KUSITISHWA AJIRA SERIKALINI:RAIS AFAFANUA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema
serikali imeamua kusimamisha kwa muda mfupi usiozidi miezi miwili zoezi
la utoaji ajira mpya na upandishaji wa vyeo kwa watumishi wa umma kwa
lengo la kupisha uhakiki wa watumishi wa umma katika orodha ya malipo ya
mshahara na kuondoa watumishi hewa.
Rais
Magufuli amesema hayo leo tarehe 22 Juni, 2016 katika Jubilei ya miaka
50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) iliyofanyika katika ukumbi wa Benki
hiyo, Mtaa wa Mirambo Jijini Dar es salaam.
Dkt.
Magufuli amesema zoezi hilo halina nia ya kuwakatisha tamaa watumishi
wa umma na amewahakikishia watumishi wote wa umma kuwa serikali
itaendelea kuajiri watumishi wapya na kuwapandisha vyeo waliopo kama
kawaida mara baada ya kukamilika kwa zoezi.
"Serikali
ninayoiongoza haina nia ya kuwakatisha tamaa wafanyakazi, lengo lake ni
kujipanga kwa makosa tuliyoyafanya, na ndio maana nimesema kwa kipindi
cha mwezi mmoja hivi au hata mwezi mmoja na nusu, haitazidi miezi
miwili, tusiajiri mtumishi yeyote serikalini, lakini pia katika kipindi
cha mwezi mmoja hatutawapandisha vyeo wafanyakazi, ninaomba wafanyakazi
waelewe hili, kwa sababu tukiendelea tutakuwa tunawapandisha vyeo hata
wafanyakazi ambao hawapo, tunafanya ukaguzi wote tukishamaliza
wafanyakazi wataendelea kupandishwa vyeo" amesema Rais Magufuli.
Wakati
huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Benki Kuu ya
Tanzania kwa kazi kubwa iliyoifanya katika kipindi cha miaka 50 katika
kusimamia sekta ya fedha na maendeleo, lakini ameitaka benki hiyo
kuchukua hatua za haraka dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoyahusu
majukumu yake.
Miongoni
mwa changamoto hizo ni idadi ndogo ya watanzania wanaonufaika na huduma
za benki hususani waishio vijijini, benki kutoza riba kubwa na hivyo
kusababisha wananchi kuogopa kukopa kwa hofu ya kushindwa kulipa,
kuilinda thamani ya Shilingi ya Tanzania, na kukusanya kodi ipasavyo kwa
miamala inayofanywa kupitia simu za mkononi kwa kushirikiana na Mamlaka
ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Changamoto
nyingine ni kusimamia ipasavyo maduka ya kubadilishia fedha (Bureau de
change) ili kuthibiti utakatishaji na utoroshaji wa fedha na
kuhakikisha ushukaji wa mfumuko wa bei uliotoka asilimia 28 hadi kufikia
asilimia 5.1 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita unaonesha matokeo
katika nafuu ya maisha ya watanzania.
Aidha,
Rais Magufuli ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuchukua hatua mara moja
dhidi ya benki ambazo hazizalishi faida zikiwemo benki za serikali,
kufuta account mfu (Domant account) na kuanzisha mara moja akaunti moja
ya mapato na matumizi ya serikali (Single Treasury Account)
Jubilei
hiyo imehudhuriwa na Magavana na Manaibu Gavana kutoka nchi 18 za
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa
Afrika (SADC), Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa Taasisi za
fedha za Afrika na Makatibu wakuu wa Wizara za Fedha na Mipango wa
Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
22 Juni, 2016
Comments
Post a Comment