TAARIFA KWA UMMA:TAMKO LA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI JUU YA KONGAMANO LA EKARISTI TAKATIFU JIMBO KUU MWANZA JUNE 9-11-2016
TAMKO RASMI LA KONGAMANO LA EKARISTI TAKATIFU JIMBO KUU MWANZA 2016
Sisi Maaskofu, Mapadre,
Watawa na Waamini wote Kutoka majimbo Katoliki Tanzania, tuliokutana katika
viwanja vya Bikira Maria Malkia wa
Kawekamo kwa madhumuni ya kuadhimisha Kongamano la tatu (3) la Ekaristi Takatifu
Kitaifa (Juni 8 mpaka 11 mwaka 2016). Kwa
taswira nzuri mithili ya ile ya
kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu
Kristo pale mlimani Tabor, na mithili ya
wanafunzi wa Emaus waliomtambua Yesu katika kuumega mkate, tunapenda kuinua
shukrani yetu kwa Mungu anayetupatia mwanae kuwa chakula cha safari yetu
kuuelekea ufalme aliotuhaidia.
Baada ya kusali na
kutafakari kwa kina juu ya neema na Baraka
ziletwazo na Ekaristi Takatifu, tunauhakika kwamba Roho Mtakatifu
anatutuma sasa, kwenda kumtangaza na kumshuhudia Yesu wa Ekaristi Takatifu. Tukiongozwa
na kauli mbiu “Kristo ndani Yenu Tumaini Letu la Utukufu, tumeitafakari
Ekaristi kwanza kama;
Mkate wa Uumbaji: Ekaristi Takatifu, ikiwa inaishi na kuleta uhai
hukutana nasi tunaoipokea, na yenyewe inakuwa ukamilifu kabisa wa fumbo la
Pasaka ambalo ni msingi wa kweli na ni kichocheo cha Uongofu binafsi. Hili
fumbo linatuimarisha sisi katika imani. Ni katika ekaristi kila kiumbe kinapata
uhai, furaha ya kweli, na Ekaristi Takatifu inatuhimiza kuutunza uumbaji kama
shukrani yetu kwa Mungu aliyeumba mbingu na dunia na vitu vyote vinavyoonekana
na visivyoonekana.
Mkate kwa Utukufu: Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wetu sisi waamini
wakatoliki kuhusu, mateso,kifo na ufufuko wa Bwana wetu ambaye ametuachia
ukumbusho wa mateso yake na fursa ya kumpokea yeye katika fumbo la Ekaristi.
Ekaristi Takatifu ni
chanzo cha wito na matumaini yetu ya utukufu,pia ni mkate wetu wa matumaini kwa
vile hutupatia nguvu ya kuishi kwa kutoa shukrani na furaha ijapokuwa maisha
yetu hukabiliwa na changamoto nyingi.Pamoja na changamoto hizo, katika Sakramenti
ya Ekaristi Takatifu, Mungu anakuwa
pamoja nasi,anatuokoa, anatutawala na kututakatifuza.
Ekaristi Takatifu kwa
hiyo itujengee ari ya kutulia na kutafakari safari ya maisha yetu na humo
tuchote nguvu za kuendelea mbele kwa uthabiti wa maisha.
Mkate wa mazungumzano: Ekaristi
Takatifu ni kiunganishi kati ya Mungu
na uumbaji,:Mungu na watu, :watu kwa watu. Kwa muktadha huo Ekaristi Takatifu inatupa nguvu ya mazungumzano ndani yetu,katika
familia,jumuia ndogondogo na inatusukuma
kuwa wahudumu wa Ekaristi katika kanisa, tukijenga misingi ya ekumenia,
tukijenga misingi ya mahusiano na dini mbalimbali tamaduni mbalimbali na
ulimwengu mzima. Ekaristi Takatifu siku zote itusaidie tusiishi kinadharia bali tuishi matendo ya injili kila siku kama kanisa la mwanzao “…na
siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa
nyumba na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe Mdo. 2:46”
Mkate kwa misioni: Baada ya kuvuviwa na
kuhuhishwa na Ekaristi Takatifu katika viwanja vya Bikira Maria Malkia wa
Kawekamo tunaalikwa kuwa wamisionari
wakristo wanaotumwa katika majimbo yetu na Tanzania kwa ujumla kuwa Mkate unaomegwa kwa ajili ya
kuiletea uhai Dunia inayomeguka. Katika umisioni huo sisi sote tuliokuwepo hapa
tunalo jukumu la kimisionari; ni dhahiri kwamba kongamano la Ekaristi Takatifu la kitaifa la mwaka 2016 ni wito wa
kimisionari kwetu sote kwa sababu kama tulivyotafakarishwa Ekaristi yetu ni
chemichemi ya msamaha kitubio. Kama tulivyotafakarishwa Ekaristi ni msingi wa
kujenga familia; ni msingi wa namna ya kumpokea Bikira Maria kama mama wa
Ekaristi na kutufundisha. Hivyo Ekaristi yetu ni chemchemi na lengo la umisionari wa kanisa.
Umisionari kwa nafsi
zetu, kwa familia zetu, kwa wasiomjua Kristo bado, kwa wanaoteswa na kuteseka,
kwa wanyonge, na kwa wasio na matumaini; umisionari wa kujitakatifuza katika
Sakramenti ya Upatanisho, na umisionari kupitia vyama vyetu vya kitume.
Mwisho kwa Mama
Mbarikiwa, Mama wa Ekaristi, tunalikabidhi kanisa zima nchini Tanzania,
tunaweka chini ya ulinzi wake.
Ee Mama mwenye kulilinda
kila jimbo, kila parokia na kila familia , tufundishe kuipokea, kuiishi,
kuitetea na kuishuhudia Ekaristi Takatifu kila tutakapokuwa. Tunamuomba Mama
yetu Malkia wa Kawekamo, alilinde jiji la Mwanza na watu wake, na alilinde
Taifa zima la Tanzania ili amani, haki, upendo, heshima kwa hadhi na utu vidumu
na kutawalahapa na nchini kote.
KRISTO NDANI YENU,TUMAINI LETU
LA UTUKUFU
Comments
Post a Comment