LAZIMA USALAMA WA CHAKULA UZINGATIWE
Ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula ni kikwazo kikubwa katika mchakato wa maendeleo endelevu na kwamba, chakula hupotea katika hatua mbali mbali tangu kinapozalishwa hadi kumfikia mlaji wa mwisho. Upotevu wa chakula una madhara makubwa kwa wakulima wadogo wadogo, ambao kwa kiasi kikubwa maisha na ustawi wao unategemea uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kupambana na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula haina budi kuwekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo ya kilimo cha kisasa; kwa kuboresha miundo mbinu ya barabara na maghala ya kuhifadhia chakula vijijini; kwa kuwa na usafiri wenye uhakika; soko, mafunzo makini ya kilimo endelevu pamoja na kuwapatia wakulima pembejeo za kilimo. Mkakati huu unalenga pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhakika wa usalama wa chakula sanjari na kupunguza upotevu wa chakula.
Lakini, ikumbukwe kwamba, uhakika wa usalama wa chakula kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko ni suala la kimaadili na kiutu na wala si tu changamoto ya kiuchumi na kiteknolojia. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhakika wa usalama wa chakula kwa wote, kwa kuwaheshimu watu ili waweze kutumia rasilimali iliyopo kujipatia chakula sanjari na kuhakikisha usalama na ubora wa chakula.
Ili kufikia lengo hili, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na sera na mipango thabiti, ili kuhakikisha kwamba, hakuna chakula kinachopotea katika mchakato mzima wa uzalishaji hadi kinapomfikia mlaji mezani, kwani sehemu kubwa ya tatizo hili si binadamu bali soko! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano wa 154 wa Baraza la Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Jumatatu, tarehe 30 Mei 2016.
Kardinali Tagle anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ili kweli rasilimali ya dunia iweze kuleta mafao ya wengi, kwa kuwa na mwelekeo mpya wa kijamii unaozingatia haki msingi za binadamu; mafao ya wengi; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Caritas Internationalis inasema, chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu.
Kumbe, wakulima wadogo wadogo wanapaswa kujengewa uwezo kwa kupewa mtaji na pembejeo pamoja na mafunzo ya kilimo cha kisasa na endelevu. Serikali mbali mbali hazina budi kuendeleza mchakato wa uragibishaji ili kuhakikisha kwamba, mchakato mzima wa uzalishaji, usambazaji, ulaji na masoko, ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa wakulima wadogo wadogo kwa sababu wao ndio wanaolisha sehemu kubwa ya umati wa dunia. Sera za uzalishaji wa chakula hazina budi kuzingatia tunu msingi za maisha ya binadamu katika kazi, ili kulinda na kudumisha haki kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wengi.
Caritas Internationalis inasema, Kanisa sehemu mbali mbali za dunia limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo kwa kuwapatia mitaji kwa njia ya vyama vya ushirika na mikopo. Udhibiti wa upotevu wa chakula unajikita mwono wa maendeleo ya binadamu na ekolojia na wala si tu suala la suluhu ya kiufundi. Kanisa linapenda kuwekeza kati ya maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu; kwa kuheshimu mazingira, binadamu na ustawi wake pamoja na kuhakikisha kwamba, sekta ya kilimo inasaidia kuzalisha fursa za ajira. Yote haya yanapania kujenga na kudumisha haki jamii, umoja na mshikamano wa kidugu unaowaambata wote bila ubaguzi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment