Miaka 65 ya Upadre imesimikwa katika huduma ya imani na mapendo!


Mama Kanisa anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi na wito wa Daraja Takatifu la Upadre alilomkirimia Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, miaka 65 iliyopita. Huu ni wito kama ule ambao Yesu alimwangalia Simoni kwa jicho la upendo na kumuuliza ikiwa kama alikuwa anampenda zaidi kuliko wengine wote, kiasi cha kumkabidhi dhamana ya kuchunga na kulinda kundi la Kristo.
Wito huu ndio umekuwa ni kielelezo cha huduma ya Kipadre na taalimungu ya kweli ya kumtafuta Kristo, ushuhuda ambao umeoneshwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto katika maisha na utume wake, ili aweze kufahamika na kupendwa zaidi, upendo ambao unaijaza nyoyo ya waamini amani na utulivu hata wakati wa shida na magumu ya maisha, kama hata ilivyotokea katika maisha ya Mtakatifu Petro. Changamoto ni kuangalia mbele kwa matumaini na furaha pasi na kujutia yale yaliyopita.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 65 tangu Papa mstaafu Benedikto XVI alipopewa Daraja Takatifu la Upadre. Katika maisha na utume wake, ameonesha na kushuhudia upendo huo wa dhati ambao ameuelekeza kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anamshukuru Papa Mstaafu kwa kuendelea kulihudumia na kulijenga Kanisa kwa ari na hekima, katika maisha yake kwenye Monasteri ya Mater Ecclesiae iliyoko mjini Vatican, tofauti kabisa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine unaopelekea watu kutelekezwa pembezoni mwa jamii na kusahaulika huko!
Baba Mtakatifu Francisko amemhakikishia Papa mstaafu Benedikto XVI kwamba, ameamua kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi ili kuendeleza hija ya upendo na imani iliyomwezesha kuwa karibu na Bikira Maria, akaonja upendo wa dhati kwa Kristo Yesu. Hii ndiyo hali ambayo Baba Mtakatifu mstaafu anaionja kwa kufika katika eneo hili la Kifranciskani, ili kuonja amani na utulivu wa ndani; Ukomavu, imani, sadaka na uaminifu; mambo yanayomjenga Baba Mtakatifu Francisko na Kanisa katika ujumla wake. Amemtakia heri na baraka ili aweze kuhisi uwepo mkono wa huruma ya Mungu unaomsindikiza, ili kushuhudia upendo na furaha wakati akielekea katika lengo la imani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI