Toba na wongofu wa ndani ni chanda na pete!


Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumamosi, tarehe 18 Juni 2016 ameendelea kutoa katekesi yake kwa kujikita katika huruma na wongofu wa ndani; mambo msingi ambayo Kristo Yesu aliwaachia wafuasi wake kabla ya kupaa kwenda kwa Baba yake wa mbinguni, kuwa ni kiini cha mahubiri na ushuhuda wao kwake. Wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi ni mambo msingi yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu ambaye kutokana na upendo wake mkuu anawahangaikia binadamu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema changamoto ya toba na wongofu wa ndani ni ujumbe uliokuwa unatolewa na Manabii kwenye Agano la Kale, ukiwa ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuacha nyendo zao mbaya na kumrudia Mungu, kwa kuomba msamaha. Wongofu wa ndani ni mchakato wa mageuzi makubwa katika maisha ili kumwendea Mwenyezi Mungu anayewapenda watu wake upeo na kwamba, upendo wake daima unajikita katika uaminifu.
Tubuni na kuiamini Injili ni maneno ambayo Yesu aliyatumia mwanzoni kabisa mwa maisha na utume wake wa hadhara kwa kuwaalika wasikilizaji wake kusikiliza Neno lake ambalo linapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye kwa sasa anazungumza na waja wake kwa njia ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo. Manabii walikazia wongofu, lakini Yesu anataka wongofu wa ndani unaomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili ili hatimaye, aweze kuwa ni kiumbe kipya, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka!
Yesu anapowaalika watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu anafanya hivi kwa kujiweka kuwa jirani na watu kama ilivyokuwa katika Fumbo la Umwilisho, alipojitwalia hali ya ubinadamu ili aweze kukutana na watu katika medani na mazingira mbali mbali ya maisha ya watu. Kwa njia hii, Yesu aliweza kuwafunulia watu huruma ya Mungu kwa njia upendo wenye mvuto na mashiko, ili kuwashirikisha wote katika historia ya ukombozi, kiasi cha kugusa nyoyo za watu na watu wenyewe kujisikia kweli wanavutwa na kupendwa na Mungu hivyo wanapaswa kubadilisha maisha yao.
Baba Mtakatifu amewataja baadhi ya watu waliotubu na kumwongokea Mungu, hawa ni kama Mathayo na Zakayo mtoza ushuru, waliosikia na kuguswa na upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Wongofu wa kweli unajionesha pale mwamini anapokubali kupokea zawadi ya imani inayomwilishwa katika matendo kwa njia ya huduma kwa jirani.
Hii ni changamoto anasema Baba Mtakatifu, kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu na kuendelea kushuhudia neema hii katika maisha, ili kuonja furaha na maisha ya kweli yanayojikita katika upyaisho wa maisha ya kiroho. Kuendelea kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani. Waamini  kwa namna ya pekee wawe ni chachu ya Injili katika ukweli, msamaha, huruma na upatanisho. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kiwe ni kielelezo cha upyaisho wa imani inayojikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI