PAPA FRANCISKO AWAASA WANAHABARI
Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanahabari kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kikamilifu dhamana hii kwani habari njema zinasaidia mchakato wa maendeleo ya watu: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu ameyasema haya, Jumapili tarehe 26 Juni 2016 alipokuwa anarejea kutoka katika hija yake ya kitume nchini Armenia. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu aliweza kujibu maswali kumi kutoka kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa kwenye msafara wake wakati wa hija yake ya kitume nchini Armenia kuanzia tarehe 24- 26 Juni 2016.
Baba Mtakatifu amegusia urithi na ushupavu wa imani kwa familia ya Mungu nchini Armenia na kwamba vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho nchini Armenia. Mauaji ya kimbari ni ukweli wa kihistoria usioweza kufumbiwa macho! Papa mstaafu Benedikto XVI ni mlinzi makini wa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Sinodi ya Kanisa la Kiorthodox imekuwa na mafanikio makubwa ingawa mambo yanaweza kuboreshwa zaidi. Umoja wa Ulaya unapaswa kujikita katika kipaji cha ugunduzi na uzalishaji.
Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni kipindi cha kusali na kujikita katika huduma makini. Ukweli kuhusu Mashemasi wanawake ulipotoshwa kwa makusudi na vyombo vya habari. Kanisa lina mambo mengi ya kuomba msamaha si tu kwa mashoga! Siku ya Vijana Duniani ni muda wa kusali, kusherehekea na kukaa kimya mbele ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia!
Baba Mtakatifu anasema, anaitakia familia ya Mungu nchini Armenia haki na amani kwani imeonesha ujasiri wa pekee unaojikita katika mchakato wa amani, utulivu na msamaha tayari kusonga mbele kwa matumaini licha ya mateso na magumu ambayo wamekabiliana nayo katika historia yao kama taifa. Ni taifa ambalo limeonesha ujasiri na ushupavu, likasimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha Mapokeo, mila na desturi zake njema.
Hii ni nchi ya kwanza ya Kikristo iliyopata baraka na neema za pekee kutoka kwa Kristo Yesu na kwamba, imani yao imewawezesha kuendelea kuwa imara na kushuhudiwa na mashahidi pamoja na watakatifu wengi walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Katika maisha na utume wake amejifunza walau ibada na liturujia yao kama sehemu ya mchakato wa kudumisha majadiliano ya kiekumene.
Baba Mtakatifu anawataka vijana nchini Armenia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mchakato wa upatanisho, haki na amani na wananchi wa Uturuki na Azebaigiani na kwamba, daima ataendelea kukazia umuhimu wa ukweli, haki na amani, ili kuwawezesha wananchi wa maeneo haya kujikita katika mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mauaji ya kimbari si neno ambalo analitumia kwa mara ya kwanza katika hotuba zake, lakini ikumbukwe kwamba, historia ya mwanadamu imekumbwa na mauaji ya kimbari yaliyosababishwa kwanza kabisa nchini Armenia, Adolf Hitler na Stalin na hivi karibuni kumekuwepo pia mauaji ya kimbari nchini Rwanda.
Mauaji ya kimbari ni neno la kiufundi anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko linalodai fidia kutokana makosa yaliyotendwa. Mauaji ya kimbari ni neno ambalo Mtakatifu Yohane Paulo II alilitumia katika hotuba zake na alipokuwa nchini Uturuki alilitumia huku akimnukuru Mtakatifu Yohane Paulo II, jambo ambalo lilizua hasira kali kutoka kwa Serikali ya Uturuki. Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, ametumia neno mauaji ya kimbari ili kukazia ukweli. Kuna wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa waliokuwa na uwezo wa kudhibiti vita kuu za dunia, lakini hawakuwa na ujasiri wa kufanya hivyo! Kuna mauaji ya kimbari pia dhidi ya Wayahudi, yote haya ni matukio yanayofumbata utamaduni wa kifo.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, historia ya Kanisa inaonesha kwamba, kuna wakati walikuwepo Mapapa watatu! Papa mstaafu Benedikto XVI aling’atuka kutoka madarakani kunako tarehe 28 Februari 2013, ili kuendelea kusaidia maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya sala na tafakari zake. Wanawasiliana mara kwa mara na kwamba, ni neema na baraka kuwa na kiongozi kama Papa mstaafu Benedikto XVI ambaye amekuwa ni mlinzi wake wa daima kwa njia ya sala na utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ni kiongozi aliyeonesha ujasiri wa pekee kwa kufungua ukurasa mpya kwa Mapapa kuweza kung’atuka kutoka madarakani na kuendelea kulisaidia Kanisa kwa njia ya sala, tafakari na ushauri wake. Tarehe 28 Juni 2016 Papa mstaafu Benedikto XVI na kaka yake Monsinyo Georg wanaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 65 ya Daraja Takatifu. Hii itakuwa ni siku ya furaha ili kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Papa mstaafu Benedikto XVI, mtu wa sala na tafakari ya kina asiyependa makuu, aliyekirimiwa kipaji cha hekima na akili, Babu katika nyumba ya kipapa!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Kanisa la Kiorthodox yamepata mafanikio makubwa na kwamba, bado kuna nafasi ya kuweza kuboresha changamoto zilizojitokeza. Imekuwa ni fursa ya kuweza kusali, kutafakari na kujadiliana kwa pamoja kama ndugu.
Kuhusu Umoja wa Ulaya unakabiliwa na changamoto nyingi kama ilivyo hata katika baadhi ya nchi zenyewe kama inavyojionesha huko Hispania na Scotland, changamoto ya kujikita katika majadiliano yanayojikita katika ukweli, ustawi na mafao ya wengi ili kupata suluhu ya kudumu. Uingereza imeonesha utashi wa wananchi wanaotaka uhuru zaidi kuhusiana na mambo yao. Umoja wa Ulaya unajenga na kudumisha umoja na udugu, lakini pia utoe nafasi kwa nchi wanachama kujiamria mambo yao wenyewe kadiri ya historia na tamaduni zao. Usaidie kutatua matatizo ya wanachama wake kwa kuwapatia fursa za ajira. Ugunduzi na uzalishaji ni changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi na Umoja wa Ulaya.
Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu Maadhimisho ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri ndani ya Kanisa anafafanua kwamba, Martin Luther alikuwa ni mwana mapinduzi aliyefanya maamuzi kadiri ya historia ya Kanisa kwa wakati wake, pengine njia alizotumia hazikuwa sahihi sana. Kanisa lilikuwa limemezwa mno na malimwengu, rushwa, tamaa ya mali pamoja na madaraka. Katika mwelekeo huu, alikuwa sahihi kabisa. Leo hii Makanisa yanakubaliana kimsingi juu ”Tamko la kuhesabiwa haki ndani ya Kanisa” Hii ilikuwa ni dawa kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.
Martin Luther anapaswa kuangaliwa katika miwani ya historia ya Kanisa kwa wakati wake, leo hii majadiliano ya kiekumene yanaendelea kushika kasi ya ajabu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Bado kuna kashfa ya utengano lakini hii ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika ukweli, heshima na kuthaminiana. Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri ni nafasi muafaka ya kusali pamoja na kujikita katika Uekumene wa damu na ushuhuda wa huduma makini kwa maskini, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji; kwa ajili ya kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.
Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu Mashemasi wanawake ndani ya Kanisa anakiri kwamba, huu ulikuwa ni upotoshaji wa makusudi uliofanywa na baadhi ya vyombo vya habari kwani mazungumzo yake na watawa yalirekodiwa na hatimaye kuchapishwa kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano. Lakini ikumbukwe kwamba, katika historia ya Kanisa kumekuwepo na Mashemasi wanawake. Kumekuwepo wanawake ambao wamejitambulisha ndani ya Kanisa kutonana huduma na ushauri wao makini. Baba Mtakatifu anavitaka vyombo vya mawasiliano ya jamii kusimamia ukweli na wala si kuwalaghai watu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, wanawake wana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa ambaye ni mchumba wa Kristo.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, msimamo wa Kanisa kuhusu mashoga na watu wenye mielekeo kama hii,ni kuwa hawapaswi kutengwa wala kunyanyaswa. Lakini ni jambo lisilokubalika watu hao kutumiwa kwa misingi ya kisiasa. Kanisa lina mambo mengi ya kuomba msamaha hasa kwa maskini wanaoendelea kunyanyasika kutokana na umaskini wao; kwa vita inayoendelea kusababisha maafa kwa watu na mali zao kutokana na biashara haramu ya silaha.
Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la mitume lakini Wakristo ndio wanaoogelea katika dhambi. Kanisa linapaswa kujenga utamaduni wa kusamehe na kufariji. Licha ya dhambi na mapungufu ya watoto wa Kanisa lakini kuna watakatifu wengi kama Mama Theresa wa Calcutta, waamini walei, mfano bora wa kuigwa katika maisha ya ndoa na familia, changamoto na mwaliko kwa waamini kutambua kwamba, wao pia ni wadhambi na wanahitaji kutembea katika mwanga wa utakatifu wa maisha.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani huko Cracovia, Poland sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanaendelea vyema. Itakuwa ni nafasi ya kumbelea kambi mbali mbali za mateso katika hali ya ukimya. Kuna wakati ambapo kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa ukimya. Baba Mtakatifu anasema anataka kwenda kwenye kambi hizi katika hali ya ukimya, akiomba neema ya kulia na kutoa machozi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment