HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU




 Na Philip Komba

Utangulizi:  Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni moja ya ibada zinazojulikana sana katika Kanisa Katoliki. Ibada hii inauona Moyo wa Kibinadamu wa Yesu kama mwakilishi wa Mapendo yake ya Kimungu kwa wanadamu, na Kanisa nayo inaiona kama Mapendo na Huruma ya Yesu kwa wanadamu wote.

Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu imefikia hatua hii tunayoishuhudia leo kutokana na maelekezo ya Mtakatifu Margareta Maria Alakok aliyejifunza uendelezaji wake wakati alipokuwa anatokewa na Yesu kwa mfululizo kati ya mwaka 1673 na mwaka 1675.

Mtawa mwingine tena, Mwenyeheri Maria wa Moyo Mtakatifu (1863-1899), kutoka Chama cha Kitawa cha Mchungaji Mwema huko Ujerumani, aliisisimkia sana ibada hii baada ya kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Yesu na akawahi hata kumwomba Papa Leo XIII, autolee ulimwengu wote kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kama alivyotumwa na Yesu.

Wakati wa kipindi cha enzi ya kati, watangulizi wa ibada hii mpya, walijitokeza kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu wa Kanisa Katoliki na kuifanya ishike kasi na kujulikana sana katika Kanisa hilo.

Asili ya Ibada: Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni maendelezo ya Ibada ya ‘Ubinadamu Mtakatifu wa Kristo.’ Uhuishaji wa maisha ya Kitawa na ari ya Mtakatifu Bernard wa Klervo na ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi katika Karne ya 12 na 13, pamoja na shauku ya wapiganaji wa vita vya Msalaba waliorudi kutoka Nchi Takatifu, walianzisha Ibada ya Mateso ya Kristo hasa ya Vidonda vyake Vitakatifu na zaidi sana lile donda la Ubavuni mwa Yesu.

Ibada hii ya Mateso ya Kristo ilishughulikiwa zaidi na vikundi vya Kitawa vya Wafransiskani ikishabikiwa sana na Mtakatifu Bonaventura pamoja na Mtakatifu Jean Eudes (1602 -1680). Kwa asili, kulikuwa na ibada mbili zilizoungana, ibada ya Moyo Safi wa Maria, na nyingine ya Moyo wa Yesu. Lakini polepole, ibada hizi mbili zilitenganishwa na tarehe 31 Agosti, 1670 kwa mara ya kwanza kabisa kulikuwa na sherehe ya pekee ya Moyo Makatifu wa Yesu katika shule ya Seminari ya Rennes huko Ufaransa.

Watakatifu wanaohusiana na Moyo Mtakatifu wa Yesu:
Mtakatifu Lutgarda (1246): Vyanzo vya kihistoria ya Kanisa, vinasema kuwa Yesu alimtokea Lutgarda na akamwambia amwombe neema yoyote aitakayo. Yeye akaomba uelewa wa lugha ya Kilatini ili asaidiwe katika kuyaelewa maandiko.Akapewa, lakini aliona bado anakosa kitu. Akamwomba Yesu wabadilishane mioyo. Yesu akakubali na kuanzia hapo  Lutgarda alikuwa na ibada ya pekee kwa Moto Mtakatifu wa Yesu.

Mtakatifu Mektildis Mkubwa (1298): Yesu alimtokea na akamwamuru Mektildis ampende na aupende moyo wake katika Sakramenti ya altare; naye akafanya kama Yesu alinyokuwa amemwamuru. Mtakatifu huyu alikuwa kati ya wale wa kwanza kabisa kuwa na ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Mtakatifu Margareta Maria   Alakok (1647-1690): Kama ilivyokwisha kudokezwa  Margareta Maria Alakok ndiye aliyekuwa mwelekezi wa ibada hii na kuifanya kama ilivyo sasa. Maelekezo kuhusu upokeaji wa Komunyo, Ibada ya Ijumaa ya kwanza ya mwezi , kuabudu Ekaristi Takatifu  kwa saa moja kila siku ya Alhamisi, na kusherehekea sikukuu ya Moyo Mtakatifu yalikuwa baadhi ya maelekezo ya Margarata Maria Alakok.

Estelle Faquette: Alipewa Skapulari ya Moyo Mtakatifu wa Yesu tarehe 9/9/1876 na Mama Bikira Maria na akaruhusiwa na Askofu wake Mkuu kutengeneza nyingi zaidi na kuwagawia waamini wengine ilipofika tarehe 12/12/1876.

Mwenyeheri Maria wa Moyo Mtakatifu (1863-1899): Tarehe 10/6/1898 Maria alipewa ujumbe na Yesu wa kumpelekea Papa Leo X111 kumwambia autolee ulimwengu wote kwa Moyo Mtakatifu wa  Yesu. Kwa kuwa  Papa hakuutilia maanani ujumbe ule wala hakuuamini, tarehe 6/1/1889 alipelekewa ujumbe mwingine tena wa kumwambia kuwa Ijumaa za Kwanza za kila mwezi ziwe kwa ajili ya Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Tarehe 9/6/1899  Papa Leo akatekeleza maagizo ya kuutolea ulimwengu wote kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Kibali cha Kipapa: Baada ya kifo cha Margareta Maria Alakok, mashirika ya Kitawa tu ndiyo yaliyoruhusiwa na Roma kuadhimisha misa maalum kwa heshima ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Lakini kuanzia mwaka 1856, Papa Pius 1X aliiruhusu Kanisa Katoliki kwa jumla kuadhimisha misa maalum kwa heshima ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Papa Pius X aliamuru ile ibada ya kuutolea ulimwengu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu iliyofanywa kwanza na Papa Leo X111 irudiwe kila mwaka. Papa Pius X1, katika Waraka wake wa Kipapa wa tarehe 8 Mei, 1928 akiri kuwa ni kweli Yesu alikuwa amejidhihirisha mwenyewe alipomtokea Margareta Maria Alakok na kutoa ahadi za neema kwa wale watakaouheshimu moyo wake. Waraka wa Papa ulikuwa unarudia tena na tena yale mazungumzo kati ya Yesu na Mtakatifu Margareta yakithibitisha umhimu wa kuuheshimu Moyo huo wa Yesu kwa fidia ya dhambi zetu.

Siku ya kumbukumbu ya miaka 100 ya kuanzishwa kwa sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu iliyozinduliwa na Papa Pius IX, Papa Pius X11 aliwaeleza Wakatoliki wote kwa kinaganaga sana kuhusu ibada hii katika Waraka wake wa Kipapa wa tarehe 15 Mei, 1956.

Ukosoaji kuhusu utoaji heshima kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu: Wakristo wa madhehebu ya Kiorthodoksi ya Mashariki wanaikosoa ibada hii wakisema kuwa imeuweka mno Moyo wa Yesu isivyostahili katika hali ya ubinadamu. Papa Pius X11 katika moja ya Barua zake aliujibu ukosoaji huo kwamba Moyo Mtakatifu wa Yesu unaheshimiwa kwa mujibu wa Nafsi Takatifu ya Neno la kudumu milele na pia kama alama ya mapendo yake inayoonekana ambayo ni ushahidi wa wokovu wetu.
             

0754 054 004 kwa msaada wa mtandao.           

Comments

  1. MOYO MT. WA YESU KRISTO WA NAZAZRETH NI UKAMILIFU WA MAPENDO YA MUNGU BABA
    tumwendee Yesu wa Huruma by Aloisius Daniel Ukweli utaponya majeraha ya jamii ya kikristo na jamii nyingine,Yesu anasisitiza TUWE WAKWELI ,TUISHI UKWELI,TUWAPE WATU UKWELI ILI WAUISHI UKWELI amina kwa jina la Yesu Mwana wa Mungu aliye hai.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)