TANZIA
Matukio yaliyojiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Mazishi ya Padri Filipo Mrope (94) aliyefariki dunia Juni 19 mwaka huu huko kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara iliyoko Ndanda katika Wilaya ya Masasi Mkoani humo.
UMATI wa waombolezaji wamejitokeza
kumzika Padri Filipo Mrope (94) aliyefariki dunia Juni 19 mwaka huu huko kwenye
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara iliyoko Ndanda katika Wilaya ya Masasi
Mkoani humo.
Akitoa
salamu zake Askofu Askofu Titus Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara amemshukuru Mungu
kwa kuwapatia zawadi ya Padri huyo na kwa namna ya pekee ameshukuru huduma na
utume alioufanya Padri Mrope katika majimbo ya zamani ya Ndanda,Nachingwea na
hatimaye Jimbo la Mtwara.
Amesema
kuwa kabla ya kuaga dunia aliagana na Padri Mrope ambaye amewahimiza wakristo Jimboni humo kuzidi
kumuomba Mungu kusudi aite vijana wengi ambao wataisikia sauti yake kusudi wawe
mapadri na watawa wa kike na kiume ili kukabiliana na changamoto ya ukame wa
miito iliyomo Kanisani hivi sasa.
Aidha
Askofu Mdoe ametumia fursa hiyo kuwataka Mapadri kuchochea miito kupitia maisha
yao na utendaji wa kazi za kueneza Injili; kama Padri Mrope alivyofanya kiasi
cha kuwavuta vijana wengi kujiunga na Seminari kupitia maneno na matendo yake
katika huduma zake za Kipadri.
Adhimisho
hilo la Misa ya Maziko limehudhuriwa pia na Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki
Mtwara Mhashamu Gabriel Mmole, Maabate Wastaafu wa Ndanda Siegifried OSB na
Dionynis OSB, Mapadri toka majimbo ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara,
Tunduru-Masasi,na Zanzibar, Watawa wa kike na kiume pamoja na waombolezaji
wengine toka sehemu mbalimbali nchini.
Kwenye
mahubiri yake, aliyekuwa Naibu wa Askofu Mmole, Padri Galus Chilamula, amesema
kama waombolezaji hususan Watawa wa kike na wa kiume wangepata nafasi ya
kumwelezea Padri Mrope, wangesimulia jinsi walivyonufaika naye kwa huduma zake
mbalimbali kwa njia ya ushauri na mafundisho yake aliyoyatoa wakati wa mafungo
na nyakati zingine enzi za uhai wake.
Kuhusu
mwaka wa Yubilei ya Huruma ya Mungu, Padri Chilamula amewahimiza waamini
kutumia fursa iliyotolewa na Kanisa kwa kujipatanisha na Mungu kwa njia ya
kupokea Sakramenti mbalimbali, hususani ya Upatanisho ,kusudi kuifaidi huruma
na wema wa Mungu ambao hauna mipaka. Kwa namna ya pekee amewakumbusha wote
kuzingatia miito waliyopewa na Mungu na kuitumia kwa manufaa ya Kanisa na hata
jamii inayowazunguka.
Naye Kiongozi (Priori) wa Nyumba ya Watawa wa
Mtakatifu Benedikto Ndanda, Padri Silvanus Kessy, kwa niaba ya Abate Plasido
OSB amewapa pole wote waliopatwa na majonzi kutokana na kifo cha Padri Mrope.
Amesema kuwa licha ya Padri huyo kuwa muungamishi wao,kuna mambo ambayo
wamejifunza katika kipindi chote cha miaka 30 aliyoishi kati ya Wanajumuiya
hao.
Mambo
hayo ni mapenzi yake ya maisha ya sala, kujali muda na kupenda mazoezi ya
mwili, kwani mara nyingi alitembea kwa miguu katika huduma zake za Kichungaji
alizotoa jirani na ilipo Nyumba ya Watawa hao.
Naye
Meneja wa Duka la Vitabu Ndanda ,Padri Sebald OSB alivionesha vitabu mbalimbali
ikiwemo Agano Jipya ambayo ilitafsiriwa kwa
Kiswahili na Padri Mrope,na kwamba alikuwa bingwa wa lugha za Kilatini,
Kiingereza na Kiswahili.
Wengine
waliotoa salamu za rambirambi ni Askofu James Almas wa Dayosisi ya Anglikana
Masasi, Naibu wa Askofu wa Lindi, Padri Angelus Chitanda na Mwakilishi wa
Askofu wa Jimbo la Tunduru Masasi Padri Herman Mchopa.
HISTORIA YA PADRI MROPE
Akiwa
mtoto wa nane kati ya watoto 10 wa Familia ya Mzee Mikael Humkamaru Mrope na Bi
Melania, amezaliwa Kijiji cha Chigugu Masasi Juni 6,1922,na baada ya miaka 12
alibatizwa.
Elimu;
Alianza Elimu ya Msingi Kijijini kwake Chigugu mwaka 1931-1937,na mwaka 1938
hadi 1941 alisoma Shule ya Walimu-TTC huko Ndanda.Katika kipindi hicho Filipo
alisikia wito wa Upadri akapelekwa Seminari ndogo ya Kigonsera Ruvuma pamoja na
wenzake Klement Mapua, Xaver Chinyang’anya,na Paulinus Nnembuka.
Kutokana
na sababu mbalimbali vijana wawili walitoka Seminari,wakabakia Paulinus na
Filipo ambao kwa miaka 1942-1946 waliongezewa madarasa ili waweze kumudu masomo
ya Falsafa na Teolojia.
Baada
ya kumaliza masomo hayo,mwaka 1946/47,mwaka 1948 walijiunga na Seminari Kuu Peramiho kwa ajili
ya masomo ya Teolojia. Iikuwa tarehe 26 Oktoba 1955,ambapo Mhashamu Askofu
Victor Haelg OSB, wa Jimbo la Ndanda wakati huo,aliwapa Daraja takatifu ya
Upadre kwenye Kanisa Kuu la Ndanda.
UCHUNGAJI:Mwaka
1956 Padre Mrope alikuwa Paroko Msaidizi Parokia ya Nkowe na miaka sita
alipelekwa Seminari Ndogo ya Namupa kuwa Mwalimu.Katika kipindi cha mwaka
1963-1964 aliazimwa na Uongozi wa Jimbo la Nachingwea wakati huo akawa Katibu
wa Elimu wa shule za Jimbo hilo,na baada ya mwaka mmoja alirudi Jimboni Ndanda
na kuendelea kuwa Katibu wa Elimu wa Jimbo hilo.
Mwaka
uliofuata alifanywa Paroko wa Parokia ya Malolo na mwaka 1967 akahamia Newala
ambako alikuwa Paroko Msaidizi. Mwaka 1968-1976 alikuwa Paroko kwenye Parokia
za Lukuledi, Nachingwea, Liwale na Migongo Masasi. Katika kipindi hicho Padri
Mrope alichaguliwa kuwa Makmu wa Askofu wa Jimbo la Nachingwea wakati huo
Askofu Arnold Cotey SDS.
1968-1998
Padri Mrope alikuwa Mjumbe wa Liturujia Kitaifa akiungana na mabingwa wengine
wa Kilatini walitafsiri Sala za Misa Takatifu katika lugha ya Kiswahili.
Wajumbe wengine walikuwa Askofu Joseph Sipendi wa Jimbo la Moshi, Padri John
Kabeya wa Jimbo la Tabora na Padri Stephen Mlunde wa Jimbo la Dodoma.
Baada
ya kazi hiyo kukamilika Padri Mrope 1976-1979 alirudi Mtwara na akafanywa
Paroko wa Rondo. Mwaka 1979-1982 Paroko Nanganga. Mwaka 1982-1988 Paroko Namupa
sanjari na kuwa Baba wa Roho katika Seminari ndogo ya Namupa.
Mwaka
1981-1982 Padri Filipo pamoja na Padri Valerian Fataki wa Dar Es Salaam
walifanya tafsiri ya Sala za Misa Takatifu huko Mafinga Iringa.
Mwaka
1988 Padri Mrope alikuwa Baba wa Roho wa Masista Wabenediktini wa Bikira Maria
Msaada wa Wakristo Ndanda hadi alipostaafu kutokana na uzee.
Pamoja
na mambo mengine Padri Mrope atakumbukwa na wengi kutokana na upole wake,
unyenyekevu wake,ucheshi wake na kwamba alikuwa Mwanasanaa aliyebobea. Na
katika matukio mbalimbali aliwavunja watu mbavu kwa vibweka na vichekesho vyake
vilivyotumbuiza watu.
Na Anthony Chilumba,
Ndanda
Comments
Post a Comment