"MSITAFUTE FAMILIA ZA KUCHONGWA"PAPA


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuzindua kongamano la Jimbo kuu la Roma Alhamisi usiku tarehe 16 Juni 2016 linaloongozwa na kauli mbiu “Hija ya familia za Roma mintarafu mwanga wa Wosia wa Kitume Furaha ya Upendo ndani ya familia” alipata nafasi ya kujibu maswali matatu ya msingi kutoka kwa washiriki wa kongamano hili. Swali la kwanza lilijikita katika ubinafsi, kinzani, migawanyiko ya kijamii, mambo yanayogumisha upendo na mshikamano wa kidugu miongoni mwa waamini.
Ubinafsi huu ndio unaowafanya hata baadhi ya viongozi wa Kanisa kushindwa kutoa Sakramenti kwa watoto ambao wamezaliwa katika hali tete ya imani na kusahau kwamba, binadamu si mkamilifu, bali yuko katika hija ya kutafuta ukamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Ubinafsi unajikita katika moyo wa binadamu anayedhani kwamba, mali na utajiri vinaweza kumkirimia furaha na uzima wa milele. Upendo kwa Mungu na binadamu umegeuzwa na kuelekezwa kwa wanyama na kwamba, maisha ya binadamu si mali kitu! Watu wanashindwa kuthubutu katika maisha, ili kuwa huru na matokeo yake wanajikita katika ubinafsi, woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto!
Viongozi wa Kanisa wathubutu kujitosa katika maisha na utume wa Kanisa, wanapokosa, waoneshe ujasiri wa kurekebishwa na kuanza tena upya, lengo liwe ni kuboresha maisha ya watu: kiroho na kimwili! Vinginevyo watamezwa na ubinafsi na woga wa kuwa huru katika maamuzi na mipango yao ya shughuli za kichungaji. Waamini wajifunze kuwa na mwono mpana wa kifamilia unaowashirikisha wengine badala ya kuwatenga na kuwabagua! Kanisa ni Mama mwenye huruma na mapendo kwa watoto wake, wema na wadhambi, kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake.
Swali la pili lilijikita katika Sakramenti ya Ndoa inayojikita katika Injili ya familia inayofumbata: udumifu, uaminifu na upendo usiogawanyika. Familia zinapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mababa wa Sinodi walikazia kwa namna ya pekee kabisa mambo makuu manne: kuwapokea, kuwasindikiza, kung’amua na kuwashirikisha waamini katika maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kurejea tena na tena tafakari iliyotolewa na Kardinali Christoph Schornborn, mwana taalilimungu aliyebobea! Ikumbukwe kwamba, Sheria ni kwa ajili ya binadamu na wala si binadamu kwa ajili ya Sheria. Kanisa litaendelea kujikita katika Biblia, Mapokeo pamoja na Mafundisho tanzu ya Kanisa, huku likiendelea kusoma alama za nyakati kwa kujikita katika kanuni maadili, utu wema pamoja na huruma ya Mungu kwa wadhambi wanaomkimbilia wakitaka kutubu na kumwongokea. Ugumu wa mioyo na usalama wa maisha ni kati cha changamoto ambazo waamini wanapaswa kuzifanyia kazi, ili kuonja wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ukweli wa kimaadili unajikita katika upendo kwa Mungu na jirani; upendo unaompatia nafasi mdhambi kuweza kutubu na kumwongokea Mungu.
Swali la tatu lilijikita kwa namna ya pekee kwenye mpasuko wa maisha ya ndoa na familia pamoja na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ni matokeo ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; ubinafsi unaowafanya watu kushindwa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao. Sakramenti ya Ndoa ni chemchemi ya neema inayosimikwa katika umoja, udumifu, uaminifu na mapendo kamili tayari kushiriki katika mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji na malezi kwa watoto.
Gharama za arusi zisiwe ni kikwazo kwa vijana kushindwa kufanya maamuzi magumu katika maisha ya ndoa na familia. Waamini wanapaswa kutambua, kuheshimu na kufumbata uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia unaodumu maisha yote hadi kifo kitakapowatenganisha hawa wapendanao. Maisha ya ndoa yana magumu na changamoto zake, lakini ni fursa ya kuonja na kushiriki wema na upendo wa Mungu kwa kukuza na kudumisha imani. Waamini wawe tayari kukuza na kudumisha uaminifu wao, amani na ujenzi wa majadiliano.
Waamini wajifunze vyema maisha ya ndoa kabla ya kuanza kuishi katika ndoa; wawe tayari kuomwongokea Mungu na kuanza kuandika kurasa za utakatifu wa maisha kwa ukarimu na ukomavu. Kwa njia hii waamini wanaweza kujenga ndoa zinazodumu na wala si ndoa za mpito zinazobabisha mateso na mahangaiko kwa wanandoa wenyewe na familia zao. Baba Mtakatifu anasema, huu ni ushuhuda na mang’amuzi yake ya shughuli za kichungaji ambayo amependa kuwashirikisha washiriki wa kongamano la shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI