na Kipaimara ,
akasoma kwenye shule ya misheni pale Msimbazi alikaa bweni na
baadaye shule ya middle school Ilala lakini alikuwa anarudi kukaa pale
msimbazi.Alikuwa pia mtumishi wa Misa.
Inasemekana alishawahi kutengwa na Kanisa akiwa mdogo.
Sababu zake ni zipi?
Tangu utoto wake mzee Kingunge alikuwa na akili nyingi na
akili hizo zilimsababisha kuhoji masuala mbalimbali ya imani.Alikuwa anauliza,
Dini ni nini? Mungu yupo wapi? Alisoma mafundisho ya Katekisimu lakini alikuwa
mdadisi sana na kile alichokuwa anakiamini.
Yeye mwenyewe Kingunge alisimulia kuwa, wakati fulani Padri
mmoja Mkapuchini kwa jina Clementi M. alimuona anadadisi mno masuala ya Imani
na kumtilia shaka. Ndipo akamtenga na Kanisa akiwa darasa la sita.
Huyo Padri alimuuliza wewe ni mkomunisti? (asiyeamini Mungu)
na kama ni umkomunisti ninakutenga na Kanisa.
Je, kama hakuamini Mungu alifungaje ndoa Takatifu?
Mons. Mbiku: Alipopata mchumba ambaye ni mkatoliki na
kutaka kufunga ndoa ya kikatoliki, Kingunge alikataa akaamuru kufunga ndoa
bomani.
Kweli wakafunga ndoa ya bomani lakini mke wake akaenda kwa
Kardinali Lauriani Rugambwa wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam akamueleza kuwa
mume wake (kwa ndoa ya bomani) amekataa kufunga ndoa ya Kikristo kwenye Kanisa
Katoliki naye anaogopa kutengwa na Kanisa.
Kard. Rugambwa akamuambia amuite wazungumze. Kingunge
alipofika Kardinali akamuuliza wewe si mkrito? Ukifunga ndoa bomani tu huyu
mkeo tunamtenga na Kanisa lakini Kingunge akabaki na msimamo wake akisema mimi
siamini Mungu kwanini nifunge ndoa Kanisani?
Kard.Rugambwa akamwambia kama unampenda mkeo fanya
lolote litakalowezekana kumsababisha mkeo arudishwe kwenye imani kwa Sakramenti
ya Ndoa Takatifu lakini itakuwa ndoa ya mseto.
Kingunge akakataa akasema hawezi kushuhudiwa na umati wa
watu akifunga ndoa Kanisani.
Kard. Rugambwa akamueleza kuwa, tutaenda mahali ambapo
hakuna watu wengi. Utakuwa wewe na mkeo na wasimamizi wawili, msimamizi
wako mmoja na wa mkeo mmoja hivyo watu wanne na mimi wa tano. Tutafanya misa ya
private. Ilimradi muweke maagano mbele ya Mungu.
Hiyo Misa itasababisha mke wako aitwe mkatoliki kamili
na hatatengwa. Kingunge akakubali wakaenda Kurasini kwa Benediktini procuria
wakafunga ndoa. Baada tu ya Misa hiyo Kingunge akamshukuru Kardinali
akaenda kazini kwake na mkewe nyumbani.
Jioni wakakutana kusherehekea kidogo. Kuanzia hapo mkewe
akawa Mkatoliki kabisa na yeye akaendelea na maisha yake.
Tangu enzi hizo mkewe alikuwa akimuombea mumewe abadilike
kwakuwa familia yake ilikuwa ya kikatoliki ingawa Kingunge pia hakuwahi
kuwazuiya wala kulidhihaki Kanisa Katoliki. Alikuwa nasumbuliwa na Falsafa ya
‘kwemi Mungu yupo?’
Ameshiriki maendeleo ya Kanisa?
Monsinyori Mbiku: Ndiyo wala alikuwa hana tatizo na Kanisa.
Kule Goba kwenye kigango cha Bikira Maria Mama wa Huruma tanki bovu kuna
shamba la Kingunge ambalo alilitoa kama zawadi lijengwe Kanisa. Na ninakumbuka
alisema, “Mtakapomaliza kujenga Kanisa nitakuwa mkristo wa kwanza kuingia
katika hilo Kanisa.’ Baadaye walipoanza harakati za ujenzi eneo lilionekana
dogo wakataka kuongeza nafasi wakanitumia mimi, nikamwombe awaongezee.
Akakubali kuwapatia hekari mbili kwa kuwauzia kwa bei ya chini sana
akishirikiana na mtoto wake mmoja aitwaye Kinje.
Kama alikuwa hamwamini Mungu kwanini ulimpatia Sakramenti ya
Upako wa wagonjwa?
Baada ya kumzika mke wake alizidiwa na kurudishwa hospitali.
Alipokuwa hospitali alizidiwa akazimia. Ndipo wakaniita nikaenda kumwona na
kweli akawa anapumulia mashine na hawezi kuzungumza.
Nikasema mimi nitampatia Sakramenti ya upako wa wagonjwa
kwasababu yeye ni Mkristo maana miaka kadhaa iliyopita nilizungumza naye
nikamuuliza wewe si mkristo? Akasema, ‘Mimi ni mkristo lakini bado ninajiuliza
kama kuna Mungu kweli. Hilo tu ndilo nagombana nalo maana falsafa yangu inataka
kuhakikisha kama kweli kuna Mungu.’
Katika mazungumzo hayo nilimuliza huwezi kurudia ukristo
wako akasema ninaweza lakini siyo sasa. Nilipoona amezimia nikakumbuka maneno
yake, ‘nitaamini lakini siyo sasa.’ Ndipo nikampatia Upako wa wagonjwa
nikiamini ndiyo muda wake sasa.
Nilipomaliza nikawambia wauguzi kuwa naondoka lakini
akizinduka naomba mniite. alipozinduka akawa yupo kawaida wauguzi wakamueleza
nilichofanya.
Akauliza niko wapi akaamuru niitwe. Wakaja kwangu kunichukua
saa tano asubuhi.
Nikamwambia una lolote tuzungumze? Akawasihi wahudumu wote
watoke abaki na mimi na nesi mmoja maana naumwa hivyo lazima awepo mmoja kwa
dharura.
Nikamueleza nilichokifanya, akaniambia, ‘Monsinyori umefanya
vizuri sana na ninakushukuru kwa ulichofanya. Asante sana. Nikamwambia sasa
tumalize kabisa urudi kwenye imani.
Akasema Monsinyori ngoja nikueleze kilichonifanya hivi. Mimi
nilikwenda Urusi, kule nilikaa miaka mingi nikisoma nikakutana na wakomunisti
nikajifunza falsafa kuhusu Mungu yupo au hayupo.
Wakomunist wakasema hakuna Mungu. Mimi niliwakatalia
nikawaambia nihakikishieni kuwa Mungu hayupo. Wakashindwa kunihakikishia. Nao
wakanilazimisha kuwahakikishia kuwa Mungu yupo? Nami nikashindwa
kuwahakikishia.
Ndiyo falsafa yangu na nikarudi katika hilo hadi sasa. Wala
sisemi kuwa hakuna Mungu lakini falsafa yangu haijanipa jibu kwamba kuna Mungu.
Ndiyo hiyo nahangaika nayo.
Kama kuna yeyote anaweza kunihakikishia (kuprove) anisaidie
kwaba kuna Mungu niko tayari hadi sasa kuwa Mkatoliki.
Katika falsafa yangu hiyo, ndipo nikakutana na
maandishi ya Mtakatifu Anselmo, alitamka ‘Naelewa akilini mwangu ili niamini,’
nami (Monsinyori) nikamwambia amini ili uelewe. Nikamwambia sasa kama una Imani
jaribu kuelewa uamini. Akasema hapana huko siko.
Tena nilipata sakramenti zote za Kanisa kasoro upadri. Kama
unaweza kunihakikishia niambie ili akili ijue. Akili haijui ndiyo maana
nahangaika.
Kwabahati mbaya katika mazungumzo akaanza kuchoka Muuguzi
akasema huyu amechoka.
Monsinyori kwa sasa tumuchane . Lakini yeye Kingunge akasema
amefurahia upako wa wagonjwa yuko radhi kurudi kwenye Imani Katoliki ananiomba
nije tena nimuelezee nielewe. Sina shaka na imani Katoliki. Falsafa tu
inanisumbua.
Maneno yake ya mwisho kwangu alisema, Monsinyori mimi
nakushukuru ulimzika mama yangu mzazi 1973 mwaka mmoja wa padri wako pale
Msimbazi, tena umezika mke wangu . “Nilitamani kumwambia nitakuzika nawewe.”
Nikaondoka.
Baada ya siku tatu akazimia tena. Nikawaambia waniite
akizinduka lakini wauguzi wakasema amezidiwa sana na baadaye wakanitaarifu kuwa
amefariki. Hapo ndo ikawa kazi na changamoto.
Nikamuambia Askofu wangu Euzebius Nzigilwa kuwa mazungumzo
yetu na Kingunge na kwamba alipata baadhi ya sakramenti.
Askofu Nzigilwa akasema nisubiri azungumze na maaskofu wengine.
Ndipo baadaye ikaamuliwa kuwa kwa heshima ya mkewe na watoto
wake waliokuwa wanamuombea abadilike, kwa heshima aliyokuwa anaonesha kwa
Kanisa maana hakuwa mpinzani wa Imani tusimtupe tu maana hakuwa mpinzani.
Pia hatuwezi kumpeleka Kanisani kwa Misa ya mazishi maana
alikuwa haendi Kanisani na hatuwezi kumtupa kama mpagani kabisa.
Tutamtuma Katekista afanye ibada kwenye maziko. Nikamchukua
Katekista wangu nikamueleza, aende nyumbani na baadaye makaburini akafanye
ibada.
Kama ndugu yake wa nini hukushiriki kama mtu wa kawaida?
Nilijihadhari kwa maswali mengi. na hata nilipewa
ushauri na askofu maana nikienda kama padri kwenye ibada wangeweza kuzusha
mengi.
Na Sarah Pelaji
Comments
Post a Comment